Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 32

Kiongozi Mpya na Wanawake Wawili Jasiri

Kiongozi Mpya na Wanawake Wawili Jasiri

Baada ya kuwaongoza watu wa Yehova kwa miaka mingi, Yoshua alikufa akiwa na umri wa miaka 110. Kwa muda wote ambao Yoshua alikuwa hai, Waisraeli walimtumikia Yehova. Lakini baada ya Yoshua kufa walianza kuabudu sanamu, kama vile Wakanaani walivyofanya. Kwa sababu Waisraeli hawakuendelea kumtii, Yehova alimruhusu mfalme Yabini wa Kanaani awakandamize. Watu walimlilia Yehova ili kupata msaada. Kwa hiyo, Yehova akamchagua kiongozi mpya aliyeitwa Baraka. Kiongozi huyo angewasaidia watu wamrudie Yehova.

Debora, nabii wa kike, alimwomba Baraka aje. Alikuwa na ujumbe huu kutoka kwa Yehova: ‘Chukua wanaume 10,000, na uende kupigana na jeshi la Yabini katika bonde la mto Kishoni. Huko utamshinda Sisera, mkuu wa jeshi la Yabini.’ Baraka akamwambia Debora hivi: ‘Nitaenda ikiwa tu utaandamana nami.’ Debora akamjibu: ‘Nitaenda pamoja nawe. Lakini ujue kwamba, wewe hutamuua Sisera. Yehova amesema kwamba mwanamke ndiye atakayemuua.’

Debora alienda pamoja na Baraka na jeshi lake katika Mlima Tabori ili kujiandaa kwa ajili ya vita. Mara moja baada ya Sisera kusikia kuhusu jambo hilo, alikusanya magari ya vita na jeshi lake katika bonde lililokuwa mbele yao. Debora akamwambia Baraka hivi: ‘Leo ni siku ambayo Yehova atakupa ushindi.’ Baraka na wanaume wake 10,000 walishuka kutoka mlimani ili kukutana na jeshi lenye nguvu la Sisera.

Kisha, Yehova akafanya kuwe na mafuriko katika bonde la Kishoni. Magari ya vita ya Sisera yalikwama kwenye matope. Sisera alishuka kwenye gari lake na kuanza kukimbia. Baraka na wanajeshi wake walilishinda jeshi la Sisera, lakini Sisera akatoroka! Alikimbia na kujificha katika hema la mwanamke aliyeitwa Yaeli. Mwanamke huyo alimpa maziwa anywe, kisha, akamfunika kwa blanketi. Shujaa huyo aliyechoka akalala usingizi. Kisha, Yaeli akaingia mahali alipolala na kumpigilia kigingi cha hema kichwani. Naye akafa.

Baraka alifika akiwa anamtafuta Sisera. Yaeli alitoka nje ya hema na kumwambia hivi: ‘Ingia ndani nikuonyeshe mwanamume unayemtafuta.’ Baraka aliingia ndani na kukuta Sisera akiwa amekufa. Baraka na Debora wakamsifu Yehova kwa wimbo kwa sababu alikuwa amewapa Waisraeli ushindi dhidi ya adui zao. Kwa miaka 40 iliyofuata, Waisraeli waliishi kwa amani.

“Wanawake wanaotangaza habari njema ni jeshi kubwa.”​—Zaburi 68:11