Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 25

Maskani ya Ibada

Maskani ya Ibada

Musa alipokuwa kwenye Mlima Sinai Yehova alimwambia ajenge hema la pekee linaloitwa maskani, ambapo Waisraeli wangemwabudu Mungu. Wangeweza kuibeba maskani waliposafiri.

Yehova alisema hivi: ‘Waambie watu watoe michango ya kujenga maskani.’ Waisraeli wakatoa dhahabu, fedha, shaba, mawe yenye thamani, na vito. Pia walitoa sufu, vitambaa vya kitani, ngozi za wanyama, na vitu vingine vingi. Walitoa kwa ukarimu sana hivi kwamba Musa akalazimika kuwaambia hivi: ‘Tumepata michango ya kutosha! Msilete zaidi.’

Wanaume na wanawake wengi wenye ustadi walisaidia kujenga maskani. Yehova aliwapa hekima ili waweze kufanya kazi hiyo. Wengine walisokota nyuzi, wakatengeneza mavazi, au wakafanya kazi ya mtarizi. Wengine walifanya kazi kwa kutumia mawe, dhahabu, na mbao.

Watu wakajenga maskani kama tu Yehova alivyokuwa amewaambia. Wakaweka pazia maridadi ili kutenganisha maskani katika sehemu mbili, Patakatifu na Patakatifu Zaidi. Katika Patakatifu Zaidi kulikuwa na sanduku la agano lililotengenezwa kwa mbao za mshita na dhahabu. Katika Patakatifu kulikuwa na kinara cha taa cha dhahabu, meza, na madhabahu ya kufukiza uvumba. Katika ua kulikuwa na beseni ya shaba na madhabahu kubwa. Sanduku la agano liliwakumbusha Waisraeli kuhusu ahadi yao ya kumtii Yehova. Je, unajua agano ni nini? Ni ahadi ya pekee sana.

Yehova alichagua Haruni na wanawe wafanye kazi kwenye maskani wakiwa makuhani. Walipaswa kuitunza na kumtolea Yehova dhabihu. Ni Haruni peke yake ambaye aliruhusiwa kuingia Patakatifu Zaidi kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa kuhani mkuu. Aliingia humo mara moja kwa mwaka ili kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake, dhambi za familia yake, na dhambi za taifa lote la Israeli.

Waisraeli walikamilisha ujenzi wa maskani mwaka mmoja baada ya kutoka Misri. Sasa walikuwa na mahali pa kumwabudu Yehova.

Yehova akaijaza maskani utukufu wake na akafanya wingu litande juu yake. Wingu lilipoendelea kukaa juu ya maskani, Waisraeli hawakuondoka mahali walipokuwa wamepiga kambi. Lakini wingu lilipoinuka, walijua ni wakati wa kuondoka. Wangebomoa maskani na kufuata wingu hilo.

“Ndipo nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha ufalme ikisema: ‘Tazama! Hema la Mungu liko pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Na Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.’”​—Ufunuo 21:3