Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Kwa nini kitabu cha Kwanza cha Wakorintho kinazungumza kuhusu nyama iliyotolewa dhabihu kwa sanamu?

Mtume Paulo aliandika: “Endeleeni kula kila kitu kinachouzwa katika soko la nyama, bila kuchunguza kwa sababu ya dhamiri yenu.” (1 Wakorintho 10:25) Nyama hizo zilitoka wapi?

Dhabihu za wanyama zilikuwa sehemu muhimu ya sherehe katika mahekalu ya Wagiriki na Waroma, lakini nyama yote iliyotolewa dhabihu haikuliwa wakati wa sherehe. Hivyo, nyama iliyobaki kwenye mahekalu hayo ya kipagani iliuzwa sokoni. Kitabu kimoja (Idol Meat in Corinth) kinasema: “Viongozi wa madhehebu . . . nyakati nyingine wanaitwa wapishi na/au wachinjaji. Nyama waliyopewa kama malipo kwa kuchinja mnyama aliyetolewa dhabihu, waliiuza sokoni.”

Kwa hiyo, si nyama zote zilizouzwa sokoni ambazo zilikuwa mabaki ya nyama zilizotumiwa katika sherehe za kidini. Kwa kuwa, viunzi vizima vya mifupa ya kondoo vilichimbuliwa katika eneo la soko la nyama (Kilatini, macellum) la Pompeii. Msomi Henry J. Cadbury anasema jambo hilo linadokeza kwamba “huenda nyama zilizouzwa ni za wanyama hai au wanyama waliochinjwa kwenye macellum na pia nyama za wanyama waliochinjwa au kutolewa dhabihu hekaluni.”

Paulo alikuwa akitoa hoja kwamba ingawa Wakristo hawangeshiriki katika ibada ya kipagani, kimsingi nyama iliyotolewa dhabihu hekaluni haikuwa imetiwa unajisi.

Kwa nini kulikuwa na utengano kati ya Wayahudi na Wasamaria wa siku za Yesu?

Andiko la Yohana 4:9 linasema kuwa ‘Wayahudi hawakuwa na shughuli na Wasamaria.’ Yaonekana utengano huo ulianza wakati Yeroboamu alipoanzisha ibada ya sanamu katika ufalme wa kaskazini wa makabila kumi ya Israeli. (1 Wafalme 12:26-30) Wasamaria walikuwa wakaaji wa Samaria, jiji kuu la ufalme wa kaskazini. Baadaye wakaaji wote wa ufalme wa kaskazini waliitwa Wasamaria. Waashuru walipoteka makabila kumi ya ufalme huo mwaka wa 740 K.W.K., walileta wapagani kutoka nchi nyingine wawe wakaaji wa eneo lote la ufalme wa kaskazini. Watu hao walioana na Wasamaria na hivyo ibada ya Wasamaria ikapotoshwa hata zaidi.

Karne nyingi baadaye, Wasamaria walipinga juhudi za Wayahudi waliorudi kutoka uhamishoni Babiloni za kujenga hekalu la Yehova na kuta za jiji la Yerusalemu. (Ezra 4:1-23; Nehemia 4:1-8) Ushindani wa kidini uliongezeka wakati Wasamaria walipojenga hekalu lao wenyewe kwenye Mlima Gerizimu, yapata karne ya nne K.W.K.

Siku za Yesu neno “Msamaria” lilihusianishwa zaidi na dini kuliko eneo, na lilitumiwa kurejelea mshiriki wa madhehebu iliyokuwa imeenea sana Samaria. Wasamaria bado waliabudu kwenye Mlima Gerizimu, na Wayahudi waliwadharau sana.—Yohana 4:20-22; 8:48.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Sahani ya udongo iliyo na picha ya watu wakitoa dhabihu ya wanyama katika karne ya sita K.W.K.

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris

[Picha katika ukurasa wa 12]

Yeroboamu alianzisha ibada ya sanamu