Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 106

Mifano Miwili Kuhusu Mashamba ya Mizabibu

Mifano Miwili Kuhusu Mashamba ya Mizabibu

MATHAYO 21:28-46 MARKO 12:1-12 LUKA 20:9-19

  • MFANO KUHUSU WANA WAWILI

  • MFANO WA WAKULIMA WA SHAMBA LA MIZABIBU

Akiwa hekaluni, Yesu ametoka kuwashangaza wakuu wa makuhani na wazee wa watu, ambao walikuwa wamemuuliza kuhusu mamlaka anayotumia kufanya mambo. Jibu la Yesu linawanyamazisha. Kisha anatoa mfano unaofunua jinsi walivyo kihalisi.

Yesu anasimulia hivi: “Mtu fulani alikuwa na watoto wawili. Akamwendea wa kwanza, akamwambia, ‘Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ Akamjibu, ‘Sitaenda,’ lakini baadaye akajuta na akaenda. Akamwendea wa pili na kumwambia jambo hilohilo. Naye akamjibu, ‘Nitaenda Baba,’ lakini hakwenda. Kati ya hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya baba yake?” (Mathayo 21:28-31) Jibu ni wazi—yule wa kwanza ndiye ambaye mwishowe alifanya mapenzi ya baba yake.

Basi, Yesu anawaambia hivi wapinzani wake: “Kwa kweli ninawaambia wakusanya kodi na makahaba wanawatangulia ninyi kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Mwanzoni, wakusanya kodi na makahaba hawakutaka kumtumikia Mungu. Hata hivyo, kama yule mwana wa kwanza, baadaye walitubu na sasa wanamtumikia Mungu. Kinyume chake, viongozi wa kidini ni kama yule mwana wa pili, wanadai kwamba wanamtumikia Mungu lakini kwa kweli hawamtumikii. Yesu anasema hivi: “Yohana [Mbatizaji] alikuja kwenu katika njia ya uadilifu, lakini hamkumwamini. Hata hivyo, wakusanya kodi na makahaba walimwamini, nanyi, ijapokuwa mliona hilo, hamkujuta na kumwamini.”​—Mathayo 21:31, 32.

Baada ya kutoa mfano huo, Yesu anasimulia mfano mwingine. Pindi hii Yesu anaonyesha kwamba kosa la viongozi wa kidini sio tu kukataa kumtumikia Mungu. Kwa kweli wao ni waovu. Yesu anasimulia hivi: “Mtu fulani alipanda shamba la mizabibu akalizungushia ua, akachimba shinikizo la divai, akajenga mnara, kisha akalikodisha kwa wakulima, naye akasafiri kwenda ng’ambo. Majira yalipofika akatuma mtumwa kwa wakulima ili achukue kutoka kwao baadhi ya matunda ya shamba la mizabibu. Lakini wakamkamata, wakampiga na kumfukuza mikono mitupu. Akamtuma tena mtumwa mwingine kwao, na huyo wakampiga kichwani na kumwaibisha. Akamtuma mwingine, na huyo wakamuua, akawatuma wengine wengi, wakawapiga baadhi yao na kuwaua wengine.”—Marko 12:1-5.

Je, wale wanaomsikiliza Yesu wataelewa mfano huo? Huenda wakakumbuka maneno haya ya shutuma yaliyosemwa na Isaya: “Shamba la mizabibu la Yehova wa majeshi ni nyumba ya Israeli; watu wa Yuda ndilo shamba alilolipenda sana. Aliendelea kutumaini haki itendwe, lakini tazama! kulikuwa na ukosefu wa haki.” (Isaya 5:7) Mfano wa Yesu unafanana na maneno hayo. Yehova ndiye anayemiliki shamba, nalo shamba la mizabibu ni taifa la Israeli, ambalo limezunguzishiwa ua na kulindwa na Sheria ya Mungu. Yehova aliwatuma manabii wawafundishe watu wake na kuwasaidia wazae matunda mazuri.

Hata hivyo, “wakulima” waliwatendea vibaya na kuwaua “watumwa” waliotumwa kwao. Yesu anaeleza hivi: “[Mwenye shamba la mizabibu] alikuwa na mmoja zaidi, mwana wake mpendwa. Mwishowe akamtuma kwao akisema: ‘Watamheshimu mwanangu.’ Lakini wakulima wakaambiana, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, na urithi utakuwa wetu.’ Kwa hiyo wakamkamata, wakamuua.”—Marko 12:6-8.

Sasa Yesu anauliza: “Mwenye shamba la mizabibu atafanya nini?” (Marko 12:9) Viongozi wa kidini wanajibu: “Kwa sababu ni waovu, atawaangamiza kabisa na kulikodisha shamba la mizabibu kwa wakulima wengine, ambao watampa matunda yatakapoiva.”—Mathayo 21:41.

Hivyo, bila kujua wanajihukumu wao wenyewe, kwa maana wao ni kati ya “wakulima” wa “shamba la mizabibu” la Yehova, taifa la Israeli. Matunda ambayo Yehova anatazamia kutoka kwa wakulima hao yanatia ndani kumwamini Mwana wake, yaani, Masihi. Yesu anawatazama moja kwa moja viongozi hao wa kidini na kusema: “Je, hamkusoma kamwe andiko hili: ‘Jiwe ambalo wajenzi walilikataa, limekuwa jiwe kuu la pembeni. Hili limetoka kwa Yehova, na ni lenye kustaajabisha machoni petu’?” (Marko 12:10, 11) Kisha Yesu anakazia jambo kuu: “Ndiyo sababu ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa taifa linalozaa matunda yake.”—Mathayo 21:43.

Waandishi na wakuu wa makuhani wanatambua kwamba “mfano aliosema uliwahusu.” (Luka 20:19) Kuliko wakati mwingine wowote, wanataka kumuua yule aliye na haki ya kuwa “mrithi.” Lakini wanauogopa umati, ambao unamwona Yesu kuwa nabii, basi hawajaribu kumuua wakati huo.