Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Mwanafunzi Stefano alifanikiwaje kuendelea kuwa mtulivu alipokuwa akiteswa?

STEFANO alikabili kundi la wanaume wenye hasira kali. Wanaume hao 71 waliotumikia kama waamuzi, walikuwa washiriki wa mahakama kuu zaidi katika Israeli, yaani, Sanhedrini, na walikuwa miongoni mwa watu wenye mamlaka zaidi wa taifa hilo. Kuhani Mkuu Kayafa ambaye miezi michache mapema alikuwa amesimamia mahakama hiyo Yesu alipohukumiwa kifo, ndiye aliyekuwa amewakusanya tena wanaume hao. (Mt. 26:57, 59; Mdo. 6:8-12) Walipokuwa wakiwaleta mashahidi wa uwongo mbele yao, mmoja baada ya mwingine, wanaume hao walitambua jambo fulani la ajabu kumhusu Stefano kwamba uso wake ulikuwa “kama uso wa malaika.”—Mdo. 6:13-15.

Stefano alifanikiwaje kuendelea kuwa mtulivu na bila wasiwasi chini ya hali hiyo yenye kutia woga? Kabla ya kukokotwa mbele ya Sanhedrini, Stefano alikuwa amezama kabisa katika huduma yake, akiongozwa na roho ya Mungu yenye nguvu. (Mdo. 6:3-7) Alipokuwa akishtakiwa, roho hiyohiyo ilikuwa ikitenda kazi ndani yake kama mfariji na kama mkumbushaji. (Yoh. 14:16, maelezo ya chini) Stefano alipokuwa akijitetea kwa ujasiri, kama tunavyosoma kwenye kitabu cha Matendo sura ya 7, roho takatifu ilimkumbusha vifungu 20 hivi au zaidi vya Maandiko ya Kiebrania. (Yoh. 14:26) Lakini imani ya Stefano iliimarishwa hata zaidi alipomwona Yesu katika maono akiwa amesimama kwenye mkono wa kuume wa Mungu.—Mdo. 7:54-56, 59, 60.

Huenda siku moja sisi pia tutakabili vitisho na mateso. (Yoh. 15:20) Ikiwa tutajilisha Neno la Mungu kwa ukawaida na kushiriki kikamili katika huduma, tutairuhusu roho ya Yehova itende kazi ndani yetu. Pia, tutapata nguvu za kukabiliana na upinzani wowote huku tukiendelea kuwa na amani ya akili.—1 Pet. 4:12-14.