Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

MATUKIO MUHIMU YA MWAKA ULIOPITA

Ripoti ya Mambo ya Kisheria

Ripoti ya Mambo ya Kisheria

ARMENIA Yaruhusu Utumishi wa Badala wa Kiraia Unaoheshimu Msimamo wa Kikristo wa Kutounga Mkono Upande Wowote

Armenia: Baadhi ya ndugu wanapangiwa na serikali kufanya utumishi wa badala wa kiraia katika maeneo ya vijijini. Wakiwa huko, wanaendelea kuhubiri kwa bidii

Katika mwaka wa 2013, serikali ya Armenia ilianzisha mpango mpya wa utumishi wa badala wa kiraia, ambao unawaruhusu Mashahidi wa Yehova nchini humo kuchagua utumishi wa kiraia badala ya kutumikia vifungo vya gereza kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Mnamo Januari 2014, ofisi ya tawi iliripoti kwamba ndugu 71 walianza utumishi huo chini ya mpango huo mpya. Kwa mfano, baadhi ya ndugu walipangiwa kufanya kazi ya upishi au kuwasaidia wauguzi hospitalini. Wasimamizi wa mpango huo wamewasifu ndugu hao kwa kufanya kazi vizuri na kuonyesha mtazamo unaofaa wanapopewa kazi ambazo mara nyingi huwa ngumu. Akina ndugu wanashukuru kwamba mpango huo umeanzishwa kwa ajili yao ili wafanye utumishi wa kiraia ili waendelee kuwa na dhamiri safi ya Kikristo. * Ndugu mmoja alisema hivi: “Tunamshukuru Yehova kwamba tunaweza kufanya utumishi wa kiraia bila kuunga mkono upande wowote na wakati huohuo tukiwa na uhuru wa kumwabudu.”

JAMHURI YA DOMINIKA Yatambua Ndoa ya Kwanza ya Kikristo Isiyo ya Kikatoliki Iliyofanywa na Mashahidi

Mwaka wa 1954, Jamhuri ya Dominika ilifanya mkataba na Vatikani, kwamba Kanisa Katoliki pekee ndilo lenye haki ya kufungisha ndoa. Ikiwa ndoa haikufungishwa na Kanisa Katoliki, ofisa wa serikali angefungisha ndoa hiyo. Hata hivyo, mwaka wa 2010, serikali ilipitisha katiba mpya ambayo inawaruhusu wawakilishi wanaostahili wa dini nyingine kufungisha ndoa. Serikali ilifanya mpango wa kuwazoeza wale wanaotaka kupata kibali cha kufungisha ndoa. Ofisi ya tawi ya Jamhuri ya Dominika ilipendekeza wazee 30 kuhudhuria mazoezi hayo, na kati ya watu zaidi ya 2,000 waliotuma maombi, ni 32 tu waliokubaliwa. Hata hivyo, ndugu zetu wote 30 walipata kibali cha kufungisha ndoa za Mashahidi.

INDIA Wameazimia Kuhubiri Bila Woga

Sundeep na Deepalakshmi Muniswamy

Januari 27, 2014, Tume ya Haki za Kibinadamu ya Jimbo la Karnataka iliamua kwamba Naibu wa Inspekta wa Polisi (PSI) wa Kituo cha Polisi cha mji wa Old Hubli katika Jimbo la Karnataka, alikiuka haki za kibinadamu za Ndugu Sundeep Muniswamy kwa kuwa hakumlinda aliposhambuliwa na wafanya-ghasia Juni 28, 2011. Tume hiyo iliamua kwamba PSI ana hatia ya kukiuka haki za binadamu, hivyo ikaiamuru serikali ya Jimbo la Karnataka kumchukulia hatua PSI huyo na pia ikaamuru Ndugu Muniswamy alipwe rupia 20,000 (dola 326 za Marekani). Tume hiyo iliamuru serikali ikate mshahara wa PSI na kulipa faini hiyo.

Ndugu Muniswamy alisema kwamba yeye na familia yake wanamshukuru Yehova kwa uamuzi huo wa kipekee, na wameazimia kuendelea kuhubiri habari njema bila woga. Uamuzi huo umeimarisha imani na tumaini la ndugu hao katika uwezo wa Yehova wa kuwalinda watu wake. Pia, ni onyo kali kwa wenye mamlaka kwamba wanapaswa kulinda haki za kibinadamu za Mashahidi wa Yehova katika Jimbo la Karnataka. Kesi ya uhalifu dhidi ya Ndugu Muniswamy na ndugu mwingine zinazohusiana na tukio hilo bado ziko mahakamani.

