Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuomba Msamaha—Ni Njia Bora ya Kufanya Amani

Kuomba Msamaha—Ni Njia Bora ya Kufanya Amani

Kuomba Msamaha—Ni Njia Bora ya Kufanya Amani

“KUOMBA msamaha huwa na matokeo makubwa. Kunasuluhisha mapambano kwa amani, kunapatanisha mataifa yenye ugomvi, kunafanya serikali zitambue kuteseka kwa raia zao, na kuimarisha uhusiano,” akaandika Deborah Tannen, mwandishi wa vitabu vinavyouzwa sana ambaye pia ni mtaalamu wa lugha kwenye Chuo Kikuu cha Georgetown, huko Washington, D. C.

Biblia huthibitisha kwamba mara nyingi kuomba msamaha kutoka moyoni kunaweza kurudisha uhusiano uliovunjika. Kwa mfano, katika mfano wa Yesu wa mwana mpotevu, wakati mwana huyo aliporudi nyumbani na kuomba msamaha kutoka moyoni, baba yake alikuwa tayari kabisa kumkaribisha tena nyumbani. (Luka 15:17-24) Naam, kiburi hakipaswi kumzuia mtu asiombe msamaha. Bila shaka, si vigumu kwa watu wanyenyekevu kuomba msamaha.

Matokeo ya Kuomba Msamaha

Abigaili, mwanamke mwenye hekima wa Israeli la kale, anatuwekea kielelezo kinachoonyesha matokeo ya kuomba msamaha, ingawa aliomba msamaha kwa kosa la mumewe. Alipokuwa akiishi nyikani pamoja na watumishi wake, Daudi, aliyekuja kuwa mfalme wa Israeli, alilinda kondoo za Nabali, mume wa Abigaili. Hata hivyo, wakati vijana hao wa Daudi walipoomba mkate na maji, Nabali aliwafukuza na kuwatusi vibaya sana. Daudi alikasirika na kuongoza wanaume 400 hivi kwenda kumpiga Nabali na nyumba yake. Alipojua habari hiyo, Abigaili alifunga safari kwenda kumlaki Daudi. Alipomwona, Abigaili alimwangukia miguuni pake na kusema: “Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.” Kisha Abigaili akaeleza hali ilivyokuwa na kumpa Daudi zawadi ya chakula na maji. Ndipo Daudi akamwambia: “Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako.”—1 Samweli 25:2-35.

Unyenyekevu wa Abigaili pamoja na kuomba msamaha kwa sababu ya ujeuri wa mumewe, uliokoa nyumba yake. Hata Daudi alimshukuru Abigaili kwa kumzuia asimwage damu. Ingawa si Abigaili aliyemtendea Daudi na watumishi wake ubaya huo, yeye alikubali makosa ya familia yake na kufanya amani na Daudi.

Mtume Paulo pia alijua wakati wa kuomba msamaha. Pindi moja ilimbidi ajitetee mbele ya Sanhedrini, mahakama kuu ya Wayahudi. Kuhani mkuu Anania alikasirishwa sana na maneno ya unyofu ya Paulo hivyo akawaagiza wale waliokuwa wamesimama karibu naye wampige mdomoni. Ndipo Paulo akamwambia: “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa. Je, wakati uleule mmoja waketi kunihukumu kupatana na Sheria na, kwa kukiuka Sheria, waamuru nipigwe?” Watazamaji walipomshutumu Paulo kwa kumtukana kuhani wa cheo cha juu, mtume huyo alikubali kosa lake mara moja na kusema: “Akina ndugu, sikujua yeye ni kuhani wa cheo cha juu. Kwa maana imeandikwa, ‘Wewe hupaswi kusema vibaya juu ya mtawala wa watu wako.’”—Matendo 23:1-5.

Maneno ya Paulo—kwamba yule aliyekuwa amewekwa kuwa hakimu hapaswi kutumia jeuri—ni ya kweli. Hata hivyo, aliomba msamaha kwa kuwa bila kujua alizungumza na kuhani wa cheo cha juu kwa njia ambayo ingeweza kuonekana kuwa yenye kukosa heshima. * Kwa sababu Paulo aliomba msamaha, Sanhedrini ilimsikiliza. Kwa kuwa Paulo alijua mabishano yaliyokuweko kati ya washiriki wa mahakama hiyo, aliwaambia kwamba alikuwa ameshtakiwa kwa sababu aliamini ufufuo. Hivyo, mgawanyiko mkubwa ukatokea, huku Mafarisayo wakimwunga mkono Paulo.—Matendo 23:6-10.

