Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 90

Yesu Afa huko Golgotha

Yesu Afa huko Golgotha

Wakuu wa makuhani wakamchukua Yesu na kumpeleka kwenye jumba la gavana. Pilato akawauliza hivi: ‘Mna mashtaka gani dhidi ya mwanamume huyu?’ Wakasema hivi: ‘Anadai kwamba yeye ni mfalme!’ Pilato akamwuliza Yesu, “Je, wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu: “Ufalme wangu si sehemu ya ulimwengu huu.”

Kisha Pilato akamtuma Yesu kwa Herode, mtawala wa Galilaya, aone ikiwa angepata kosa lolote juu yake. Herode hakuweza kupata jambo lolote la kumshtaki Yesu na hivyo akamtuma tena kwa Pilato. Kisha Pilato akawaambia watu hivi: ‘Mimi wala Herode hatujapata kosa lolote dhidi ya mwanamume huyu. Nitamwachilia huru.’ Umati ukapiga kelele na kusema: ‘Muue! Muue!’ Askari wakampiga Yesu kwa mjeledi, wakamtemea mate, na kumpiga ngumi. Wakamvisha taji la miiba juu ya kichwa chake na kumdhihaki wakisema, “Siku njema, ewe Mfalme wa Wayahudi.” Pilato akawaambia watu tena: ‘Sijaona kosa lolote juu ya mtu huyu.’ Lakini wakapiga kelele na kusema: “Mtundike mtini!” Hivyo, Pilato akamtoa ili akauawe.

Wakampeleka Yesu mahali panapoitwa Golgotha, wakampigilia misumari kwenye mti na kisha wakainua mti huo. Yesu akasali hivi: ‘Baba, wasamehe kwa kuwa hawajui wanachokifanya.’ Watu wakamdhihaki Yesu wakisema: ‘Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka kwenye mti! Jiokoe.’

Mhalifu mmoja aliyekuwa ametundikwa kando yake akasema hivi: “Unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Yesu akamwahidi hivi: “Utakuwa pamoja nami katika Paradiso.” Ilipofika saa sita, kukawa na giza juu ya nchi kwa saa tatu. Baadhi ya wanafunzi walisimama karibu na mti huo, kutia ndani Maria mama ya Yesu. Yesu akamwambia Yohana amtunze Maria kama ambavyo angemtunza mama yake mzazi.

Mwishowe, Yesu akasema: “Imetimizwa!” Akainamisha kichwa chake na kukata pumzi. Wakati huohuo, tetemeko kubwa la nchi likatokea. Ndani ya hekalu, lile pazia zito lililotenganisha Patakatifu na Patakatifu Zaidi likararuka katikati. Ofisa-jeshi mmoja akasema: “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”

“Hata ahadi za Mungu ziwe nyingi kadiri gani, zimekuwa ‘ndiyo’ kupitia yeye.”​—2 Wakorintho 1:20