KYRGYZSTAN Baraza la Kikatiba la Mahakama Kuu Latetea Haki ya Kutojiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Novemba 19, 2013, ilikuwa siku muhimu sana kwa wale wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Baraza la Kikatiba la Mahakama Kuu lilitupilia mbali uamuzi wa kesi za Mashahidi wa Yehova 11, na likasema kwamba mpango wa utumishi wa badala wa Kyrgyzstan unapingana na katiba. Sheria iliwataka wote wanaofanya utumishi wa badala kulipa pesa moja kwa moja ili kutegemeza shughuli za kijeshi. Pia, sheria iliwataka wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri wawe wanajeshi wa akiba wanapomaliza kipindi cha utumishi wa badala. Baraza hilo la Kikatiba liliamua kwamba kuwalazimisha watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kufanya utumishi wa badala katika hali kama hizo, ni ukiukaji wa haki ya uhuru wa kuabudu. Kwa hiyo, mwanzoni mwa mwaka wa 2014, Mahakama Kuu ya Kyrgyzstan ilitekeleza uamuzi wa Baraza la Kikatiba na kuwaondolea mashtaka Mashahidi wa Yehova 14 ambao walishtakiwa kama wahalifu chini ya sheria ya zamani. Uamuzi huo umemaliza kesi iliyoendeshwa kwa miaka saba ya kupigania uhuru wa kidini wa wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Azimio la vijana hao wapenda-amani unatetea jina la Yehova na uhuru wetu wa kuabudu katika Jamhuri ya Kyrgyz.

Kyrgyzstan: Mashahidi ambao kesi zao zilipelekwa kwenye mahakama kuu ya Kyrgyzstan

NIGERIA “Yehova Alinithawabisha”

Katika Jimbo la Abia, nchini Nigeria, mara nyingi Mashahidi wa Yehova wanatishwa na kuchukiwa kwa sababu wanakataa kujiunga na vikundi vya kijamii * ambavyo shughuli zake zinatia ndani kupigana na kufanya matambiko ya kishirikina. Asubuhi moja mwezi Novemba 2005, washiriki wa kikundi kama hicho katika kijiji cha Asaga Ohafia walivamia nyumba ya Ndugu Emmanuel Ogwo na mke wake, halafu wakachukua kwa nguvu mali zao zote kama malipo ya wanachama wa kikundi hicho. Wenzi hao walibaki tu na nguo walizokuwa wamevaa. Mwaka wa 2006, wanakijiji walimfukuza Ndugu Ogwo kutoka nyumbani kwake na kijijini. Ndugu na dada Ogwo walipata hifadhi kwa ndugu katika kijiji kingine ambako walipata mahitaji yao. Ingawa Ndugu Ogwo alirudi nyumbani kwake mwaka uliofuata, aliendelea kupambana na shinikizo la kujiunga na kikundi hicho, na maombi yake ya kurudishiwa mali zake yalipuuzwa.

Hatimaye, Aprili 15, 2014, Mahakama Kuu ya Jimbo la Abia ilimpa ushindi Ndugu Ogwo, ikitetea haki yake ya kikatiba ya uhuru wa kidini na wa kushirikiana. Mali za Ndugu Ogwo zilizoporwa zilirudishwa, Mashahidi hawachukiwi sana na jamii kama ilivyokuwa awali, na sasa ndugu katika kijiji cha Asaga Ohafia wanahubiri kwa uhuru.

Uamuzi huo wa mahakama ulipotangazwa, Ndugu  Ogwo alisema hivi: “Niliruka kwa shangwe. Nilifurahi sana. Nilihisi kwamba Yehova ameshinda kesi, na malaika walikuwa pamoja nami. Yehova alinithawabisha.”

URUSI Uamuzi Uliotetea Tovuti ya jw.org

Changamoto nyingi za kisheria ambazo ndugu zetu wanakabiliana nazo nchini Urusi ‘zimegeuka na kuwa zenye kuendeleza mbele habari njema’ nchini humo. (Flp. 1:12) Ingawa baadhi ya maofisa wa serikali na viongozi wa kidini wanapinga sana ibada yetu, ndugu zetu nchini Urusi wanadumisha utimilifu wao, na Yehova anabariki jitihada zao.

