Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Mtume Paulo alimaanisha nini aliposema kwamba alikuwa na “alama za mtumwa wa Yesu” mwilini mwake?—Wagalatia 6:17.

▪ Yawezekana wasikilizaji wa karne ya kwanza walielewa maneno ya Paulo kwa njia mbalimbali. Kwa mfano, zamani, chuma cha moto kilitumika kuwatia alama wafungwa wa vita, watu walioiba mahekaluni, na watumwa waliotoroka. Watu waliona alama kama hiyo kwenye mwili wa mwanadamu kuwa ishara isiyo ya heshima.

Hata hivyo, si wakati wote alama hizo zilionekana kuwa ishara isiyo ya heshima. Watu wengi wa zamani walitumia alama hizo kuonyesha kabila lao au dini yao. Kwa mfano, kulingana na kamusi moja, (Theological Dictionary of the New Testament), “Wasiria walionyesha kuwa wamejitoa kwa miungu ya Hadadi na Atargatisi kwa kutiwa alama kwenye kifundo cha mikono au shingo zao . . . Mwabudu wa Dionisio alitiwa alama ya jani la mwefeu.”

Wachunguzi wengi wa siku hizi wanafikiri kwamba Paulo alikuwa akizungumzia makovu yaliyotokana na mapigo mbalimbali aliyopata akiwa mmishonari Mkristo. (2 Wakorintho 11:23-27) Hata hivyo, huenda Paulo alimaanisha kuwa njia yake ya maisha—bali si alama halisi mwilini mwake—ndiyo iliyomtambulisha kuwa Mkristo.

Je, majiji ya makimbilio katika Israeli la kale yalikuwa maficho ya wahalifu?

▪ Katika ulimwengu wa kale wa kipagani, mahekalu mengi yalikuwa maficho ya wahalifu na watu waliotoroka. Pia, katika enzi za kati makao ya watawa na makanisa ya dini zinazojidai kuwa za Kikristo, yalikuwa maficho ya wahalifu. Hata hivyo, sheria zilizotumiwa kuhusiana na majiji ya makimbilio ya Israeli la kale zilihakikisha kwamba wahalifu hawakujificha katika majiji hayo.

Sheria ya Musa ilisema kuwa majiji ya makimbilio yalikusudiwa tu kuandaa ulinzi kwa mtu aliyeua bila kukusudia. (Kumbukumbu la Torati 19:4, 5) Mtu huyo angekimbilia jiji la makimbilio lililo karibu, ili mwanamume wa ukoo wa mtu aliyeuawa asilipize damu iliyomwagwa. Baada ya kesi yake kusikilizwa na wanaume wazee wa jiji la makimbilio, mtu huyo aliyeua angepelekwa ili kuhukumiwa katika jiji linalosimamia eneo ambapo alitenda kitendo hicho. Hapo alikuwa na nafasi ya kuthibitisha kuwa hana hatia. Wazee walichunguza uhusiano kati ya mtu aliyeuawa na mtu aliyeua ili kujua kama walikuwa na uadui wowote kabla ya mauaji hayo.—Hesabu 35:20-24; Kumbukumbu la Torati 19:6, 7; Yoshua 20:4, 5.

Ikiwa hakuwa na hatia, mtu huyo angerudi katika jiji la makimbilio na kuishi katika eneo la jiji hilo. Majiji hayo hayakuwa magereza. Wakimbizi walifanya kazi na kutumika kama washiriki wa jamii ya eneo hilo. Kuhani mkuu alipokufa, wakimbizi wote wangeweza kuondoka katika majiji ya makimbilio na kurudi makwao bila hofu.—Hesabu 35:6, 25-28.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MAJIJI YA MAKIMBILIO

1 KEDESHI

2 GOLANI

3 RAMOTHI-GILEADI

4 SHEKEMU

5 BESERI

6 HEBRONI

Mto Yordani