Hamia kwenye habari

Jengo la Mahakama Kuu ya Uzbekistan kule Tashkent.

NOVEMBA 8, 2018
UZBEKISTAN

Mahakama Kuu ya Uzbekistan Yatetea Haki ya Mashahidi wa Yehova Kumiliki Machapisho ya Biblia

Mahakama Kuu ya Uzbekistan Yatetea Haki ya Mashahidi wa Yehova Kumiliki Machapisho ya Biblia

Katika kipindi cha miezi sita kuanzia Machi 2018, Mahakama Kuu ya Uzbekistan na Mahakama ya Usimamizi ya Karakalpakstan, jamhuri inayojitegemea nchini Uzbekistan, zilitoa maamuzi yanayowafaa Mashahidi wa Yehova katika kesi zinazohusiana na uhuru wetu wa ibada. Mahakama Kuu ilibadili maamuzi manne ya mahakama za chini yaliyotolewa dhidi ya ndugu zetu, na Mahakama ya Usimamizi ikabadili uamuzi wa tano.

Kesi kadhaa zinazowahusu ndugu zetu zilitokana na upelelezi wa polisi ambao walikamata vitabu vinavyotegemea Biblia, kutia ndani vifaa vya kielektroni vilivyokuwa na nakala za Biblia. Kwa sababu hiyo, mahakama za chini ziliwahukumu akina ndugu kuwa na hatia na kuwapiga faini kwa msingi wa sheria ambayo inaweza kutafsiriwa kuwa inazuia mtu yeyote asisambaze habari za kidini. Kwa kupendeza, maamuzi hayo ya karibuni ya mahakama kuu yanawaondolea kabisa hatia ndugu zetu kutokana na hukumu zilizotolewa na kuonyesha kwamba hawahitaji kulipa faini.

Timur Satdanov, mmoja wa akina ndugu walioondolewa mashtaka na Mahakama Kuu ya Uzbekistan.

Shahidi mmoja ambaye mwanzoni alihukumiwa kuwa na hatia katika mahakama za chini, Timur Satdanov, alimwandikia barua rais wa Jamhuri, akimshukuru kwa uamuzi unaofaa wa Mahakama Kuu. Ndugu Satdanov alitoa shukrani na kueleza kwamba yeye na Mashahidi wenzake wataendelea kusali kwa ajili ya wale “wenye vyeo vya juu,” ili waweze kuendelea “kuishi kwa amani na utulivu na ujitoaji-kimungu kamili na kuchukua mambo kwa uzito.” (1 Timotheo 2:2) Kaimu wa mwenyekiti wa Baraza la Mahakimu wa Mahakama ya Usimamizi kwenye Mahakama Kuu alijibu barua hiyo na kusema kwamba ilipokelewa na kuzungumziwa na mahakama hiyo.

Mashahidi ulimwenguni pote wanashangilia kwa sababu ya matukio hayo na wanawashuruku wenye mamlaka. Zaidi ya wote wanamshukuru Yehova kwa mwongozo na utegemezo wake “katika kuitetea na kuithibitisha kisheria habari [yake] njema.”—Wafilipi 1:7.