Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unabii wa 1. Matetemeko ya Nchi

Unabii wa 1. Matetemeko ya Nchi

Unabii wa 1. Matetemeko ya Nchi

“Kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi.”—LUKA 21:11.

● Winnie, mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu hivi, anaokolewa kwenye mabaki ya nyumba iliyobomoka nchini Haiti. Wapiga picha wa kituo fulani cha televisheni, wanaoripoti kuhusu msiba huo, walimsikia akilia kwa sauti hafifu chini ya mabomoko hayo. Anaokoka tetemeko hilo, lakini wazazi wake wanakufa.

MAMBO ya HAKIKA YANAONYESHA NINI? Inakadiriwa kuwa watu zaidi ya 300,000 walikufa wakati tetemeko la nchi lenye kipimo cha 7.0 lilipotokea nchini Haiti mnamo Januari (Mwezi wa 1) 2010. Wengine milioni 1.3 waliachwa bila makao kwa ghafula. Ingawa tetemeko hilo lilikuwa kubwa sana, halikuwa ndilo tetemeko pekee duniani. Matetemeko makubwa ya nchi yapatayo 18 yalitokea kote duniani kati ya Aprili (Mwezi wa 4) 2009 na Aprili 2010.

NI KIPINGAMIZI GANI KINACHOTOLEWA MARA NYINGI? Matetemeko ya nchi si mengi kuliko zamani; yanaonekana kuwa mengi kwa sababu tekinolojia ya kisasa inatuwezesha kupata habari nyingi zaidi kuyahusu kuliko hapo zamani.

JE, KIPINGAMIZI HICHO KINA MSINGI? Fikiria jambo hili: Biblia haikazii idadi ya matetemeko ya nchi yanayotokea katika siku za mwisho. Hata hivyo, inasema kuwa “matetemeko makubwa ya nchi” yatatokea “katika mahali pamoja baada ya pengine,” na hivyo kuyafanya kuwa sehemu ya maana ya kipindi hiki muhimu katika historia.—Marko 13:8; Luka 21:11.

UNA MAONI GANI? Je, tunaona matetemeko makubwa ya nchi, kama Biblia ilivyotabiri?

Huenda matetemeko ya nchi pekee yasiwe uthibitisho wa kutosha kuwa tunaishi katika siku za mwisho. Hata hivyo, matetemeko hayo ni sehemu moja tu ya unabii unaotimia. Fikiria unabii wa pili.

[Blabu katika ukurasa wa 4]

“Sisi [wanajiofizikia] tunayaita matetemeko makubwa ya nchi. Wengine wanayaita misiba mikubwa.”​—KEN HUDNUT, SHIRIKA LA MAREKANI LA UCHUNGUZI WA KIJIOLOJIA.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]

© William Daniels/Panos Pictures