Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Wanajimu walienda kumwona Yesu wakati gani?

Katika Injili ya Mathayo, tunaambiwa kwamba “wanajimu kutoka sehemu za mashariki” walienda kumwona Yesu, na kumpelekea zawadi. (Mathayo 2:1-12) Idadi ya wanajimu au “mamajusi” ambao walienda kumwona mtoto Yesu haitajwi, na maoni ya watu wengi kwamba walikuwa watatu hayana msingi imara; wala majina yao hayatajwi katika masimulizi ya Biblia.

Tafsiri moja ya Biblia (The New International Version Study Bible) inatoa maelezo yafuatayo kuhusu Mathayo 2:11: “Kinyume na mapokeo, Mamajusi hawakwenda kumwona Yesu kwenye hori usiku alipozaliwa kama walivyofanya wachungaji. Walikuja baada ya miezi kadhaa na walienda kumwona akiwa ‘mtoto’ ‘nyumbani’ kwake.” Hilo linathibitishwa na uhakika wa kwamba Herode, alipotafuta kumuua mtoto huyo mchanga, aliamuru wavulana wote wa umri wa miaka miwili na kwenda chini katika Bethlehemu yote na katika wilaya zake wauawe. Alilenga wavulana wa umri huo kwa kuhesabu “kulingana na wakati aliokuwa amehakikisha kwa uangalifu kutoka kwa wale wanajimu.”—Mathayo 2:16.

Ikiwa wanajimu hao walienda kumwona Yesu usiku aliozaliwa na kumpelekea dhahabu na zawadi nyingine zenye thamani, haielekei kwamba Maria angetoa tu ndege wawili siku 40 baadaye wakati alipompeleka Yesu kwenye hekalu huko Yerusalemu. (Luka 2:22-24) Mpango huo wa kutoa ndege wawili ulikuwa katika Sheria ya Musa kwa ajili ya watu maskini ambao hawangeweza kutoa kondoo-dume mchanga. (Mambo ya Walawi 12:8) Hata hivyo, huenda zawadi hizo zenye thamani zilitolewa kwa wakati uliofaa na zilisaidia sana kulipia gharama za familia ya Yesu huko Misri.—Mathayo 2:13-15.

Kwa nini ilimchukua Yesu siku nne ili kufika kwenye kaburi la Lazaro?

Inaelekea kwamba Yesu alipanga kimakusudi ili mambo yawe hivyo. Kwa nini tunaweza kusema hivyo? Fikiria simulizi lililo katika Yohana sura ya 11.

Lazaro, mkaaji wa Bethania na rafiki wa Yesu, alipokuwa mgonjwa sana, dada zake walituma ujumbe kwa Yesu. (Mistari 1-3) Wakati huo, Yesu alikuwa umbali wa safari ya siku mbili hivi kutoka Bethania. (Yohana 10:40) Ni wazi kwamba Lazaro alikufa karibu wakati habari ya ugonjwa wake ilipomfikia Yesu. Yesu alifanya nini? ‘Alikaa siku mbili mahali alipokuwa,’ na kisha akaondoka kwenda Bethania. (Mistari 6,  7) Hivyo, kwa kungoja siku mbili na kisha kusafiri siku mbili, alifika kwenye kaburi siku nne baada ya kifo cha Lazaro.—Mstari 17.

Mapema, Yesu alikuwa amewafufua watu wawili. Yesu alimfufua mtu wa kwanza baada tu ya mtu huyo kufa, na alimfufua yule wa pili muda mfupi baada ya kufa. (Luka 7:11-17; 8:49-55) Je, angeweza kumfufua mtu aliyekuwa amekufa kwa muda wa siku nne na ambaye mwili wake ulikuwa tayari umeanza kuoza? (Mstari wa 39) Inapendeza kujua kwamba kitabu kimoja cha marejeo ya Biblia kinasema kuwa Wayahudi waliamini kwamba “hakukuwa na tumaini kwa mtu aliyekuwa amekufa kwa muda wa siku nne; kwa kuwa mwili wake ulikuwa umeanza kuoza, na nafsi, ambayo ilidhaniwa inaelea angani juu ya mwili kwa muda wa siku tatu, ilikuwa imeondoka.”

Ikiwa kulikuwa na watu wowote wenye mashaka kati ya wale waliokusanyika kwenye kaburi hilo, walikuwa karibu kushuhudia nguvu za Yesu juu ya kifo. Akiwa amesimama mbele ya kaburi lililo wazi, Yesu alipaaza sauti: “Lazaro, njoo huku nje!” Ndipo, “huyo mtu aliyekuwa mfu akatoka.” (Mistari 43, 44) Tumaini hakika kwa ajili ya wafu ni ufufuo wala si wazo lisilo la kweli ambalo wengi wanaamini kwamba nafsi inaishi baada ya kifo.—Ezekieli 18:4; Yohana 11:25.