Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wanyama Humtukuza Yehova

Wanyama Humtukuza Yehova

Wanyama Humtukuza Yehova

WANYAMA huonyesha kwamba Yehova ni mkuu. Mungu huwatunza wanyama, kama vile anavyowatunza wanadamu. (Zaburi 145:16) Ni kosa kubwa kama nini kumchambua Muumba wa wanyama na wanadamu! Ingawa Ayubu alikuwa mtu mtimilifu, aliitangaza “nafsi yake mwenyewe kuwa adilifu badala ya Mungu.” Basi, Ayubu alihitaji kujifunza mambo fulani!—Ayubu 32:2; 33:8-12; 34:5.

Mifano ya wanyama mbalimbali ilimwonyesha Ayubu kwamba wanadamu hawastahili kumchambua Mungu. Hilo linaonekana wazi tunapochunguza maneno ambayo Yehova alimwambia mtumishi wake Ayubu!

Hawahitaji Kusaidiwa na Wanadamu

Ayubu hangeweza kujibu maswali ya Mungu kuhusu wanyama. (Ayubu 38:39-41) Ni wazi kwamba Yehova humtunza simba na kunguru bila kusaidiwa na wanadamu. Ingawa kunguru huruka huku na huku wakitafuta chakula, wao hupata chakula chao hasa kutoka kwa Mungu.—Luka 12:24.

Ayubu alipigwa na bumbuazi wakati Mungu alipomuuliza kuhusu wanyama wa mwituni. (Ayubu 39:1-8) Hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kuwalinda mbuzi wa milimani na paa. Hata ni vigumu kuwakaribia mbuzi wa milimani! (Zaburi 104:18) Paa hujitenga msituni anapokaribia kuzaa kwa sababu amepewa silika na Mungu. Yeye huwatunza sana watoto wake, lakini wanapokuwa “wenye nguvu,” wao “huenda zao wala hawarudi.” Kisha wanaishi peke yao.

Punda-milia hukimbia huku na huku akiwa huru, na nchi tambarare ya jangwa ndiyo makao ya punda-mwitu. Ayubu hangeweza kumtumia punda-mwitu kubeba mizigo. Punda-mwitu hutafuta “kila namna ya mmea wa kijani,” na kutafuta-tafuta malisho milimani. Mnyama huyo hawezi kukubali kuacha maisha yake yenye uhuru mwituni ili apate chakula kwa urahisi mjini. Punda-mwitu “hasikii kelele za mwindaji” kwa kuwa yeye hukimbia mwanadamu anapoingia katika makao yake.

Kisha Mungu anamtaja ng’ombe-mwitu. (Ayubu 39:9-12) Mchunguzi Mwingereza wa vitu vya kale, Austen Layard, alisema hivi kuhusu mnyama huyo: “Michongo mingi ya ng’ombe-mwitu inaonyesha kwamba mnyama huyo alionwa kuwa anamkaribia simba kwa kutisha na kwa fahari. Mara nyingi mfalme anaonyeshwa akipambana naye, na mashujaa humfuata kwa farasi na kwa miguu.” (Nineveh and Its Remains, 1849, Buku la 2, ukurasa wa 326) Hata hivyo, hakuna mwanadamu mwenye hekima anayeweza kujaribu kumfunga ng’ombe-mwitu asiyeweza kudhibitiwa.—Zaburi 22:21.

Viumbe Wenye Mabawa Humtukuza Yehova

Kisha Mungu alimuuliza Ayubu kuhusu viumbe wenye mabawa. (Ayubu 39:13-18) Korongo huruka juu kwa mabawa yake yenye nguvu. (Yeremia 8:7) Hata ingawa mbuni hupigapiga mabawa yake, hawezi kuruka. Tofauti na korongo, mbuni haweki mayai yake ndani ya kiota kilichojengwa kwenye mti. (Zaburi 104:17) Yeye huchimba shimo mchangani na kutaga mayai yake humo. Lakini ndege huyo hayaachi mayai yake kabisa. Mayai hayo hufunikwa kwa mchanga, nayo hupata joto linalofaa huku mbuni-dume na mbuni-jike wakiyatunza.

Huenda ikaonekana kwamba mbuni ‘husahau hekima’ anapotambua hatari ya mwindaji na kukimbia. Hata hivyo, kitabu kimoja (An Encyclopedia of Bible Animals) kinasema hivi: “Hiyo ni mbinu ya kukengeusha: [mbuni] hujionyesha waziwazi, nao hupigapiga mabawa yao ili kumvutia mnyama au mtu yeyote anayetaka kuvamia na kumkengeusha asikaribie mayai.”

