Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 51

Mauaji Kwenye Sherehe ya Sikukuu ya Kuzaliwa

Mauaji Kwenye Sherehe ya Sikukuu ya Kuzaliwa

MATHAYO 14:1-12 MARKO 6:14-29 LUKA 9:7-9

  • HERODE AAGIZA YOHANA MBATIZAJI AKATWE KICHWA

Mitume wa Yesu wanapohubiri huko Galilaya, mtu aliyemtambulisha Yesu hana uhuru kama huo. Yohana Mbatizaji amekuwa gerezani kwa miaka miwili hivi.

Yohana alikuwa amesema hadharani kwamba ni kosa kwa Mfalme Herode Antipa kumchukua Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake wa kambo, awe mke wake. Herode alikuwa amemtaliki mke wake wa kwanza ili amwoe Herodia. Kulingana na Sheria ya Musa, ambayo Herode anadai kufuata, ndoa hiyo ni ya uzinzi na si halali. Yohana anapomkemea, Herode anamtupa gerezani, labda baada ya kuhimizwa na Herodia afanye hivyo.

Herode hajui amchukulie Yohana hatua gani kwa sababu watu ‘wanamwona kuwa nabii.’ (Mathayo 14:5) Hata hivyo, Herodia hana wasiwasi kama huo. Herodia ‘ana kinyongo kumwelekea Yohana’ na anatafuta njia ya kufanya auawe. (Marko 6:19) Hatimaye, nafasi inapatikana.

Muda mfupi kabla ya Pasaka ya mwaka 32 W.K., Herode anapanga sherehe kubwa kwa ajili ya sikukuu yake ya kuzaliwa. Maofisa wote wa cheo cha juu wa Herode, maofisa wa jeshi, na watu wote mashuhuri wa Galilaya wanakuja kwenye sherehe hiyo. Wakati wa sherehe hiyo, Salome, binti ya Herodia na Filipo, mume wake wa kwanza, anatumwa kuwachezea dansi wageni. Watu wanafurahishwa sana na jinsi anavyocheza.

Herode anafurahishwa sana na binti yake wa kambo, basi anamwambia: “Niombe chochote unachotaka, nami nitakupa.” Hata anaapa hivi: “Chochote utakachoomba nitakupa, hata ikiwa ni nusu ya ufalme wangu.” Kabla ya kujibu, Salome anaenda kumuuliza mama yake: “Niombe nini?”—Marko 6:22-24.

Hii ndiyo fursa ambayo Herodia amekuwa akitafuta! Bila kusita anamwambia: “Kichwa cha Yohana Mbatizaji.” Mara moja Salome anarudi kwa Herode na kutoa ombi lake: “Nataka unipe sasa hivi kwenye sinia kichwa cha Yohana Mbatizaji.”—Marko 6:24, 25.

Jambo hilo linamhuzunisha sana Herode, lakini tayari wageni wake wamesikia kiapo chake kwa Salome. Anaaibika kutotimiza kiapo hicho, licha ya kwamba kitamaanisha kumuua mwanamume asiye na hatia. Basi Herode anamtuma mlinzi gerezani akatekeleze mauaji hayo. Muda si muda, mlinzi anarudi akiwa na kichwa cha Yohana kwenye sinia. Anampatia Salome, naye anampelekea mama yake.

Wanafunzi wa Yohana wanaposikia jambo lililotukia, wanakuja na kuutoa mwili wake kisha wanauzika. Baada ya hapo, wanamjulisha Yesu jambo hilo.

Baadaye, Herode anaposikia jinsi Yesu anavyowaponya watu na kuwafukuza roho waovu, anakuwa na wasiwasi. Anajiuliza ikiwa mtu anayefanya mambo hayo—Yesu—ni Yohana Mbatizaji ambaye sasa “amefufuliwa kutoka kwa wafu.” (Luka 9:7) Basi Herode Antipa anatamani sana kumwona Yesu. Si kwa sababu angependa kusikia Yesu akihubiri. Bali Herode anataka kumwona Yesu ili ahakikishe kwamba yeye ni Yohana au la.