Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 41

Daudi na Sauli

Daudi na Sauli

Baada ya Daudi kumuua Goliathi, Mfalme Sauli akamweka Daudi asimamie jeshi lake. Daudi alishinda vita vingi, naye akajulikana na kusifiwa na watu wengi. Wakati wowote ambapo Daudi alirudi nyumbani, wanawake wangetoka nje wakicheza dansi na kuimba: ‘Sauli amepiga maelfu yake, na Daudi amepiga makumi ya maelfu yake!’ Sauli akaanza kumwonea Daudi wivu na akataka kumuua.

Daudi alijua kupiga kinubi vizuri sana. Naye alikuwa na kawaida ya kumpigia Sauli muziki. Siku moja Daudi alipokuwa akipiga kinubi, Sauli alimrushia mkuki. Daudi akakwepa kabla tu ya mkuki kumpata nao ukapiga ukuta. Baada ya hapo, Sauli akajaribu mara nyingi zaidi kumuua Daudi. Mwishowe, Daudi akakimbia na kujificha nyikani.

Sauli akachukua jeshi la watu 3,000 na kwenda kumwinda Daudi. Sauli akaingia ndani ya pango ambamo Daudi na wanaume wake walikuwa wakijificha. Wanaume hao wakamwambia Daudi kwa sauti ya chini: ‘Hii ndiyo nafasi yako ya kumuua Sauli.’ Daudi akamnyemelea Sauli na kukata koti lake. Sauli hakutambua. Baadaye, Daudi akahisi vibaya kwa sababu alikuwa amemvunjia heshima mfalme mtiwa-mafuta wa Yehova. Hakuwaruhusu wanaume wake wamshambulie Sauli. Hata alimwambia Sauli kwamba alikuwa amepata nafasi ya kumuua lakini hakufanya hivyo. Je, Sauli alibadili nia yake kumwelekea Daudi?

Hapana. Sauli aliendelea kumwinda Daudi. Usiku mmoja Daudi na mpwa wake Abishai wakaingia kimyakimya kwenye kambi ya Sauli. Hata Abneri, mlinzi wa Sauli, alikuwa amelala. Abishai akasema: ‘Hii ndiyo nafasi yetu! Niruhusu nimuue.’ Daudi akajibu: ‘Yehova atamwadhibu Sauli. Acha tuchukue mkuki wake na gudulia lake la maji tuondoke.’

Daudi akapanda juu ya mlima uliokuwa karibu na kambi ya Sauli. Akasema kwa sauti kubwa: ‘Abneri, kwa nini hukumlinda mfalme? Uko wapi mkuki wa Sauli na gudulia lake la maji?’ Sauli akatambua sauti ya Daudi na kusema: ‘Ungeweza kuniua, lakini hukufanya hivyo. Ninajua kwamba utakuwa mfalme anayefuata wa Israeli.’ Sauli akarudi kwenye jumba lake la kifalme. Lakini si wote katika familia ya Sauli waliomchukia Daudi.

“Ikiwezekana, kwa kadiri inavyowategemea ninyi, fanyeni amani na watu wote. Wapendwa, msijilipizie kisasi bali iachieni nafasi ghadhabu.”​—Waroma 12:18, 19