Inakuwaje kwamba mbuni “humcheka farasi na mpandaji wake”? Kitabu kimoja (The World Book Encyclopedia) kinasema hivi: “Mbuni hawezi kuruka, lakini anajulikana kwa uwezo wake wa kwenda kasi. Miguu yake mirefu inaweza kupiga hatua zenye urefu wa meta 4.6 kwa mwendo wa kilometa 64 kwa saa.”

Mungu Humpa Farasi Nguvu

Kisha Mungu alimuuliza Ayubu kuhusu farasi. (Ayubu 39:19-25) Zamani, mashujaa wa vita walipigana wakiwa wamepanda farasi, na farasi walivuta magari ya vita yaliyokuwa na mwendeshaji na labda askari-jeshi wengine wawili. Farasi wa vita hulia na kuparapara chini kwa miguu yake kwa sababu ya hamu ya kwenda vitani. Hatishiki, naye harudi nyuma kwa sababu ya upanga. Baragumu inapopiga, farasi wa vita huitikia kana kwamba anasema, “Aha!” Kisha yeye husonga mbele na ‘kuimeza nchi.’ Hata hivyo, farasi wa vita humtii mpandaji wake.

Kwa kulinganisha, Layard aliandika hivi: “Ingawa yeye ni mpole kama kondoo, naye hahitaji kuongozwa kwa kitu kingine ila kwa hatamu, farasi-jike wa Uarabuni anaposikia kilio cha vita na kuona mkuki wa mpandaji wake ukitikisika-tikisika, macho yake hung’aa kana kwamba yamewaka moto, matundu mekundu ya pua yake hupanuka kabisa, shingo yake hukunjwa kwa madaha, na mkia na manyoya yake huinuliwa kuelekea upepo.”—Discoveries Among the Ruins of Nineveh and Babylon, 1853, ukurasa wa 330.

Mfikirie Kipanga na Tai

Kisha Yehova akazungumza na Ayubu kuhusu ndege wengine. (Ayubu 39:26-30) Vipanga ‘hupaa juu na kunyoosha mabawa yao kuuelekea upepo.’ Kitabu kimoja (The Guinness Book of Records) kinasema kwamba jamii fulani ya vipanga ndio ndege wanaoruka kwa kasi zaidi ulimwenguni. Pia, kinasema kwamba vipanga hao “huenda kasi zaidi wanaporuka kutoka juu sana wakati wanapoonyesha mipaka ya eneo lao, au wanapokamata mawindo hewani.” Ndege hao wamewahi kuruka hata kwa mwendo wa kilometa 349 kwa saa wakiteremka kutoka juu.

Tai wamewahi kuruka kwa mwendo wa zaidi ya kilometa 130 kwa saa. Ayubu alilinganisha jinsi maisha yanavyosonga upesi na mwendo wa tai anayetafuta mawindo. (Ayubu 9:25, 26) Mungu hutupa nguvu za kuvumilia kana kwamba tuko kwenye mabawa ya tai anayepaa juu ambayo yanaonekana kuwa hayachoki. (Isaya 40:31) Tai anaporuka, yeye hutumia hewa yenye joto inayopaa. Ndege huyo huzunguka katika hewa hiyo, nayo humwinua zaidi na zaidi. Tai anapofikia kiwango fulani, yeye huruka hadi kwenye hewa nyingine yenye joto iliyo karibu, naye anaweza kubaki hewani kwa saa nyingi bila kutumia nguvu nyingi.

Tai “hujenga kiota chake huko juu,” mahali pasipoweza kufikiwa, na hivyo kuwazuia watoto wake wasipatwe na hatari. Yehova amemwezesha tai kufanya hivyo kisilika. Mungu amempa uwezo wa kuona ambao unawezesha ‘macho ya tai kuendelea kutazama mbali sana.’ Uwezo wa tai wa kubadili haraka mkazo wa macho yake humwezesha kukazia macho mawindo yake au mzoga ulio mbali wakati anaposhuka. Kwa kuwa tai anaweza kula mizoga, “mahali walipo wale waliouawa, yeye yupo hapo.” Ndege huyo huwakamata wanyama wadogo na kuwapelekea watoto wake.

Yehova Anamtia Nidhamu Ayubu

Kabla ya kumuuliza Ayubu maswali mengine kuhusu wanyama, Mungu alimtia nidhamu Ayubu. Ayubu alitendaje alipotiwa nidhamu? Alijinyenyekeza na kukubali kwa utayari mashauri mengine.—Ayubu 40:1-14.

Sehemu hii ya simulizi la Ayubu inatufunza jambo muhimu sana: Hakuna mwanadamu yeyote anayestahili kutafuta kosa katika Mweza-Yote. Tunapaswa kuzungumza na kutenda kwa njia inayompendeza Baba yetu wa mbinguni. Isitoshe, tunapaswa kuhangaikia hasa kutakaswa kwa jina takatifu la Yehova na kutetewa kwa enzi yake kuu.

