Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Katika nyakati za zamani, msafiri alipangaje safari zake za baharini?

KWA ujumla, katika siku za Paulo hakukuwa na meli za abiria. Kwa kawaida, msafiri angewauliza watu wengine ikiwa wana habari kuhusu meli yoyote ya mizigo iliyokuwa ikisafiri kwenda upande aliotaka kwenda na ikiwa abiria waliruhusiwa kuipanda. (Mdo. 21:2, 3) Hata ikiwa meli haikuwa ikisafiri kwenda mahali hususa ambapo msafiri alitaka kufika, meli hiyo iliposimama kwenye bandari fulani ikiwa safarini, msafiri angetafuta meli nyingine ambayo ingemsaidia kufika karibu zaidi na mahali alipotaka kwenda.​—Mdo. 27:1-6.

Usafiri wa baharini ulikuwa wa msimu, na meli hazikufuata ratiba fulani hususa ya usafiri. Mbali na hali mbaya ya hewa, mabaharia washirikina wangeahirisha safari yao ikiwa wangeona ishara ya bahati mbaya kama vile kunguru akitoa milio yake akiwa kwenye kamba zinazoshikilia matanga, au ikiwa wangeona mabaki ya meli iliyozama ufuoni mwa bahari. Mabaharia wangesubiri hadi pepo za bahari zivume kuelekea upande waliokuwa wakielekea, kisha wangeng’oa nanga. Msafiri alipopata meli iliyokubali kubeba abiria, alikaa karibu na bandari pamoja na mizigo yake akisubiri tangazo litolewe kwamba meli iko karibu kuanza safari.

Mwanahistoria Lionel Casson anasema hivi: “Jiji la Roma lilikuwa na huduma zilizowasaidia wasafiri kupata meli kwa urahisi, hivyo hawakulazimika kwenda huku na kule bandarini wakitafuta meli. Bandari ya jiji hilo ilikuwa kwenye mlango wa Mto Tiber. Katika jiji la Ostia lililokuwa karibu, kulikuwa na uwanja mkubwa uliozungukwa na ofisi mbalimbali. Idadi kubwa ya ofisi hizo zilikuwa za wasafirishaji wa mizigo waliowakilisha bandari tofauti-tofauti: Kulikuwa na ofisi ya bandari ya Narbonne [sasa ni Ufaransa], ofisi ya bandari ya Carthage [sasa ni Tunisia], . . . na kadhalika. Mtu yeyote aliyetaka kusafiri alihitaji tu kwenda kwenye ofisi zilizosimamia meli zilizopita kwenye majiji yaliyokuwa kwenye upande aliotaka kwenda.”

Usafiri wa baharini uliwasaidia wasafiri kuokoa muda, lakini ulikuwa hatari pia. Mara kadhaa, Paulo alivunjikiwa na meli alipokuwa katika safari zake za umishonari.​—2 Kor. 11:25.