Mojawapo ya mambo yanayoonyesha kwamba Yehova anawabariki ni ushindi katika kesi dhidi yao jijini Tver’. Mwaka wa 2013, mwendesha mashtaka wa jiji la Tver’ alifungua kesi mahakamani kupiga marufuku Tovuti ya jw.org nchini Urusi. Bila kumjulisha mwakilishi yeyote wa Mashahidi wa Yehova, mahakama hiyo ilimpa ushindi mwendesha mashtaka huyo. Ndugu zetu waliposikia kuhusu uamuzi huo wa mahakama, walikata rufaa. Januari 22, 2014, Mahakama ya Eneo la Tver’ ilibadili uamuzi wa mahakama ndogo na kuwapa ushindi Mashahidi. Tunamshukuru Yehova na sala za ndugu na dada ulimwenguni pote, sasa ndugu zetu wengi nchini Urusi wananufaika kiroho kupitia Tovuti ya jw.org.

UTURUKI Inaendelea Kupuuza Haki ya Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri

Bariş Görmez, Shahidi wa Yehova nchini Uturuki alifungwa gerezani kwa zaidi ya miaka minne kwa sababu alikataa kutumika jeshini. Akiwa kwenye kambi, aliteswa sana na wanajeshi waliompiga mateke na marungu. Aliteseka pia alipokuwa gerezani. Kwa kuwa Ndugu Görmez ana urefu wa futi saba, alishindwa kulala kwenye kitanda alichopewa na ilibidi alale akiwa amekingama na kujipinda kwenye vitanda viwili. Baadaye, wasimamizi wa gereza walimruhusu kutumia godoro kubwa alilopewa na kutaniko la kwao.

Mwaka wa 2008, Ndugu Görmez na Mashahidi wengine watatu walipeleka malalamiko yao kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, kwamba Uturuki ilikiuka uhuru wao wa kidini kwa kutotambua haki yao ya kutojiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Juni 3, 2014, Mahakama hiyo iliwapa ushindi Mashahidi * hao wanne na ikaamuru serikali ya Uturuki iwalipe gharama za usumbufu na za kesi hiyo. Hii ni mara ya tatu Mahakama ya Ulaya kuwapa ushindi Mashahidi wa Yehova dhidi ya serikali ya Uturuki kuhusiana na swala hilo. Ingawa kwa sasa hakuna Shahidi wa Yehova aliye gerezani, suluhisho la kudumu litapatikana serikali ya Uturuki itakapotambua haki ya kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Ripoti za Awali

Azerbaijan: Ndugu wanaendelea kuvamiwa mikutanoni, machapisho yao yanazuiwa kuingia nchini, wanakamatwa wanapohubiri, na kunyimwa haki nyingine za kibinadamu. Wakati huohuo, serikali inaendelea kukataa kusajili tena Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova. Malalamiko 19 yamepelekwa kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu dhidi ya Azerbaijan kuhusiana na masuala hayo. Licha ya hali hizo ngumu, ongezeko la wahubiri ni uthibitisho ulio wazi kwamba Yehova anaendelea kuwabariki. Kutolewa kwa Biblia TakatifuTafsiri ya Ulimwengu Mpya katika Kiazerbaijani ni sababu nyingine iliyowafanya washangilie zaidi.

Eritrea: Katika nchi hiyo, ndugu zetu wanaendelea kumtumikia Yehova kwa uaminifu wakivumilia mateso makali. Ndugu watatu, Paulos Eyassu, Isaac Mogos, na Negede Teklemariam, sasa wako gerezani kwa miaka 20—tangu Septemba 24, 1994. Wenye mamlaka nchini Eritrea waliwakamata Mashahidi na wapendezwa 150 hivi wakati wa Ukumbusho wa Kifo cha Kristo Aprili 14, 2014. Waliokamatwa walikuwa na umri wa kati ya miezi 16 na miaka zaidi ya 85. Pia, Mashahidi na wapendezwa wengine 30 hivi walikamatwa wakati wa hotuba ya pekee Aprili 27, 2014. Wengi wao wameachiliwa.

Kazakhstan: Kitengo cha Masuala ya Dini kimekataa kuingizwa au kugawanywa kwa aina 14 kati ya machapisho yetu katika Jamhuri ya Kazakhstan. Pia, ndugu zetu hawana uhuru wa kuongea na wengine kuhusu imani yao nje ya majengo yao ya ibada yaliyosajiliwa, na ndugu zetu 50 hivi wameshtakiwa kwa kusingiziwa kufanya kazi ya umishonari iliyopigwa marufuku. Ili kutetea uhuru wao wa kusema, kesi 26 zimepelekwa kwenye Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

^ fu. 1 Kufanya au kutofanya utumishi wa kiraia wa badala ni jambo linalohusu dhamiri ya mtu.

^ fu. 1 Kikundi cha kijamii hufanyizwa na watu, hasa wanaume wa rika moja wanaoishi kijiji kimoja.

^ fu. 2 Buldu and Others v. Turkey, Na. 14017/08, Juni 3, 2014.