Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Safari ya Kuchunguza Mambo ya Kale

Safari ya Kuchunguza Mambo ya Kale

Barua Kutoka Marekani

Safari ya Kuchunguza Mambo ya Kale

WAZIA safari ya kuchunguza jinsi mababu zako walivyoishi inavyoweza kuwa yenye kusisimua. Kwa njia fulani tulifunga safari kama hiyo. Tulianzia Uswisi hadi Marekani. Watu wengi hudhani kuwa Marekani ni nchi iliyoendelea katika kila nyanja, lakini safari yetu iliturudisha nyuma zaidi ya miaka 200 iliyopita. Acha tukueleze kuihusu.

Kwa kuwa sisi huzungumza lahaja ya Kijerumani cha Uswisi, tulialikwa tutumikie kwa miezi mitatu katika jimbo la Indiana. Lengo letu lilikuwa kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu kwa familia za Waamishi ambao bado wanazungumza lahaja iliyotumiwa na mababu zao. Mamia ya familia hizi wanaishi katika jimbo la Indiana.

Waamishi ni wazao wa kikundi cha Wanabaptisti wa karne ya 17. Jina lao linatokana na kiongozi wao aliyeitwa Jacob Amman aliyeishi Uswisi. Kutokana na kujifunza Biblia, watu hawa waliomwogopa Mungu walitambua kuwa ni makosa kuwabatiza watoto na kutumikia jeshini. Waliteswa na serikali kwa sababu ya msimamo wao. Wengine hata waliuawa kwa sababu ya imani yao. Mateso yaliongezeka, na hilo liliwafanya wengine wakimbilie sehemu nyingine za Uswisi na hata Ufaransa. Kufikia katikati ya karne ya 19, maelfu walikuwa wamekimbilia Marekani. Hawakusahau tamaduni zao na lahaja ya Kijerumani cha Uswisi.

Tulipowatembelea watu hao wapole, walishangaa sana kusikia tukiongea katika lahaja yao! Hebu wazia tukio hilo.

“Inawezekanaje kuwa mnaongea lugha yetu?” waliuliza katika Kijerumani cha Uswisi.

“Kwa sababu tumetoka Uswisi,” tuliwajibu.

“Lakini nyinyi si Waamishi!” Walishangaa.

Tulikaribishwa katika nyumba nyingi na hivyo tuliona kwamba waliishi kama watu wa kale. Badala ya umeme, wanatumia taa za mafuta; badala ya magari, wanatumia magari yanayokokotwa na farasi; badala ya kutumia maji yanayotoka kwenye bomba, wanatumia kisima na kinu cha upepo; badala ya redio, wao huimba.

Kile kilichotushangaza hata zaidi ni sifa ya kiasi na unyenyekevu wa watu hawa tuliowatembelea. Familia nyingi za Waamishi hujaribu kusoma Biblia kila siku na wanathamini sana mazungumzo ya Biblia. Hili lilitupa fursa ya kuwa na mazungumzo kuhusu kusudi la Mungu kwa wanadamu na dunia.

Baada ya muda mfupi, habari ilikuwa imesambaa kotekote katika eneo hilo kuwa kulikuwa na wageni kutoka Uswisi. Wengi walituomba tuwatembelee watu wao wa ukoo na tukafanya hivyo. Tuliombwa tutembelee shule ya Kiamishi na tulitazamia kwa hamu kufanya hivyo. Tungepata nini huko?

Tulibisha mlango, naye mwalimu akafungua na kutukaribisha ndani ya darasa, ambamo kulikuwa na wanafunzi 38 waliotuangalia kwa hamu. Wanafunzi kutoka madarasa manane walikuwa wamekusanyika pamoja ndani ya darasa moja, umri wao ulikuwa kati ya miaka 7 hadi 15. Wasichana walikuwa wamevalia sare ya bluu na kofia nyeupe; wavulana nao walikuwa na suruali fupi nyeusi na shati za rangi ya bluu iliyokolea. Chumba hicho kilikuwa na dari iliyokuwa juu sana. Kuta tatu za jengo hilo zilikuwa zimepakwa rangi ya bluu, na ukuta wa mbele ulikuwa na ubao. Pia kulikuwa na tufe yenye ramani ya dunia na ramani nyingine ambazo zilikuwa zimekunjwa. Pembeni kulikuwa na jiko kubwa la chuma.

