Ona video zinazopatikana

Ona habari zilizo ndani

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Kwa kuwa Israeli ina majira marefu ya ukame, wakaaji wake wa nyakati za kale walitumia mbinu gani kuhakikisha kuwa wanapata maji ya kutosha?

Israeli inapata mvua kati ya mwezi wa Oktoba (Mwezi wa 10) na Aprili (Mwezi wa 4), na nyakati nyingine maji ya mvua hutiririka kwa kasi kwenye mabonde ya mito. Hata hivyo, wakati wa kiangazi, mingi ya “mito” hiyo hukauka, na huenda mvua isinyeshe kwa miezi mingi. Kwa hiyo, watu wa nyakati za Biblia walitumia mbinu gani kuhakikisha kuwa wanapata maji ya kutosha?

Walitatua tatizo hilo kwa kuchimba mitaro kwenye milima na kuelekeza maji ya mvua ya majira ya baridi kali kwenye mashimo ya chini ya ardhi, au matangi ya maji. Paa zilijengwa zikiwa zimeinama vya kutosha ili kuelekeza maji ya mvua kwenye matangi hayo. Familia nyingi zilikuwa na tangi la kuhifadhia maji ambayo wangeweza kuyatumia kukata kiu.—2 Wafalme 18:31; Yeremia 6:7.

Waisraeli pia walitumia chemchemi kupata maji. Katika maeneo yaliyoinuka, mvua ya majira ya baridi kali hupenya chini kwenye udongo na kufikia miamba isiyoweza kupenya maji. Maji hayo hutiririka juu ya miamba hiyo na hatimaye kutokea kama chemchemi. Vijiji vingi vilijengwa karibu na chemchemi (Kiebrania, en) na hilo linadokezwa na majina ya maeneo kama vile En-shemeshi, En-rogeli, na En-gedi. (Yoshua 15:7, 62) Huko Yerusalemu bomba lilichimbwa kwenye jiwe ili kupeleka maji ya chemchemi jijini.—2 Wafalme 20:20.

Mahali ambapo hapakuwa na chemchemi, watu walichimba kisima (Kiebrania, beʼerʹ), kama kile kilichoko Beer-sheba, ili kupata maji ya chini ya ardhi. (Mwanzo 26:32, 33) Mwandishi André Chouraqui anasema kuwa “mbinu walizotumia [Waisraeli] kutatua tatizo la ukosefu wa maji zinavutia sana hata sasa.”

Yaelekea Abramu (Abrahamu) aliishi katika nyumba ya aina gani?

Abramu na mke wake waliishi katika jiji la Wakaldayo la Uru lenye ufanisi. Lakini kwa kutii agizo la Mungu, waliondoka katika jiji hilo na kuanza kuishi katika mahema. (Mwanzo 11:31; 13:12) Fikiria mambo ambayo huenda walihitaji kudhabihu ili kutii agizo hilo.

Uru, ambalo sasa ni eneo la Iraq ya kisasa, lilichimbuliwa na Leonard Woolley kati ya mwaka wa 1922 na 1934. Kati ya majengo aliyopata, kulikuwa na nyumba 73 zilizojengwa kwa matofali. Vyumba vingi katika nyumba hizo vilikuwa vimejengwa kuzunguka uga, au sehemu ya katikati iliyokuwa na sakafu ya mawe. Sakafu hiyo ilitengenezwa ikiwa imeinama kidogo kuelekea sehemu ya katikati, ambapo palikuwa na shimo la kuondolea maji machafu. Katika nyumba zilizokuwa kubwa kidogo, vyumba vya wageni vilikuwa na vyoo ndani. Chini ya vyumba vilivyokuwa juu kulikuwa na vyumba vya watumwa na vyumba vya kupikia vyenye majiko. Familia ilikaa katika vyumba vya juu na ilitumia ngazi kufika kwenye vyumba hivyo. Ngazi hizo zilimfikisha mtu kwenye roshani ya mbao iliyokuwa imejengwa kuzunguka uga. Walitembea kwenye roshani hiyo ili kufika kwenye milango ya vyumba hivyo vya juu.

“Nyumba . . . , yenye uga wa mawe na kuta zilizopakwa chokaa vizuri, yenye mfumo wa kuondolea maji machafu, . . . na vyumba 12 au zaidi, inaonyesha watu waliishi maisha ya juu sana,” akaandika Woolley. “Na hizo ndizo nyumba . . . zilizomilikiwa na watu wasio matajiri sana, wenye maduka, wafanyabiashara ndogondogo, waandishi, na wengineo.”

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kisima, Horvot Mezada, Israeli

[Hisani]

© Masada National Park, Israel Nature and Parks Authority

[Picha katika ukurasa wa 19]

Mchoro wa nyumba katika siku za Aabrahamu

[Hisani]

© Drawing: A. S. Whitburn