Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mahali Ambako Ibada ya Kweli na Upagani Ilitofautiana

Mahali Ambako Ibada ya Kweli na Upagani Ilitofautiana

Mahali Ambako Ibada ya Kweli na Upagani Ilitofautiana

KWA muda unaozidi karne moja, magofu ya Efeso la kale, kwenye pwani ya magharibi ya Uturuki, yamefanyiwa utafiti mwingi sana wa kiakiolojia. Majengo kadhaa yamejengwa upya na vitu vingi vya kale vimefukuliwa, vikachunguzwa, na kuelezwa na wanasayansi. Kwa sababu hiyo, Efeso ni mojawapo ya sehemu zinazotembelewa sana na watalii nchini Uturuki.

Ni nini ambacho kimegunduliwa kuhusu Efeso? Jiji hilo la kale lenye kuvutia huonekanaje leo? Kutembea kwenye magofu ya Efeso na kwenye Jumba la Makumbusho la Efeso huko Vienna, Austria, kutatusaidia kuelewa jinsi ibada ya kweli ilivyotofautiana na upagani huko Efeso. Acheni tuchunguze habari fulani kuhusu Efeso.

Eneo Ambalo Watu Wengi Walitaka Kumiliki

Katika karne ya 11 K.W.K., mizozo na kuhamia sehemu nyingine yalikuwa mambo ya kawaida katika mabara ya Ulaya na Asia. Ni wakati huo Wagiriki wa Ioni walipoanza kutawala pwani ya magharibi ya Asia Ndogo. Walowezi hao wa mapema walikutana na watu waliojulikana kwa ibada ya mungu-mama, mungu ambaye baadaye aliitwa Artemi wa Efeso.

Katikati ya karne ya saba K.W.K., Wasimeria wenye kuhama-hama walikuja kutoka Bahari Nyeusi upande wa kaskazini ili kuvamia Asia Ndogo. Baadaye, yapata mwaka wa 550 K.W.K., Mfalme Croesus mwenye nguvu na aliyekuwa mashuhuri kwa utajiri wake mwingi alianza kutawala Lydia. Milki ya Uajemi ilipopanuka, Mfalme Koreshi alishinda majiji ya Ioni, kutia ndani Efeso.

Mnamo mwaka wa 334 K.W.K., Aleksanda wa Makedonia alianzisha kampeni yake dhidi ya Uajemi, na hivyo akawa mtawala mpya wa Efeso. Baada ya Aleksanda kufa ghafula mwaka wa 323 K.W.K., majenerali wake walianza kung’ang’ania mamlaka huko Efeso. Mnamo mwaka wa 133 K.W.K., Attalus wa Tatu, mfalme wa Pergamamu ambaye hakuwa na watoto, aliwaachia Waroma jiji la Efeso, na hivyo likawa sehemu ya jimbo la Roma la Asia.

Ibada ya Kweli Yatofautiana na Upagani

Mtume Paulo alipoenda Efeso karibu na mwisho wa safari yake ya pili ya umishonari katika karne ya kwanza W.K., alipata jiji lenye wakaaji 300,000 hivi. (Matendo 18:19-21) Katika safari yake ya tatu ya umishonari, Paulo alirudi Efeso, na akiwa na ujasiri hata zaidi, alizungumza kuhusu Ufalme wa Mungu katika sinagogi. Hata hivyo, baada ya miezi mitatu, upinzani wa Wayahudi uliongezeka, hivyo Paulo akaamua kutoa hotuba zake za kila siku kwenye ukumbi wa shule ya Tirano. (Matendo 19:1, 8, 9) Alihubiri kwa miaka miwili huku akifanya kazi zenye nguvu, kama vile kuwaponya watu kimuujiza na kufukuza roho waovu. (Matendo 19:10-17) Haishangazi kwamba wengi walipata kuwa waamini! Naam, neno la Yehova lilisitawi hivi kwamba watu wengi waliokuwa wamezoea kufanya ufundi wa uchawi waliteketeza vitabu vyao vyenye thamani.—Matendo 19:19, 20.

