Hamia kwenye habari

Kuanzia kushoto hadi kulia: Eldor na ndugu yake Sanjarbek Saburov

AGOSTI 7, 2020
TURKMENISTAN

Mahakama ya Turkmenistan Yawahukumu Ndugu Eldor na Sanjarbek Saburov Miaka Miwili Gerezani

Mahakama ya Turkmenistan Yawahukumu Ndugu Eldor na Sanjarbek Saburov Miaka Miwili Gerezani

Agosti 6, 2020, mahakama ya Turkmenistan iliwahukumu Ndugu Eldor Saburov na Sanjarbek Saburov miaka miwili gerezani kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Eldor ana umri wa miaka 21 na Sanjarbek ana umri wa miaka 25. Mahakama hiyo ilikataa ombi lao la kukata rufaa uamuzi huo. Hii ni mara ya pili kwao kufungwa kwa sababu ya msimamo wao wa kutounga mkono upande wowote.

Mwaka 2016, Ndugu Sanjarbek Saburov alikataa kujiunga na jeshi. Kwa sababu hiyo, alihukumiwa kifungo cha masharti cha miaka miwili.

Mwaka uliofuata, ndugu ya Sanjarbek, anayeitwa Eldor, alikataa pia kujiunga na jeshi. Alipewa adhabu ya kutumikia utumishi wa kubadili tabia kwa miaka miwili na kuilipa serikali asilimia 20 ya mshahara wake.

Kulingana na sheria ya Turkmenistan, watu wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri wanaweza kushtakiwa kwa mara ya pili kuwa wahalifu ikiwa wataendelea kukataa kujiunga na jeshi. Aprili 2020, ofisi ya kuajiri wanajeshi iliwaita tena ndugu hao ili wajiunge na jeshi. Ndugu hao walikataa. Walihukumiwa kuwa wahalifu na kufungwa gerezani.

Mbali na athari za kihisia, kufungwa kwa ndugu hao kutasababisha wazazi wao kuwa na hali ngumu ya kiuchumi. Baba yao ana matatizo ya mgongo yanayomzuia kufanya kazi. Watoto wake hutegemeza familia kwa kulima pamba. Kwa kuwa sasa wamefungwa gerezani, wazazi wao hawatakuwa na utegemezo wa kifedha. Badala yake, wazazi hao watahitaji kuwategemeza watoto wao waliofungwa gerezani.

Hakuna utumishi wa badala wa kiraia nchini Turkmenistan. Hivyo, ndugu vijana wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao wanakabili kifungo cha mwaka mmoja hadi minne gerezani. Mbali na Ndugu Eldor na Sanjarbek Saburov, kuna vijana wengine kumi Mashahidi waliofungwa gerezani nchini Turkmenistan kwa sababu ya kutounga mkono upande wowote.

Tunajua kwamba Yehova atawabariki ndugu zetu vijana nchini Turkmenistan kwa sababu ya ujasiri wao. Na kila mmoja wao akumbuke ahadi hii ya Yehova kwa Mfalme Asa: “Ninyi, iweni imara na msivunjike moyo, kwa maana mtapata thawabu kwa ajili ya kazi yenu.”—2 Mambo ya Nyakati 15:7.