Tunaweza kujifunza nini kutokana na vielelezo hivyo viwili vya Biblia? Katika visa vyote viwili, kuomba msamaha kwa unyofu kulifanya iwezekane kuwa na mazungumzo zaidi. Kwa hiyo, kuomba msamaha kunaweza kutusaidia kufanya amani. Naam, kukubali makosa yetu na kuomba msamaha kwa madhara tuliyofanya kunaweza kufanya iwezekane tuwe na mazungumzo yenye kujenga.

‘Lakini Sikufanya Kosa Lolote’

Tunapogundua kwamba usemi au matendo yetu yalimwudhi mtu fulani, huenda tukafikiri kwamba mtu huyo anakosa busara au anaudhika upesi. Lakini Yesu Kristo aliwashauri hivi wanafunzi wake: “Basi, ikiwa wewe unaleta zawadi yako kwenye madhabahu na huko wakumbuka kwamba ndugu yako ana jambo fulani dhidi yako, acha zawadi yako hapo mbele ya madhabahu, na uende zako; kwanza fanya amani yako na ndugu yako, na ndipo, ukiisha kurudi, toa zawadi yako.”—Mathayo 5:23, 24.

Kwa mfano, huenda ndugu akahisi kwamba umemkosea. Katika hali kama hiyo, Yesu anasema kwamba inakupasa uende na ‘kufanya amani na ndugu yako,’ iwe unahisi umemkosea au la. Kulingana na maandishi ya Kigiriki, neno ambalo Yesu alitumia hapa ‘linadokeza kupatana baada ya uadui.’ (Vine’s Expository Dictionary of Old and New Testament Words) Naam, kunapokuwa na kutoelewana kati ya watu wawili, huenda wote wakawa na makosa, kwa kuwa wote si wakamilifu na wanaweza kukosea. Kwa kawaida hali kama hiyo hutaka watu wapatane.

Jambo lililo muhimu si kujua ni nani mwenye hatia au asiye na hatia, bali ni nani atakayechukua hatua ya kwanza kufanya amani. Mtume Paulo alipoona kwamba Wakristo wa Korintho walikuwa wakiwapeleka Wakristo wenzao katika mahakama za kilimwengu kwa sababu ya kutoelewana katika mambo kama ya pesa, aliwasahihisha: “Kwa nini badala ya hivyo hamjiachi mkosewe nyinyi wenyewe? Kwa nini badala ya hivyo hamjiachi mpunjwe nyinyi wenyewe?” (1 Wakorintho 6:7) Ingawa Paulo alisema hivyo ili kuwazuia Wakristo wasipeleke wenzao katika mahakama za kilimwengu kwa sababu ya kutoelewana, kanuni ya andiko hilo ni wazi: Amani miongoni mwa waamini wenzetu ni muhimu kuliko kuthibitisha ni nani mwenye hatia au asiye na hatia. Kukumbuka kanuni hiyo hufanya iwe rahisi kuomba msamaha kwa kosa ambalo mtu anafikiri tumemfanyia.

Unyofu Unahitajiwa

Hata hivyo, watu wengine hutumia kupita kiasi maneno ya kuomba msamaha. Kwa mfano, nchini Japan, neno sumimasen, hutumiwa mara nyingi sana kuomba msamaha. Linaweza hata kutumiwa kutoa shukrani, likidokeza kwamba mtu anahisi vibaya kwa kuwa hawezi kumtendea mwenzake vile alivyomtendea. Kwa sababu neno hilo linaweza kutumika katika njia nyingi, huenda wengine wakaona kwamba linatumiwa kupita kiasi na huenda wakajiuliza kama wenye kulitumia wanafanya hivyo kwa unyofu. Maneno ya kuomba msamaha yanaweza kutumiwa kupita kiasi katika jamii nyingine pia.

Katika lugha yoyote ile, ni muhimu kuwa wanyofu tunapoomba msamaha. Maneno na sauti yetu yanapaswa kuonyesha tumesikitika kikweli. Katika Mahubiri ya Mlimani, Yesu Kristo aliwafunza wanafunzi wake hivi: “Acheni tu neno lenu Ndiyo limaanishe Ndiyo, La yenu, La; kwa maana lizidilo hayo ni kutoka kwa yule mwovu.” (Mathayo 5:37) Unapoomba msamaha, fanya hivyo kwa unyofu! Kwa mfano: Kwenye uwanja mmoja wa ndege, mtu mmoja aliyekuwa amepanga foleni kwenda kwenye meza ya kuwahudumia wasafiri aliomba msamaha sanduku lake lilipomgonga mwanamke aliyekuwa mbele yake. Dakika chache baadaye, foleni hiyo iliposonga, sanduku hilo lilimgusa tena mwanamke huyo. Kwa heshima, mtu huyo aliomba msamaha tena. Wakati mwanamke huyo alipogongwa mara nyingine, mwanamume aliyekuwa akisafiri pamoja naye alimwambia mtu huyo kwamba kama kwa kweli alitaka kusamehewa, alipaswa kuhakikisha kwamba sanduku hilo halimgusi tena mwanamke huyo. Naam, tunapoomba msamaha kwa unyofu, tunapaswa pia kujitahidi kutorudia kosa.

