Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Ni nini lililokuwa kusudi la agizo la kuhesabiwa kwa watu lililofanya Yesu azaliwe Bethlehemu?

Kulingana na Injili ya Luka, wakati Kaisari Augusto alipoamuru kuhesabiwa kwa watu waliokuwa chini ya milki ya Roma, “watu wote wakaanza kusafiri kwenda kuandikishwa, kila mmoja kwenye jiji lake mwenyewe.” (Luka 2:1-3) Mji wa Yosefu, baba mlezi wa Yesu, ulikuwa Bethlehemu, na kwa kutii sheria hiyo yeye na Maria walisafiri hadi Bethlehemu ambako Yesu alizaliwa. Serikali ziliandikisha watu ili iwe rahisi kukusanya kodi na pia kuandikisha watu jeshini.

Waroma walipoteka Misri mwaka wa 30 K.W.K., tayari Wamisri walikuwa wakiwahesabu watu kwa miaka mingi. Wasomi fulani husema Waroma waliiga jinsi Wamisri walivyokuwa wakiwahesabu watu na wakaanza kufanya hivyo kotekote katika milki yao.

Uthibitisho mmoja wa kuandikishwa kwa watu unapatikana katika agizo la gavana Mroma wa Misri mwaka wa 104 W.K. Nakala moja ya agizo hilo ambayo imehifadhiwa katika Maktaba la Uingereza lilikuwa na maneno haya: “Gaius Vibius Maximus, Liwali wa Misri (anasema): Kwa kuwa wakati wa kuhesabiwa kwa watu kutoka nyumba hadi nyumba umefika, watu wote wanaoishi nje ya wilaya zao kwa sababu zozote zile wanashurutishwa warudi nyumbani kwao ili waweze kuhesabiwa na pia ili waweze kupalilia kwa bidii mashamba yao waliyogawiwa.”

Kwa nini Yosefu alifikiria kumpa Maria cheti cha talaka ingawa walikuwa wanachumbiana tu?

Injili ya Mathayo inasema kwamba Yosefu aligundua kwamba Maria alikuwa na mimba ‘alipokuwa akimchumbia,’ na hawakuwa wameoana. Kwa kuwa hakujua kwamba Maria alikuwa na mimba “kwa njia ya roho takatifu,” huenda Yosefu alifikiria kwamba Maria hakuwa mwaminifu kwake na hivyo alitaka kumtaliki.—Mathayo 1:18-20.

Kati ya Wayahudi, watu waliokuwa wakichumbiana walionwa kuwa wameoana tayari. Lakini hawakuruhusiwa kuishi pamoja kama mume na mke hadi walipooana kihalali. Uchumba ulionwa kuwa jambo zito sana hivi kwamba ikiwa bwana-arusi angebadili msimamo wake au kwa sababu yoyote ile waamue kutofunga ndoa, msichana huyo alihitajika kutafuta cheti cha talaka ili awe huru kuolewa tena. Ikiwa mume wa msichana aliyekuwa amechumbiwa angekufa kabla ya harusi, msichana huyo alionwa kuwa mjane. Kwa upande mwingine, ikiwa msichana huyo angefanya uasherati akiwa amechumbiwa, angechukuliwa kuwa mzinzi na hivyo kuhukumiwa kifo.—Kumbukumbu la Torati 22:23, 24.

Huenda Yosefu alifikiria sana adhabu ambayo Maria angepewa ikiwa watu wangejua kwamba ana mimba. Ingawa alihisi kuwa alipaswa kuwaeleza wenye mamlaka kuhusu jambo hilo, hakufanya hivyo kwa kuwa alitaka kumlinda na kuepuka kumwaibisha Maria. Hivyo aliamua kumtaliki kisiri. Ikiwa mwanamke mwenye watoto angekuwa na cheti cha talaka, hilo lingeonyesha wazi kwamba alikuwa ameolewa awali.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Nakala ya agizo la kuhesabiwa kwa watu lililotolewa na Gavana Mroma wa Misri, mwaka wa 104 W.K.

[Hisani]

© The British Library Board, all rights reserved (P.904)