Behemothi Humtukuza Mungu

Akizungumza tena kuhusu wanyama, Mungu alimuuliza Ayubu kuhusu Behemothi, ambaye kwa kawaida hutambulishwa kuwa kiboko. (Ayubu 40:15-24) Kiboko aliyekomaa anaweza kuwa na urefu wa meta 4 hadi 5 na uzito wa kilo 3,600. “Nguvu [za Behemothi] zimo katika viuno vyake,” yaani, misuli iliyo mgongoni mwake. Ngozi ngumu ya tumbo lake humsaidia sana mnyama huyo mwenye miguu mifupi wakati anapovuta mwili wake juu ya mawe yaliyo kwenye kingo za mito. Ni wazi kwamba mwanadamu hawezi kushindana na Behemothi, kwa kuwa ana mwili mkubwa sana, mdomo mkubwa, na mataya yenye nguvu.

Behemothi hutoka mtoni ili kula “majani.” Inaonekana anahitaji kula majani mengi kama yale yanayopatikana kwenye mlima mzima! Yeye hula kilo 90 hadi 180 za majani kila siku. Behemothi anaposhiba, yeye hulala chini ya miyungiyungi au katika kivuli cha mierebi. Mto anaoishi ndani yake ukifurika, kiboko anaweza kuinua kichwa chake juu ya maji na kuogelea. Ikiwa Ayubu angeshambuliwa na mdomo mkubwa wa Behemothi na meno yake yenye kutisha, hangethubutu kumchoma puani kwa kulabu.

Leviathani Humletea Mungu Sifa

Kisha Ayubu akaelezwa kuhusu Leviathani. (Ayubu 41:1-34) Neno la Kiebrania la mnyama huyo linamaanisha “mnyama mwenye magamba,” ambaye inaonekana ni mamba. Je, Ayubu angeweza kumfanya Leviathani kuwa kitu cha kuchezewa na watoto? La hasha! Kiumbe huyo amethibitika kuwa hatari. Naam, ikiwa mwanadamu angejaribu kupambana na Leviathani, pambano hilo lingekuwa kali sana hivi kwamba mwanadamu hangethubutu kurudia kufanya hivyo!

Leviathani anapoinua kichwa chake juu ya maji wakati jua linapochomoza, macho yake hung’aa “kama miali ya mapambazuko.” Magamba ya Leviathani yameshikamana kabisa, na kwenye ngozi yake kuna magamba yaliyo kama mifupa ambayo ni magumu sana yasiweze kupenywa na risasi, wala upanga au mikuki. Magamba yenye ncha kali kwenye tumbo la mamba hufanyiza alama za “kifaa cha kupuria” juu ya matope yaliyo kwenye kingo za mto. Hasira zake akiwa ndani ya maji huyafanya yawe kama marhamu yenye mapovu mengi. Isitoshe, kwa sababu ya ukubwa wake na silaha zake, yaani, mdomo wenye kutisha na mkia wenye nguvu, Leviathani hawezi kutishika.

Ayubu Anatangua Mambo Aliyosema

Ayubu alikubali kwamba ‘alisema lakini hakuwa anaelewa mambo yaliyo ya ajabu mno kwake.’ (Ayubu 42:1-3) Alikubali mashauri ya Mungu, akayatangua mambo aliyosema, na kutubu. Rafiki zake walikemewa, lakini Ayubu alibarikiwa sana.—Ayubu 42:4-17.

Ni jambo la hekima kama nini kukumbuka kisa cha Ayubu! Hatuwezi kamwe kujibu maswali yote ambayo Mungu alimuuliza. Hata hivyo, tunaweza na tunapaswa kuonyesha uthamini kwa maajabu mengi ya uumbaji yanayomtukuza Yehova.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Mbuzi wa milimani

[Picha katika ukurasa wa 13]

Kunguru

[Picha katika ukurasa wa 13]

Simba-jike

[Picha katika ukurasa wa 14]

Punda-milia

[Picha katika ukurasa wa 14]

Mbuni huondoka mahali mayai yake yalipo, lakini hayaachi kabisa

[Picha katika ukurasa wa 14]

Mayai ya mbuni

[Picha katika ukurasa wa 14, 15]

Kipanga

[Hisani]

Falcon: © Joe McDonald/Visuals Unlimited

[Picha katika ukurasa wa 15]

Farasi-jike wa Uarabuni

[Picha katika ukurasa wa 15]

Tai

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kwa kawaida Behemothi hutambulishwa kuwa kiboko

[Picha katika ukurasa wa 16]

Inasemekana kwamba Leviathani ni mamba mwenye nguvu