Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 30

Rahabu Awaficha Wapelelezi

Rahabu Awaficha Wapelelezi

Wapelelezi Waisraeli walipoenda kwenye jiji la Yeriko, walikaa katika nyumba ya mwanamke anayeitwa Rahabu. Mfalme wa Yeriko akatambua jambo hilo na kuwatuma askari kwenye nyumba ya Rahabu. Lakini Rahabu akawaficha wapelelezi hao wawili kwenye dari la nyumba yake na kuwaelekeza askari upande mwingine. Kisha Rahabu akawaambia wapelelezi hao hivi: ‘Nitawasaidia kwa sababu ninajua kwamba Yehova yuko upande wenu na kwamba mtaishinda nchi hii. Tafadhali mniahidi kwamba mtaiokoa familia yangu.’

Wapelelezi wakamwambia Rahabu hivi: ‘Tunaahidi kwamba hakuna mtu ndani ya nyumba yako atakayeumia. Funga kamba nyekundu dirishani, na watu wa familia yako wataokolewa.’

Rahabu akawashusha wapelelezi hao kwa kamba kupitia dirisha lake. Wakaenda milimani na kujificha kwa siku tatu kabla ya kurudi kwa Yoshua. Kisha Waisraeli wakavuka Mto Yordani na kujitayarisha kuishinda nchi. Yeriko lilikuwa jiji la kwanza waliloshinda. Yehova aliwaambia wapige mwendo kulizunguka jiji mara moja kila siku kwa siku sita. Siku ya saba, walipiga mwendo kulizunguka jiji mara saba. Kisha makuhani wakapiga tarumbeta, nao askari wakapaaza sauti kwa kelele kadiri walivyoweza. Kuta za jiji hilo zikaanguka chini! Lakini nyumba ya Rahabu, ambayo ilikuwa kwenye ukuta, ikaendelea kusimama. Rahabu na familia yake wakaokolewa kwa sababu alimtegemea Yehova.

“Vivyo hivyo, je, Rahabu . . . hakutangazwa pia kuwa mwadilifu kwa matendo, baada ya kuwakaribisha wale wajumbe na kuwatoa nje kupitia njia nyingine?”​—Yakobo 2:25