Mahubiri ya Paulo yalifanikiwa kuwachochea wengi waache ibada ya mungu Artemi na pia yaliwakasirisha wale walioendeleza ibada hiyo ya kipagani. Kazi ya kutengeneza vihekalu vya fedha vya Artemi ilikuwa biashara yenye faida. Biashara yao ilipotishwa, mtu fulani aliyeitwa Demetrio aliwachochea mafundi wa fedha wazushe ghasia.—Matendo 19:23-32.

Makabiliano hayo yalifikia upeo wakati umati wenye hasira ulipopaaza sauti hivi kwa muda wa saa mbili: “Artemi wa Waefeso ni mkuu!” (Matendo 19:34) Ghasia zilipopungua, Paulo aliwatia moyo Wakristo wenzake kwa mara nyingine tena kisha akaendelea na safari yake. (Matendo 20:1) Hata hivyo, alipoondoka kwenda Makedonia, hilo halikuzuia kuporomoka kwa madhehebu ya Artemi yaliyokuwa yaangamie.

Hekalu la Artemi Laporomoka

Madhehebu ya Artemi yalikuwa yametia mizizi huko Efeso. Kabla Mfalme Croesus kuanza kutawala, mungu-mke Cybele ndiye aliyekuwa mungu mkuu katika eneo hilo. Kwa kudai kwamba Cybele alikuwa na uhusiano wa kiukoo na miungu ya Kigiriki, Croesus alitumaini kuanzisha ibada ya mtu ambaye angeabudiwa na Wagiriki na wasio Wagiriki. Kwa msaada wake, kazi ya kujenga hekalu la Artemi, aliyekuwa mrithi wa Cybele, ilianza katikati mwa karne ya sita K.W.K.

Kujengwa kwa hekalu hilo kulikuwa hatua muhimu katika ustadi wa kujenga wa Wagiriki. Kabla ya hapo, hakuna jengo kama hilo lililojengwa kwa vipande vikubwa vya marumaru na lenye ukubwa kama huo lililopata kujengwa. Hekalu hilo liliharibiwa kwa moto mwaka wa 356 K.W.K. Watu wengi walipata kazi na pia mahujaji walitembelea hekalu lililojengwa upya na lenye fahari kama lile la kwanza. Hekalu hilo lenye upana wa meta 50 hivi na urefu wa meta 105 lilijengwa kwenye eneo lililoinuka lenye upana wa meta 73 hivi na urefu wa meta 127. Lilionwa kuwa mojawapo ya maajabu saba ya ulimwengu. Hata hivyo, si kila mtu aliyependezwa nalo. Mwanafalsafa Heracleitus wa Efeso alifananisha njia yenye giza iliyoelekea kwenye madhabahu na giza la kiadili, naye aliona maadili ya hekalu kuwa mabaya zaidi kuliko ya wanyama. Hata hivyo, wengi waliona kwamba patakatifu pa Artemi huko Efeso hapangeporomoka kamwe. Historia ilionyesha jambo lililo kinyume na hilo. Kitabu Ephesos—Der neue Führer (Efeso—Mwongozo Mpya) kinasema: “Kufikia karne ya pili, ibada ya Artemi na ya miungu mingine iliporomoka kwa ghafula.”

Katika karne ya tatu W.K., Efeso lilikumbwa na tetemeko kubwa la nchi. Isitoshe, vitu vyenye thamani na vyenye kuvutia ambavyo vilikuwa katika hekalu la Artemi viliporwa na mabaharia Wagothi kutoka Bahari Nyeusi, ambao waliteketeza hekalu hilo. Kitabu kilichotangulia kutajwa kinasema: “Artemi angeendeleaje kuonwa kuwa mlinzi wa jiji na hali hakuweza kulinda makao yake mwenyewe?”—Zaburi 135:15-18.

