Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ufisadi—Umeenea Kwa Kadiri Gani?

Ufisadi—Umeenea Kwa Kadiri Gani?

“Kampuni yetu inatoa huduma kwa mamlaka ya mji fulani. Mara nyingi tunasuburi kwa miezi miwili au mitatu ili kupata malipo ya huduma tunazotoa. Hata hivyo, hivi karibuni nilipigiwa simu na mmoja wa wafanyakazi wa mamlaka hiyo. Alitaka kunisaidia kupata malipo yetu bila kuchelewa ikiwa ningekubali kumpa kiasi fulani cha pesa kama rushwa.”—JOHN. *

JE, UMEWAHI kuathiriwa na ufisadi? Labda si ufisadi kama uliotajwa hapo juu, lakini bila shaka ulipatwa na matokeo mabaya ya ufisadi.

Kulingana na Orodha ya 2011 ya Makadirio ya Ufisadi, * iliyotolewa na shirika la Transparency International (TI), ‘Nyingi kati ya nchi 183 zilizoorodheshwa zilikuwa na kiwango cha ufisadi kisichozidi 5. Kulingana na makadirio hayo, kiwango cha 0 kiliwakilisha nchi zenye ufisadi mwingi na kiwango cha 10 kiliwakilisha nchi zisizo na ufisadi.’ Miaka miwili mapema, shirika la TI lilitaja katika ripoti yake ya kila mwaka ya 2009 kuwa ufisadi umeenea sana liliposema: “Ni wazi kwamba hakuna sehemu yoyote ulimwenguni ambayo haijaathiriwa na ufisadi.”

“Ufisadi ni matumizi mabaya ya mamlaka ili kupata faida za kibinafsi. Ufisadi huathiri kila mtu ambaye maisha yake, riziki yake au furaha yake inategemea unyoofu wa watu wenye mamlaka.”​—SHIRIKA LA TRANSPARENCY INTERNATIONAL

Katika hali fulani, matokeo ya ufisadi yanaweza kuwa mabaya sana. Kwa mfano, gazeti Time lilisema kwamba “ufisadi na kutojali” ndiyo mambo yaliyosababisha kwa kiasi fulani vifo vya watu wengi baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba nchi ya Haiti mwaka wa 2010. Liliendelea kusema: “Majengo hujengwa kwa usaidizi mdogo au bila usaidizi wa wahandisi, na wale wanaoitwa wakaguzi wa serikali hupokea rushwa kwa wingi.”

Je, inawezekana kukomesha kabisa ufisadi? Ili tupate jibu, tunahitaji kuelewa mambo ya msingi yanayosababisha ufisadi. Tutachunguza mambo hayo katika makala inayofuata.

^ fu. 2 Jina limebadilishwa.

^ fu. 4 “Orodha ya Makadirio ya Ufisadi hupanga nchi kulingana na kiwango cha ufisadi kinachodhaniwa katika idara za umma.”—Transparency International.