Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SIERRA LEONE NA GUINEA

Mtu wa Mnara wa Mlinzi

James Koroma

Mtu wa Mnara wa Mlinzi
  • ALIZALIWA 1966

  • ALIBATIZWA 1990

  • MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alikuwa mjumbe wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

MNAMO 1997, wanajeshi waasi walipokuwa wakipigana na majeshi ya serikali katika jiji la Freetown, nilijitolea kubeba barua kutoka Freetown hadi kwenye ofisi ya tawi ya muda iliyokuwa jijini Conakry, nchini Guinea.

Nilipanda basi kwenye kituo cha mabasi pamoja na kikundi cha watu wengine. Tulisikia milio ya bunduki kwa mbali, jambo hilo lilituogopesha sana. Kadiri tulivyozidi kupita katika barabara za jiji, ndivyo tulivyozidi kusikia risasi zikifyatuliwa kila mahali. Dereva wa basi tulilopanda aligeuza mwelekeo wa basi na kufuata njia nyingine. Muda mfupi baadaye, tulisimamishwa na kikundi cha waasi waliokuwa wamebeba bunduki na kutuamuru tutoke kwenye basi. Baada ya kutuuliza maswali, wakaturuhusu tuendelee na safari. Baadaye tena, tulisimamishwa na kikundi kingine cha wanajeshi. Kwa kuwa mmoja wa abiria alimjua kamanda wa kikundi hicho, wao pia walituruhusu tuendelee na safari yetu. Tulipofika mwishoni mwa mji, tukakutana na kikundi cha tatu cha waasi ambao walituuliza maswali na kisha wakatuamuru tuendelee na safari. Tulipokuwa tukiendelea na safari kuelekea kaskazini, tulipita vizuizi vingine vingi barabarani hadi basi hilo lililopigwa na vumbi lilipowasili jijini Conakry siku hiyo jioni.

Katika safari zilizofuata nilibeba maboksi ya machapisho, vifaa vya ofisini, rekodi za ofisi ya tawi, na misaada. Mara nyingi nilisafiri kwa gari au mabasi madogo ya abiria. Lakini pia, nilitumia mitumbwi mahali penye mito, na vijana wabeba mizigo ili kubeba machapisho katikati ya misitu yenye mvua nyingi.

Pindi fulani, nilipokuwa nimebeba vifaa vya ofisi kutoka jijini Freetown kwenda jiji la Conakry, basi letu lilisimamishwa mpakani na wanajeshi waasi. Mmoja wa waasi hao alikagua mzigo wangu na kuanza kunitilia shaka na kuniuliza maswali. Wakati huohuo, nilimwona mtu ambaye nilisoma naye zamani akiwa miongoni mwa waasi hao. Wanajeshi wenzake walimwita Mhuni, na ndiye aliyekuwa mkatili zaidi katika kikundi hicho. Nilimwambia askari huyo aliyekuwa akiniuliza maswali kwamba nilikuja kumwona Mhuni, na kisha nikamwita. Mhuni alinitambua mara moja na akaja mahali nilipokuwa. Tulikumbatiana na kucheka. Kisha sura yake ikabadilika.

Akaniuliza: “Una tatizo lolote?”

Nikamjibu: “Nataka kuvuka mpaka niingie nchini Guinea.”

Mara moja akawaamuru wanajeshi hao waliruhusu basi letu lipite bila kukaguliwa.

Kuanzia siku hiyo na kuendelea, kila nilipofika kwenye kituo hicho cha ukaguzi, Mhuni aliwaamuru wanajeshi hao waniruhusu nipite. Niliwapa wanajeshi hao magazeti, nao walithamini sana. Baada ya muda mfupi, wakaanza kuniita Mtu wa Mnara wa Mlinzi.