Tulipoketi mbele ya darasa, watoto hao walitutazama kwa mshangao mkubwa. Wanafunzi wa kila darasa waliitwa mbele ya mwalimu wao na kuulizwa kuhusu kazi za shuleni walizopewa siku iliyotangulia. Tulishangaa wakati mwalimu alipowauliza watoto kuhusu milima ya Alps ya Uswisi. Vitabu walivyokuwa wakitumia vilikuwa vya zamani na hivyo mwalimu alituuliza kama nchi ya Uswisi bado ilikuwa jinsi vitabu vyake vilivyokuwa vikieleza. Je, bado ng’ombe hulisha juu ya milima ya wakati wa kiangazi au bado milima hiyo huwa na theluji? Mwalimu huyo alitabasamu tulipowaonyesha picha zetu zenye rangi, tofauti na zao ambazo hazikuwa na rangi.

Mke wa mwalimu huyo, ambaye pia ni msaidizi wake alituuliza maswali mara kwa mara, “Je, mnajua kuimba kwa njia ya yodel?” * La hatuwezi. Lakini, tukifahamu jinsi Waamishi wanavyojua kuimba kwa njia ya yodel, tuliwaomba watuimbie wimbo mmoja. Walikubali, kwa hiyo tukasikiliza kwaya yenye waimbaji 40. Kisha mwalimu akawapa wanafunzi ruhusa waende mapumziko.

Mke wa mwalimu huyo alituomba tuwaimbie wimbo. Tulikubali kufanya hivyo, kwa kuwa tulijua nyimbo kadhaa za kitamaduni katika Kijerumani cha Uswisi. Mara moja wanafunzi walisikia tukiimba nao wote wakarudi darasani. Kwa kuwa tulikuwa tumesimama mbele ya darasa, tulijitahidi kuwaimbia vizuri.

Baadaye tulialikwa kula mlo wa mchana na familia moja ya watu 12. Juu ya meza ya mbao, kulikuwa na vyakula vyenye kupendeza sana—viazi vilivyopondwa-pondwa, nyama ya paja la nguruwe, mahindi, mkate, jibini, mboga, keki, na aina nyingine ya vitinda-mlo. Kabla ya kuanza kula, kila mtu alitoa sala ya kimyakimya. Tulipokuwa tukiendelea kula, tulizungumza kuhusu Uswisi, nchi ambayo mababu zao walitoka, nao walitueleza kuhusu maisha ya shambani. Watoto walinong’onezana na kuchekacheka kwa sauti ya chini hadi tulipomaliza mlo. Kila mtu alipomaliza kula, sala ya pili ilitolewa ikiwa ishara kuwa watoto wanaruhusiwa kuondoka mezani—lakini si kwenda kucheza. Kila mmoja alikuwa na mgawo wa kuondoa vyombo mezani na kuviosha, hilo lilimaanisha kuteka maji kutoka kwenye kisima na kuyapasha moto.

Watoto walipokuwa wakiosha vyombo, wazazi walitupeleka sebuleni. Hakukuwa na sofa, lakini tulikalia viti vyenye kustarehesha vinavyobembea vilivyotengenezwa kwa mbao. Walitoa Biblia nzee ya Kijerumani, na kama ilivyo kawaida ya familia nyingi za Waamishi, tulianza kuzungumzia Biblia. Ni nini kusudi la Yehova Mungu kwa dunia na wanadamu? Yesu alimaanisha nini aliposema kuwa wapole watairithi dunia? Je, Mungu anapanga kuwatesa watu waovu milele katika moto wa mateso? Ni nani anayetii agizo la Yesu la kuhubiri habari njema kwa watu wote duniani? Kuzungumzia maswali yote hayo na mengine mengi pamoja na watu wanaothamini kweli za Biblia wakiwa wameshika Biblia yao mkononi kulituletea furaha kwelikweli.

Tunapokumbuka safari hiyo ya kuchunguza mambo ya kale, tunafurahi sana kwani ilikuwa imejaa mambo mengi mazuri. Tunasali na kutumaini kwamba safari yetu na mazungumzo tuliyokuwa nayo katika Kijerumani cha Uswisi, yaliwapa wote waliotukaribisha fursa ya kupata ujuzi sahihi wa kweli zinazopatikana katika Neno la Mungu, Biblia.

[Maelezo ya chini]

^ fu. 15 Kuimba kwa njia ya yodel ni kuimba kwa kuinua sauti kana kwamba mtu anapiga vigelegele.