Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Polisi wa Kiyahudi wa hekaluni walikuwa nani? Walifanya kazi gani?

Mojawapo ya majukumu mengi yaliyoshughulikiwa na watu wa kabila la Lawi ambao hawakuwa makuhani lilikuwa kutumikia katika utumishi unaofanana na wa maofisa wa polisi. Kikosi hicho kilikuwa chini ya uongozi wa kapteni wa hekalu. Philo, mwandishi Myahudi anafafanua hivi majukumu ya maofisa hao: “Baadhi yao [Walawi] wamepewa kazi ya kusimama kwenye miingilio wakiwa walinda malango, wengine kwenye [eneo la hekalu] mbele ya mahali patakatifu ili kumzuia yeyote asiyeruhusiwa na sheria kuingia mahali hapo, iwe anafanya hivyo kimakusudi au la. Wengine wanalinda doria kwa zamu wakipokezana usiku na mchana.”

Kikosi hicho cha polisi kilikuwa tayari kulitumikia baraza la Sanhedrini. Hicho ndicho kikosi pekee cha Wayahudi kilichobeba silaha ambacho Waroma walikiruhusu kufanya kazi.

Kulingana na msomi Joachim Jeremias, “Maneno ya kushutumu ambayo Yesu alitamka alipokamatwa, kwamba siku baada ya siku alikuwa hekaluni akifundisha lakini hakukamatwa (Mt. 26:55), yanaeleweka waziwazi zaidi ikiwa polisi wa Hekaluni ndio waliokuja kumkamata.” Msomi huyo anaamini kwamba wale waliotumwa ili kumkamata Yesu hapo awali walikuwa pia polisi wa hekaluni. (Yoh. 7:32, 45, 46) Baadaye, maofisa pamoja na kapteni wao walitumwa na Sanhedrini wawalete wanafunzi wa Yesu mbele yao, na inaonekana kwamba walihusika wakati mtume Paulo alipokokotwa nje ya hekalu.—Mdo. 4:1-3; 5:17-27; 21:27-30.