Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Kwa nini hairuhusiwi kuweka machapisho ya Mashahidi wa Yehova kwenye tovuti ya kibinafsi au kwenye mitandao ya kijamii?

Kwa kuwa machapisho yetu hutolewa bila malipo, wengine huhisi kwamba ni jambo linalokubalika kuyanakili na kuyaweka kwenye tovuti nyingine au kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo, kufanya hivyo kunakiuka Masharti ya Matumizi * ya tovuti zetu na kumesababisha matatizo makubwa. Kama inavyotajwa wazi katika Masharti hayo, hakuna yeyote anayeruhusiwa “kuweka michoro, machapisho ya kielektroni, nembo au alama za usajili, muziki, picha, video, au makala kwenye Intaneti kutoka kwenye tovuti hii (iwe ni katika tovuti, kituo cha kushiriki faili au video, au mtandao wa kijamii).” Kwa nini masharti kama hayo yanahitajika?

Hakuna yeyote anayeruhusiwa kuweka machapisho yetu ambayo yanalindwa na haki ya kunakili kwenye vituo vya Intaneti

Habari zote zilizo katika tovuti zetu zinalindwa na haki ya kunakili. Waasi imani na wapinzani wengine huweka machapisho yetu kwenye tovuti zao ili kuwavuta kwa ujanja Mashahidi wa Yehova na watu wengine. Tovuti hizo zina habari fulani zilizokusudiwa kupanda shaka akilini mwa wasomaji. (Zab. 26:4; Met. 22:5) Wengine wametumia habari zilizo katika machapisho yetu au nembo ya jw.org kwenye matangazo, bidhaa za biashara, na programu kwa ajili ya vifaa vya mkononi. Kwa kuwa tuna haki ya kunakili na nembo au alama za usajili, tuna msingi wa kisheria wa kuzuia matumizi hayo yasiyofaa. (Met. 27:12) Lakini ikiwa tutawaruhusu watu, hata ndugu zetu, waweke habari zilizo katika tovuti zetu kwenye tovuti nyingine au kutumia nembo ya jw.org kuuza bidhaa, mahakama zinaweza kukataa kuunga mkono jitihada zetu za kuwazuia wapinzani au mashirika ya kibiashara kutumia tovuti zetu kwa njia isiyofaa.

Vyanzo pekee vinavyoaminika vya kusambaza chakula cha kiroho:

Kupakua machapisho yetu kwenye tovuti nyingine yoyote isipokuwa jw.org ni hatari. Yehova amempa “mtumwa mwaminifu na mwenye busara” pekee jukumu la kuandaa chakula cha kiroho. (Mt. 24:45) “Mtumwa” huyo ana tovuti rasmi za kusambaza chakula cha kiroho, yaani, www.pr418.com, tv.pr418.com, na wol.pr418.com. Na tuna programu tatu tu rasmi kwa ajili ya vifaa vya mkononi, yaani, JW Language®, JW Library®, na JW Library Sign Language®. Tunaweza kuwa na uhakika kwamba tovuti na programu hizo hazina matangazo yoyote na hazijachafuliwa na ulimwengu wa Shetani. Ikiwa tunapokea chakula cha kiroho kutoka katika chanzo kingine, hatuwezi kuwa na uhakika kwamba hakijabadilishwa au kuchafuliwa.—Zab. 18:26; 19:8.

Isitoshe, kuweka machapisho yetu kwenye tovuti zinazowaruhusu wasomaji kutoa maoni yao, huwapa nafasi waasi imani na wachambuzi wengine kupanda shaka kuelekea tengenezo la Yehova. Baadhi ya akina ndugu wamevutwa kwenye mijadala inayofanywa kwenye mitandao, jambo ambalo limefanya jina la Yehova lizidi kuchafuliwa. Kushiriki katika mijadala inayofanywa mtandaoni si njia inayofaa ya “[kuwafundisha] kwa upole wale wasio na mwelekeo unaofaa.” (2 Tim. 2:23-25; 1 Tim. 6:3-5) Pia, imeonekana kwamba tovuti na akaunti bandia za mitandao ya kijamii zimeanzishwa kwa kutumia jina la tengenezo, Baraza Linaloongoza, au mshiriki mmojammoja wa Baraza hilo. Hata hivyo, hakuna mshiriki wa Baraza Linaloongoza aliye na ukurasa wake binafsi mtandaoni au mwenye akaunti katika mtandao wowote wa kijamii.

Kuwaelekeza watu kwenye tovuti ya jw.org husaidia kueneza “habari njema.” (Mt. 24:14) Programu na tovuti tunazotumia katika huduma huboreshwa mara kwa mara. Tungependa kila mtu anufaike nazo. Hivyo, kama inavyoonyeshwa kwenye Masharti ya Matumizi, unaweza kumtumia mtu chapisho la kielektroni kupitia barua-pepe au kumtumia kiunganishi kitakachomwelekeza kwenye habari inayopatikana kwenye Tovuti ya jw.org. Tunapowaongoza watu wenye kupendezwa kwenye tovuti zetu rasmi, tunawaelekeza kwa “mtumwa mwaminifu na mwenye busara” ambaye ndiye chanzo hasa cha chakula cha kiroho.

^ fu. 1 Kiunganishi kinachomwelekeza mtu kwenye ukurasa wa Masharti ya Matumizi kinapatikana kwenye sehemu ya chini ya ukurasa wa mwanzo wa Tovuti ya jw.org, na masharti hayo yanahusu kila kitu kinachopatikana katika tovuti zetu.