Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 134

Kaburi Tupu​—Yesu Yuko Hai!

Kaburi Tupu​—Yesu Yuko Hai!

MATHAYO 28:3-15 MARKO 16:5-8 LUKA 24:4-12 YOHANA 20:2-18

  • YESU AFUFULIWA

  • MATUKIO KWENYE KABURI LA YESU

  • AWATOKEA WANAWAKE KADHAA

Wale wanawake wanashtuka sana wanapokuta kaburi likiwa tupu! Maria Magdalene anakimbia kwenda kwa “Simoni Petro na yule mwanafunzi mwingine, ambaye Yesu alimpenda,” yaani, mtume Yohana. (Yohana 20:2) Hata hivyo, wale wanawake wengine walio kwenye kaburi wanamwona malaika. Na ndani ya kaburi kuna malaika mwingine, ambaye “amevaa kanzu nyeupe.”—Marko 16:5.

Mmoja wa wale malaika anawaambia hivi: “Msiogope, kwa maana ninajua mnamtafuta Yesu aliyeuawa kwenye mti. Hayupo hapa, kwa maana amefufuliwa kama alivyosema. Njooni, tazameni mahali alipokuwa amelala. Basi nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba alifufuliwa kutoka kwa wafu, na tazama! anawatangulia kwenda Galilaya.” (Mathayo 28:5-7) Basi wale wanawake “wakitetemeka huku wakiwa wamelemewa na hisia,” wanakimbia kwenda kuwajulisha wanafunzi.—Marko 16:8.

Kufikia sasa, Maria amewapata Petro na Yohana. Akiwa anahema, anawaambia: “Wamemwondoa Bwana kaburini, nasi hatujui wamemlaza wapi.” (Yohana 20:2) Petro na Yohana wanaondoka mbio. Yohana anakimbia haraka zaidi naye anafika kwenye kaburi kwanza. Anachungulia ndani na kuviona vitambaa, lakini haingii ndani.

Petro anapofika, anaingia ndani moja kwa moja. Anaona vitambaa vya kitani na kitambaa kilichotumiwa kufunga kichwa cha Yesu. Sasa Yohana anaingia ndani naye anaamini ripoti ya Maria. Licha ya mambo ambayo Yesu alikuwa amesema, hakuna yeyote kati yao anayetambua kwamba amefufuliwa. (Mathayo 16:21) Wanarudi nyumbani wakiwa wamechanganyikiwa. Lakini Maria, ambaye amerudi kwenye kaburi, anabaki hapo.

Wakati huohuo, wale wanawake wengine wako njiani kwenda kuwajulisha wanafunzi kwamba Yesu amefufuliwa. Wakiwa wanakimbia kwenda kuwajulisha, Yesu anakutana nao na kusema: “Siku njema!” Wanaanguka miguuni pake na “kumsujudia.” Kisha Yesu anasema: “Msiogope! Nendeni, mkawajulishe ndugu zangu ili waende Galilaya, na huko wataniona.”—Mathayo 28:9, 10.

Hapo awali, kulipokuwa na tetemeko la ardhi na malaika wakatokea, wanajeshi waliokuwa kaburini ‘walitetemeka, wakawa kama wafu.’ Baada ya kurudiwa na nguvu, waliingia jijini na “kuwajulisha wakuu wa makuhani mambo yote yaliyotokea.” Kisha makuhani wakashauriana na wazee wa Wayahudi. Wakaamua kuwahonga wanajeshi hao ili wafiche jambo hilo na waseme: “Wanafunzi wake walikuja usiku wakamwiba tulipokuwa tumelala usingizi.”—Mathayo 28:4, 11, 13.

Wanajeshi Waroma wanaweza kuuawa ikiwa watalala wanapolinda, basi makuhani wanawaahidi hivi: “Na gavana akisikia [uwongo wao kwamba walikuwa wamelala], sisi tutamwelezea jambo hilo, nanyi hamtahitaji kuwa na wasiwasi.” (Mathayo 28:14) Wanajeshi wanachukua hongo na kufanya kama wanavyoambiwa na makuhani. Basi habari za uwongo kwamba mwili wa Yesu uliibiwa zinaenea sana kati ya Wayahudi.

Bado Maria Magdalene anaomboleza kaburini. Anapoinama na kuchungulia ndani ya kaburi, anawaona malaika wawili wakiwa wamevaa mavazi meupe! Mmoja ameketi mahali ambapo kichwa cha Yesu kilikuwa kimelazwa na mwingine miguuni. Wanamuuliza: “Mwanamke, kwa nini unalia?” Maria anawajibu: “Wamemwondoa Bwana wangu, nami sijui wamemlaza wapi.” Maria anapogeuka anamwona mtu mwingine. Mtu huyo anarudia swali walilouliza malaika na kuongezea hivi: “Unamtafuta nani?” Akifikiri kwamba ni mtunza-bustani, Maria anasema: “Bwana, ikiwa umemchukua, niambie umemlaza wapi, nami nitamwondoa.”—Yohana 20:13-15.

Kwa kweli, Maria anazungumza na Yesu aliyefufuliwa, lakini pindi hiyo hamtambui. Hata hivyo, Yesu anaposema, “Maria!” anamtambua kupitia njia ambayo amekuwa akizungumza naye. Maria anasema hivi kwa shangwe: “Raboni!” (maana yake “Mwalimu!”) Lakini akiogopa kwamba Yesu yuko karibu kupaa mbinguni, Maria anamshika. Basi Yesu anamwambia hivi: “Acha kuning’ang’ania, kwa maana bado sijapanda kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu, nawe uwaambie, ‘Ninapanda kwenda kwa Baba yangu na Baba yenu na kwa Mungu wangu na Mungu wenu.’”—Yohana 20:16, 17.

Maria anakimbia kwenda mahali ambapo mitume na wale wanafunzi wengine wamekusanyika. Anawaambia hivi: “Nimemwona Bwana!” na hivyo kuongezea simulizi lake kwenye mambo ambayo wamesikia kutoka kwa wale wanawake wengine. (Yohana 20:18) Ingawa hivyo, ‘wanayaona maneno hayo kama upuuzi.’—Luka 24:11.