Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 MATUKIO MUHIMU YA MWAKA ULIOPITA

Video za Vibonzo Zagusa Mioyo Minyofu

Video za Vibonzo Zagusa Mioyo Minyofu

Kalebu, mvulana mdogo katika mfululizo wa video Uwe Rafiki ya Yehova kwenye tovuti ya jw.org, anajulikana sana ulimwenguni pote. Video hiyo ya kwanza ya mvulana huyo mwenye shauku imetafsiriwa katika lugha zaidi 130, na tumepokea barua nyingi zinazohusu video hiyo.

Barua ifuatayo ilitumwa na mtoto wa umri wa miaka 11 na dada yake mwenye umri wa miaka 8: “Tungependa kutoa mchango kwa ajili ya kazi ya kuhubiri ulimwenguni pote. Tulipata pesa hizo kwa kuuza ndama wawili tuliowafuga. Ndama hao walikuwa wanaitwa Big Red na Earl. Tulitaka kuwapa pesa hizo ili mzitumie kutengeneza filamu nyingine za Uwe Rafiki ya Yehova. Ingependeza ikiwa Kalebu atapata dada yake mdogo ili aache kukaziwa fikira sana. Tunaipenda sana filamu ya Kalebu!”

Watoto wengi wamekariri video nzima, kutia ndani wimbo na hata maelezo ya msimuliaji. Dada mmoja aliandika kwamba kutaniko lao lenye wahubiri 100 lina watoto 40, wengi wao wana umri wa miaka chini ya 10. Alikuwa kwenye safu ya tatu wimbo namba 120 ulipokuwa ukiimbwa mwishoni mwa mkutano. Alitokwa na machozi aliposikia watoto wote wakiimba “wimbo wao” kwa shauku kubwa.

Nyanya (bibi) mmoja anaeleza kwamba baada ya mjukuu wake kutazama video hiyo mara mbili, alisema hivi: “Nitasafisha chumba changu ili vitu vyangu vya kuchezea visimwangushe mtu yeyote.” Alijitahidi sana kutimiza lengo lake hivi kwamba alisisitiza kuwa ni lazima asafishe chumba chake kabla hajaanza kula.

Katika kijiji fulani nchini Afrika Kusini, kila siku watoto wengi walikuwa wakiingia na kutoka kwenye nyumba ya Shahidi mmoja. Watu walidhani ni kwa sababu familia hiyo ilikuwa ikiuza peremende. Kumbe watoto hao walikuwa wamealikwa na watoto wenzao kutazama video ya vibonzo Sikiliza, Tii, Upate Baraka katika lugha yao ya Kixhosa. Pindi moja kulikuwa na watoto 11 na wote walikuwa wamekariri maneno ya wimbo huo.

Nchini Ekuado wavulana wawili wasio Mashahidi wanaozungumza lugha ya Quichua, Isaac mwenye umri wa miaka nane na mdogo wake Saul mwenye umri wa miaka mitano, walikuwa wakihifadhi pesa zao za kununulia biskuti na vitu vingine ili wanunue vitu vya kuchezea kama vile bunduki na mapanga. Siku moja mama yao aliwaambia wasafishe chumba chao na waweke vitu vyao vya kuchezea kwenye sanduku lilokuwa chini ya kitanda. Baadaye, wavulana hao walipewa zawadi ya DVD mpya Uwe Rafiki ya Yehova, na wakaitazama pamoja. Juma moja baadaye, mama yao alipokuwa akisafisha nyumba, aliona kwamba sanduku hilo lilikuwa na kigari cha kuchezea pekee. Akawauliza wavulana hao, “Vitu vyenu vya kuchezea viko wapi?” Wakamjibu, “Yehova havipendi, kwa hiyo tuliamua kuvitupa.” Sasa watoto wengine wanapochezea vitu vinavyofundisha jeuri, Isaac anawaambia: “Msichezee vitu hivyo. Yehova havipendi!”

Croatia: Nyimbo za Ufalme hugusa mioyo ya watoto