Hamia kwenye habari

JANUARI 21, 2015
POLAND

Waokokaji wa Kambi ya Auschwitz Waadhimisha Miaka 70 Tangu Kuachiliwa Huru, Mashahidi wa Yehova Wakiwa Miongoni Mwao

Waokokaji wa Kambi ya Auschwitz Waadhimisha Miaka 70 Tangu Kuachiliwa Huru, Mashahidi wa Yehova Wakiwa Miongoni Mwao

WARSAW, Poland—Januari 27, 2015, maelfu wataadhimisha miaka 70 tangu kuwekwa huru kwa wafungwa wa kambi ya Auschwitziliyokuwa kambi ya mateso na ya kifo ya Wanazi wa Ujerumani. Kambi hiyo iliyojulikana sana ilitumiwa hasa kuua watu wa jamii zilizochukiwa na Wanazi, na pia ilitumiwa kuwanyanyasa Mashahidi wa Yehova kutoka mataifa mbalimbali, kutia ndani Ujerumani.

Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Auschwitz-Birkenau na Baraza la Kimataifa la Auschwitz wanaandaa tukio hilo. Rais wa Poland, Bronisław Komorowski na wajumbe rasmi wa serikali kutoka nchi nyingi wanatarajiwa kuwepo. Maadhimisho hayo pia yataunganishwa moja kwa moja kupitia Intaneti.

Kambi ya Auschwitz iko katika eneo lililo mbali kidogo na jiji la Oświęcim, jiji ambalo lilitawaliwa na Wanazi wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Mwanzoni ilikuwa kambi ya mateso ya Wajerumani yenye wafungwa 700 hivi kutoka Poland, waliowasili hapo mnamo Juni 1940. Baada ya muda mfupi, Auschwitz ikawa na kambi zaidi ya 40 pamoja na kambi zingine ndogondogo. Karibu watu 20,000 waliuawa kila siku kwa gesi, katika vyumba vinne vilivyoko huko Auschwitz-Birkenau. Watu milioni 1.1 hivi, kutia ndani zaidi ya Mashahidi wa Yehova 400, walipelekwa kwenye kambi ya Auschwitz katika kipindi cha miaka mitano ambayo kambi hiyo ilikuwa ikitumiwa.

Tovuti ya Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Auschwitz-Birkenau inaeleza hivi: “Mbali na kutaja mambo machache tu, habari zilizoandikwa kuhusu historia ya kambi ya mateso ya Auschwitz hazizungumzi kuhusu Mashahidi wa Yehova, (walijulikana kama [Wanafunzi] wa Biblia katika rekodi za kambi hiyo) ambao walifungwa kwa sababu ya imani yao ya kidini. Wafungwa hao wanastahili kusifiwa kwa sababu ya kushikilia imani yao chini ya hali zilizokuwa katika hiyo.” Rekodi za jumba hilo la makumbusho zinaonyesha kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa miongoni mwa wafungwa wa kwanza kupelekwa Auschwitz, na kati ya mamia ya Mashahidi hao, zaidi ya asilimia 35 walikufia huko.

Andrzej Szalbot (Mfungwa–IBV 108703): Mwaka wa 1943, alikamatwa na Wanazi na kupelekwa katika kambi ya Auschwitz kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri..

Serikali ya Wanazi ilianza kushambulia utendaji wa Mashahidi wa Yehova kuanzia mwaka wa 1933 na kupiga marufuku tengenezo hilo kotekote Ujerumani. Mwenendo na mafundisho ya Mashahidi haukupatana na mafundisho ya Wanazi. Kwa mfano, Mashahidi walikataa kusema “Heil Hitler!,” kwa kuwa waliona kumtukuza Hitler katika njia hiyo kungekuwa kukosa ushikamanifu kwa Mungu wao. Pia, Mashahidi walikataa kufanya kazi zozote za kijeshi, msimamo ambao Wanazi waliona kuwa kukosa ushikamanifu kwa nchi yao. Andrzej Szalbot, aliyekamatwa mwaka 1943 na kupelekwa Auschwitz akiwa na umri wa miaka 19 tu, anaeleza hivi: “Kukataa kufanya utumishi wa kijeshi kulifanya mtu apelekwe kwenye kambi ya mateso.” Mashahidi wa Yehova waliahidiwa kuachiliwa huru mara moja ikiwa wangetia sahihi hati ya kukataa kuwa mshiriki wa tengenezo hilo na kukubali kuwa mafundisho yake si sahihi. Bw. Szalbot alikataa kutia sahihi hati hiyo.

Mashahidi wa Yehova waliahidiwa kuachiliwa huru ikiwa wangekana imani yao kwa kutia sahihi katika hati kama hii.

Hati rasmi za Wanazi, ziliwarejelea Mashahidi wa Yehova kwa herufi “IBV,” ambazo ni ufupisho wa Internationale Bibelforscher-Vereinigung (International Bible Students Association), jina rasmi la tengenezo lao nchini Ujerumani. Wanazi waliamuru Mashahidi wavae alama ya pembetatu ya zambarau kwenye sare zao. Alama hiyo iliwasaidia Mashahidi kutambua Mashahidi wenzao wakiwa kambini. Walikutana kila jioni kabla ya kuhesabiwa ili kutiana moyo. Mikutano ya siri ilipangwa pia ili kuzungumzia Biblia na wafungwa wengine ambao walivutiwa na fadhili na imani ya Mashahidi. Wafungwa kadhaa walikuwa Mashahidi wa Yehova wakiwa kwenye kambi za Auschwitz.

Jumamosi asubuhi, Januari 27, 1945, Jeshi la Muungano wa Sovieti linaloitwa Red Army liliwasili Oświęcim. Kufikia saa 9 mchana, majeshi ya Sovieti yalikuwa yamewaweka huru wafungwa 7,000 kutoka kambi za Auschwitz I, Auschwitz II (Birkenau), na Auschwitz III (Monowitz).

Stanisław Zając. Aliwasili Auschwitz Februari 16, 1943.

Stanisław Zając, Shahidi wa Yehova, alikuwa miongoni mwa makumi ya maelfu waliolazimishwa na Wanazi kuondoka katika kambi za Auschwitz kabla ya jeshi la Red Army kufika. Zając na wafungwa wengine 3,200 hivi waliondoka katika kambi ndogo ya Jaworzno na kuanza safari katika theluji nyingi, safari iliyokuja kujulikana kama safari ya kifo. Inakadiriwa kwamba waliofanikiwa kumaliza safari hiyo ya siku tatu kwenda kwenye kambi ndogo iliyokuwa msituni, ya Blechhammer, hawakufika watu 2,000. Katika maandishi yake ya kumbukumbu, Bw. Zając alieleza kuhusu vita vilivyoendelea wakati yeye na wafungwa wengine walipokuwa wamejificha kambini. Aliandika hivi: “Tulisikia sauti za magari ya vita yakipita, lakini hakuna aliyekuwa na ujasiri wa kuangalia magari hayo yalikuwa ya jeshi lipi. Asubuhi ilipofika, tuligundua kwamba yalikuwa ya Warusi. . . . Jeshi la Urusi lilikuja katika eneo hilo na huo ukawa mwisho wa mateso yangu kambini.”

Mwaka huu, siku ya Januari 27, mikutano na maonyesho yanayohusu maadhimisho ya miaka 70 tangu kuachiliwa huru kwa wafungwa kutoka Auschwitz yatafanywa katika majiji tofauti-tofauti ulimwenguni pote.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Ujerumani: Wolfram Slupina, simu +49 6483 41 3110

Poland: Ryszard Jabłoński, simu +48 608 555 097