Mwishowe, kuelekea mwisho wa karne ya nne W.K., Maliki Theodosius wa Kwanza alitangaza “Ukristo” kuwa dini rasmi. Upesi kuta za hekalu la Artemi ambalo wakati mmoja lilikuwa maarufu zikawa machimbo ya vifaa vya kujengea. Ibada ya Artemi ikapoteza umashuhuri kabisa. Shahidi mmoja asiyetajwa jina alisema hivi kuhusu shairi fupi la kutukuza hekalu hilo kuwa mojawapo ya maajabu ya ulimwengu wa kale: “Sasa limekuwa mahali penye ukiwa na penye kuaibisha zaidi.”

“Mama ya Mungu” Achukua Mahali pa Artemi

Paulo aliwaonya wanaume wazee wa kutaniko huko Efeso kwamba baada ya yeye kuondoka “mbwa-mwitu wenye kukandamiza” wangetokea na kutoka miongoni mwao watu wangesimama na “kusema mambo yaliyopotoka.” (Matendo 20:17, 29, 30) Hivyo ndivyo ilivyotukia. Matukio yanaonyesha kwamba ibada bandia ilisitawi huko Efeso kwa namna ya uasi-imani wa Ukristo bandia.

Mnamo mwaka wa 431 W.K., baraza la tatu la makanisa lilifanywa huko Efeso ambako suala kuhusu asili ya Kristo lilizungumziwa. Kichapo Ephesos—Der neue Führer kinasema: “Watu wa Aleksandria ambao waliamini kwamba Kristo ana asili moja tu, yaani, asili ya Kimungu, walipata ushindi . . . kamili.” Matokeo yalikuwa makubwa sana. “Uamuzi uliofikiwa huko Efeso ambako Maria alipandishwa cheo kutoka kuwa aliyemzaa Kristo hadi kuwa aliyemzaa Mungu, haukuweka tu msingi wa ibada ya Maria bali pia ulitokeza mgawanyiko wa kwanza mkubwa katika kanisa. . . . Mjadala huo unaendelea hadi leo hii.”

Hivyo, ibada ya Maria “aliyemzaa Mungu” au “mama ya mungu” ilichukua mahali pa ibada ya Cybele na Artemi. Kama kitabu hicho kisemavyo, ‘ibada ya Maria huko Efeso bado inafuatwa, nayo inahusianishwa na Madhehebu ya Artemi.’

Ibada ya Artemi Yasahauliwa

Baada ya ibada ya Artemi kuporomoka, Efeso lilianguka. Matetemeko ya nchi, malaria, na kuongezeka hatua kwa hatua kwa mchanga bandarini kulifanya maisha yawe magumu zaidi jijini.

Kufikia karne ya saba W.K., Uislamu ulikuwa umeanza kusambaa sana. Uislamu ulifanya mengi zaidi ya kuunganisha tu mataifa ya Waarabu ambayo yaliukubali. Katika karne ya saba na ya nane W.K., meli za Waarabu zilipora Efeso. Hatima ya Efeso ilijulikana wakati bandari ilipojaa mchanga kabisa na jiji hilo likawa rundo la magofu. Kuhusiana na jiji hilo lililokuwa lenye kuvutia, ni kijiji kimoja kidogo tu kinachoitwa Aya Soluk (sasa ni Selçuk) kilichobaki.

Kutembea Kwenye Magofu ya Efeso

Ili kupata picha ya umaarufu wa Efeso la kale, unaweza kutembea kwenye magofu yake. Ukianza safari yako kwa kupitia lango la juu, mara moja utaona mandhari yenye kuvutia ya Barabara ya Curetes inayoelekea kwenye Maktaba ya Celsus. Upande wa kuume wa barabara hiyo kuna Odeum, jumba dogo la maonyesho lililojengwa katika karne ya pili W.K., litakalokuvutia. Jumba hilo ambalo linaweza kutoshea watu 1,500 hivi yaelekea lilitumiwa kama chumba cha baraza na pia kwa vitumbuizo vya umma. Kando ya Barabara ya Curetes kuna majengo kama vile, mahali pa kukutania pa Serikali ambako masuala ya Serikali yalizungumziwa, hekalu la Hadrian, chemchemi kadhaa za umma, na nyumba zilizojengwa juu ya kilima—nyumba za Waefeso mashuhuri.

