Hamia kwenye habari

Kulinda Wanyama Pori na Mazingira Katika Eneo la Warwick

Kulinda Wanyama Pori na Mazingira Katika Eneo la Warwick

Mashahidi wa Yehova wameanza kujenga makao yao makuu mapya ya ulimwenguni pote karibu na Ziwa Sterling Forest (Ziwa Blue) katika eneo la mashambani la Jimbo la New York. Wameweka mikakati gani ya kuwalinda wanyama-pori na mazingira ya eneo hilo?

Mashahidi waliweka wigo wa muda mfupi kuzunguka eneo la ujenzi ili kuwazuia nyoka ambao hupenda kuishi kwenye mbao pamoja na kobe wa aina mbalimbali wanaopatikana katika eneo hilo ili wasiingie kwenye eneo la ujenzi ambako wanaweza kuumizwa. Wigo huo hukaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa wanyama hawawezi kupenya na kuingia ndani ambako shughuli za ujenzi zinaendelea. Ujenzi utakapokamilika na wigo kuondolewa, nyoka wowote watakaopatikana karibu sana na majengo hayo watahamishwa na kupelekwa eneo jingine na mtu aliyezoezwa kufanya kazi hiyo kwa njia ya usalama.

Eastern bluebird

Miti ilikatwa katika kipindi cha baridi kali ili kuepuka kuwasumbua ndege aina ya eastern bluebird katika msimu wao wa kutengeneza viota. Baada ya ujenzi kukamilika katika maeneo ambayo miti ilikatwa, Mashahidi wataweka masanduku madogo yatakayokuwa viota vya ndege ili kuwatia moyo ndege hao kurudi eneo hilo.

Vivyo hivyo, wanasafisha na kusawazisha ardhi katika maeneo fulani kati ya mwezi wa Oktoba hadi Machi ili mbegu za aina fulani ya mhisopo ulio katika hatari ya kutoweka ziweze kutawanyika na kukua vizuri. Ratiba hii inafuatwa hata ingawa aina hiyo ya mimea haipatikani katika eneo la ujenzi la Warwick tangu mwaka wa 2007.

Ziwa Sterling Forest, linalopakana na uwanja huo, lina aina nyingi za ndege wa majini pamoja na samaki mbalimbali kama vile trauti, bass, pickerel, na sangara. Ili kulinda ziwa hilo, wataalamu walichagua mbinu za ujenzi zitakazohifadhi mazingira. Mbinu hizo zinahusisha kupanda mimea katika paa za majengo, mimea ambayo itasaidia maji mengi ya mvua yasipotee na ambayo itachuja uchafu kutoka katika maji hayo. Pia, mimea iliyo kando ya ziwa hilo inatunzwa na kulindwa.

Shahidi fulani anayehusika moja kwa moja katika shughuli mbalimbali za ujenzi huo anasema, “Hata ingawa kufanya mambo yote hayo kutatulazimu tufanye mambo mengi ya ziada na tutumie muda mwingi zaidi, tumejitoa kabisa kulinda mazingira katika eneo hilo la ujenzi la Warwick.”