Ikiwa tu wanyofu, tutaomba msamaha, tukubali kosa, kisha tujitahidi kurekebisha hali kadiri tuwezavyo. Naye aliyekosewa anapaswa kuwa tayari kusamehe mkosaji mwenye kutubu. (Mathayo 18:21, 22; Marko 11:25; Waefeso 4:32; Wakolosai 3:13) Kwa kuwa wote wawili si wakamilifu, huenda isiwe rahisi sana kufanya amani. Hata hivyo, kuomba msamaha kunasaidia sana kufanya amani.

Wakati Kuomba Msamaha Hakuhitajiki

Ingawa maneno ya kuonyesha sikitiko na huzuni hutuliza aliyekosewa na kuleta amani, mtu mwenye hekima huepuka kuyatumia wakati usiofaa. Kwa mfano, tuseme unatakiwa kuomba msamaha kwa jambo linalohusiana na uaminifu wako kwa Mungu. Yesu Kristo alipokuwa duniani, “alijinyenyekeza mwenyewe akawa mtiifu hadi kifo, ndiyo, kifo juu ya mti wa mateso.” (Wafilipi 2:8) Hata hivyo, Yesu hakuomba msamaha kuhusiana na imani yake ili apunguziwe mateso. Yesu hakuomba msamaha wakati kuhani wa cheo cha juu alipomwambia hivi: “Kwa Mungu aliye hai nakuweka chini ya kiapo utuambie kama wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu!” Badala ya kuomba msamaha kwa woga, Yesu alijibu hivi kwa ujasiri: “Wewe mwenyewe umesema hilo. Lakini nawaambia nyinyi watu, Tangu sasa mtaona Mwana wa binadamu ameketi kwenye mkono wa kuume wa nguvu na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” (Mathayo 26:63, 64) Yesu hangeweza kamwe kuvunja uaminifu wake kwa Baba yake, Yehova Mungu, ili adumishe amani na kuhani wa cheo cha juu.

Wakristo huwaonyesha heshima na staha wenye mamlaka. Hata hivyo, hawahitaji kuomba msamaha kwa sababu ya kumtii Mungu na kuwapenda ndugu zao.—Mathayo 28:19, 20; Waroma 13:5-7.

Hakuna Kizuizi cha Amani

Leo, tunafanya makosa kwa sababu tulirithi kutokamilika na dhambi kutoka kwa Adamu, mzazi wetu wa kale. (Waroma 5:12; 1 Yohana 1:10) Adamu aliingia katika dhambi alipomwasi Muumba. Awali, Adamu na Hawa walikuwa wakamilifu bila dhambi, naye Mungu ameahidi kurudisha wanadamu wawe wakamilifu kama vile Adamu na Hawa walivyokuwa. Atafutilia mbali dhambi na matokeo yake.—1 Wakorintho 15:56, 57.

Hebu wazia hilo litamaanisha nini! Yakobo, ndugu wa kambo wa Yesu alisema hivi alipotoa shauri kuhusu matumizi ya ulimi: “Ikiwa yeyote hajikwai katika neno, huyu ni mtu mkamilifu, awezaye kuuongoza kwa hatamu mwili wake wote pia.” (Yakobo 3:2) Mtu mkamilifu anaweza kudhibiti ulimi wake na hivyo asihitaji kuomba msamaha kwa kuutumia vibaya. ‘Anaweza kuuongoza kwa hatamu mwili wake wote.’ Hali itakuwa nzuri kama nini tutakapokuwa wakamilifu! Kisha, hakutakuwepo jambo lolote lenye kuzuia watu wasiwe na amani. Hata sasa, kuomba msamaha ifaavyo na kwa unyofu tunapofanya kosa, kutasaidia sana kufanya amani.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Huenda Paulo hakumtambua kuhani huyo wa cheo cha juu kwa sababu hakuwa anaona vizuri.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Tunaweza kujifunza nini kutokana na kielelezo cha Paulo?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wakati kila mtu atakapokuwa mkamilifu, hakutakuwa na kizuizi cha amani