Hamia kwenye habari

OKTOBA 29, 2019
AZERBAIJAN

Uamuzi wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Waunga Mkono Msimamo wa Mashahidi Watano Nchini Azerbaijan Waliokataa Utumishi wa Kijeshi

Uamuzi wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Waunga Mkono Msimamo wa Mashahidi Watano Nchini Azerbaijan Waliokataa Utumishi wa Kijeshi

Oktoba 17, 2019, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi kwamba ndugu zetu nchini Azerbaijan wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri hawapaswi kuhukumiwa kama wahalifu. Uamuzi huo unakazia tena kwamba kuwaadhibu wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri ni kukiuka haki za uhuru wa dhamiri, fikira, na kidini. Hii ni mara ya kwanza kwa ECHR kutoa uamuzi unaounga mkono Mashahidi wa Yehova nchini Azerbaijan.

Uamuzi huo ulihusisha kuunganishwa kwa kesi nne zilizopelekwa katika mahakama hiyo kati ya mwaka wa 2008 na 2015. Kesi hizo zilihusisha akina ndugu wanne: Mushfig Mammadov, Samir Huseynov, Farid Mammadov, Fakhraddin Mirzayev, na Kamran Mirzayev. Kila mmoja wao alihukumiwa na kufungwa gerezani nchini Azerbaijan kwa kukataa utumishi wa kijeshi. Mahakama hiyo iligundua kwamba uamuzi wa ndugu hao wa kukataa utumishi wa kijeshi ulitegemea “itikadi za kweli za kidini,” na hivyo nchi ya Azerbaijan iliwatendea ndugu hao kinyume na Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu. Isitoshe, Mahakama hiyo ilisema kwamba utumishi wa badala haupaswi kuandaliwa kwa ajili tu ya makasisi na wanafunzi wa taasisi za kidini. Vilevile Mahakama hiyo ilisema kwamba nchi ya Azerbaijan inapaswa kuwalipa akina ndugu hao hasara waliyopata kutokana na uamuzi huo.

Kama ilivyofafanuliwa katika uamuzi wa mahakama hiyo, Azerbaijan ilikubali rasmi kuweka sheria za utumishi wa badala wa kiraia nchi hiyo ilipojiunga na Baraza la Ulaya mwaka wa 2001. Isitoshe, katiba ya Azerbaijan ina utumishi wa badala wa kiraia kwa ajili ya watu ambao itikadi zao zinapingana na utumishi wa lazima wa kijeshi. Hata hivyo, bado wenye mamlaka hawajaanza kutekeleza mpango wa utumishi wa badala, na hivyo bado ndugu zetu wanahukumiwa kuwa wahalifu kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.

Tunatumaini kwamba uamuzi wa Mahakama hiyo utawachochea wenye mamlaka nchini Azerbaijan wafanye mipango ya kutekeleza utumishi wa badala wa kiraia. Kwa sasa, tunasali kwamba ndugu zetu nchini Azerbaijan waendelee kumtumikia Yehova kwa ujasiri.—Zaburi 27:14.