Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Yesu alizungumza lugha gani?

Wasomi mbalimbali hawakubaliani kuhusu lugha ambayo Yesu alizungumza. Hata hivyo, inaelekea kwamba akiwa mwanadamu duniani, huenda Yesu alizungumza aina fulani ya Kiebrania na lahaja ya Kiaramu. Yesu alipokuja Nazareti kule Galilaya, aliingia kwenye sinagogi na akasoma kutoka kwenye unabii wa Isaya ambao bila shaka ulikuwa umeandikwa katika lugha ya Kiebrania. Biblia haisemi kwamba Yesu alitafsiri maneno aliyosoma katika Kiaramu.—Luka 4:16-21.

Kuhusu lugha zilizotumiwa kule Palestina Yesu alipokuwa duniani, Profesa G. Ernest Wright anasema: “Inaonekana kwamba Kigiriki na Kiaramu zilikuwa lugha za kawaida . . . Huenda wanajeshi na maofisa Waroma walisikiwa wakizungumza katika Kilatini, huku Wayahudi waliofuata mapokeo wakizungumza Kiebrania cha wakati huo.” Basi haishangazi kuona ni kwa nini ubao uliowekwa na Pilato kwenye mti wa mateso wa Yesu uliandikwa katika lugha tatu—Kiebrania, Kilatini na Kigiriki.—Yohana 19:20.

Katika kitabu chake (Discoveries From the Time of Jesus), Alan Millard anasema hivi: “Katika shughuli zao za kila siku, bila shaka magavana Waroma walizungumza Kigiriki, na wakati wa kesi yake huenda Yesu alijibu maswali aliyoulizwa na Pilato katika Kigiriki.” Hata ingawa Biblia haionyeshi kwamba Yesu alimjibu Pilato katika Kigiriki, inapendeza kuona kwamba haitaji kulikuwa na mkalimani katika mazungumzo yao.—Yohana 18:28-40.

Kulingana na Profesa Wright, “hatuwezi kuwa na hakika ikiwa [Yesu] angeweza kuzungumza Kigiriki au Kilatini, lakini kwa kawaida katika huduma yake ya kufundisha alitumia Kiaramu au Kiebrania kilichotumiwa na watu wengi kilichokuwa kimeathiriwa sana na Kiaramu.”—Biblical Archeology, 1962, ukurasa wa 243.

Mawe ya hekalu la Yerusalemu yalikuwa makubwa kadiri gani?

Wakizungumza na Yesu kuhusu hekalu lililokuwa Yerusalemu, wanafunzi walimwambia hivi: “Mwalimu, ona! jinsi yalivyo mawe haya na majengo haya!” (Marko 13:1) Baadhi ya mawe hayo yalikuwa na makubwa kadiri gani?

Yesu alipokuwa duniani, Mfalme Herode alikuwa amelipanua Hekalu la Mlimani kuwa kubwa mara mbili zaidi ikilinganishwa na lile lililojengwa katika siku za Sulemani. Lilikuwa ndilo jukwaa kubwa zaidi kuwahi kutengenezwa na mwanadamu katika ulimwengu wa kale likiwa na urefu wa mita 480, na upana wa mita 280. Inasemekana kwamba baadhi ya mawe yaliyotumiwa kulijenga yalikuwa na urefu wa mita 11, upana wa mita 5, na kimo cha mita 3. Baadhi yake yalikuwa na uzito wa zaidi ya tani 50 kwa kila jiwe. Kuna jiwe moja ambalo lilikuwa na uzito wa karibu tani 400, na kulingana na msomi mmoja, “hakuna jiwe lolote katika ulimwengu wa kale lililokuwa kubwa kuliko hilo.”

Akizungumza kuhusu jambo ambalo wanafunzi wake walikuwa wamesema, Yesu alisema: “Unayaona majengo haya makubwa? Hakuna jiwe litakaloachwa hapa juu ya jiwe nalo lisiangushwe chini.” (Marko 13:2) Mengi ya mawe hayo makubwa yanaweza kupatikana mahali yalipoanguka baada ya kung’olewa na kusukumwa chini na wanajeshi Waroma katika mwaka wa 70 W.K.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mawe ya Hekalu yakiwa yameangushwa nje ya hekalu la mlimani, Yerusalemu