Utavutiwa na umaridadi wa Maktaba ya Celsus ambayo ilijengwa katika karne ya pili W.K. Vitabu vyake vingi vya kukunjwa viliwekwa kwenye nafasi iliyotengenezwa ukutani katika chumba kikubwa cha kusomea. Upande wa mbele wa maktaba hiyo ulikuwa na sanamu nne ambazo ziliwakilisha sifa ambazo mtumishi wa umma wa cheo cha juu Mroma kama vile Celsus, alipaswa kuonyesha yaani: Sophia (hekima), Arete (wema wa adili), Ennoia (ujitoaji-kimungu), na Episteme (ujuzi au uelewaji). Sanamu za awali zinaweza kutazamwa kwenye Jumba la Makumbusho la Efeso huko Vienna. Karibu na ua wa mbele wa maktaba hiyo, kuna mlango mkubwa sana unaokuelekeza kwenye soko la Tetragonos. Watu walifanya shughuli zao za kibiashara za kila siku kwenye sehemu hiyo kubwa, ambayo ilizungukwa na barabara pana za waendao kwa miguu.

Kisha unafika kwenye barabara inayoitwa Marble Road ambayo inaelekea kwenye jumba kuu la maonyesho. Jumba hilo lilipanuliwa mara ya mwisho wakati wa utawala wa Waroma, nalo lilitoshea watazamaji wapatao 25,000. Ukuta wa mbele ulirembeshwa kwa nguzo, sanamu zilizochongwa ukutani, na sanamu nyinginezo. Unaweza kuwazia waziwazi ile ghasia kubwa iliyozushwa na Demetrio, fundi wa fedha miongoni mwa umati uliokusanyika huko.

Barabara inayotoka kwenye jumba kuu la maonyesho hadi jijini, ni nzuri sana. Ina urefu wa meta 500 hivi na upana wa meta 11, nayo imepambwa kwa nguzo pande zote. Pia kumbi mbili za mazoezi ya viungo zilijengwa kandokando ya barabara hiyo. Matembezi yetu mafupi kwenye magofu yenye kuvutia zaidi ulimwenguni yanafikia kikomo tunapofika mwishoni mwa barabara hiyo, ambapo kuna lango kubwa la bandari iliyotumiwa kusafiri kwenye nchi nyingine. Kwenye Jumba la Makumbusho la Efeso huko Vienna kuna mfano wa jiji hilo la kale uliotengenezwa kwa mbao na vilevile minara ya ukumbusho.

Mtu anapotembelea jumba hilo la makumbusho na kuona sanamu ya Artemi wa Efeso, atafikiria mara moja jinsi Wakristo wa mapema huko Efeso walivyovumilia. Iliwabidi kuishi katika jiji lililojaa uwasiliani-roho na lenye ubaguzi wa kidini. Ujumbe wa Ufalme ulipingwa vikali na waabudu wa Artemi. (Matendo 19:19; Waefeso 6:12; Ufunuo 2:1-3) Ibada ya kweli ilisitawi chini ya hali hizo zisizofaa. Ibada hiyo ya Mungu wa kweli itasitawi pia wakati dini za uwongo za wakati wetu zitakapoharibiwa kama ibada ya Artemi ya kale.—Ufunuo 18:4-8.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MAKEDONIA

Bahari Nyeusi

ASIA NDOGO

Efeso

Bahari ya Mediterania

MISRI

[Picha katika ukurasa wa 27]

Magofu ya hekalu la Artemi

[Picha katika ukurasa wa 28, 29]

1. Maktaba ya Celsus

2. Picha iliyopigwa karibu ya sanamu ya Arete

3. Barabara ya Marble Road, inayoelekea kwenye jumba kuu la maonyesho