Hamia kwenye habari

Mahakama Kuu ya Monaco

NOVEMBA 23, 2022
MONACO

Mashahidi wa Yehova Wasajiliwa Kisheria Monaco

Mashahidi wa Yehova Wasajiliwa Kisheria Monaco

Novemba 19, 2022, Mashahidi wa Yehova walisajiliwa kisheria Monaco. Usajili huo unatokea baada ya uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Monaco na pia uamuzi mwingine uliotolewa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR). Maamuzi yote mawili yaliwaunga mkono Mashahidi wa Yehova.

Miaka miwili hivi baada ya ndugu zetu kupeleka kesi yao kwenye ECHR, mahakama hiyo iliwasilisha uamuzi wake kwa serikali ya Monaco na kuiomba itafute suluhisho.

Kwa kawaida, baada ya uamuzi wa kesi kuwasilishwa kwa serikali, jambo la kwanza ambalo wahusika hufanya ni kujaribu kutatua tatizo lao kwa njia ya kirafiki. Katika kisa hiki, serikali ya Monaco iliunga mkono hatua hiyo kwa kukubali kuwasajili Mashahidi wa Yehova. Desemba 9, 2021, ECHR ilitoa uamuzi uliokubali utatuzi uliofikiwa kwa njia ya kirafiki ambapo serikali ya Monaco ilikubali kusajili kisheria tengenezo letu bila kuweka vizuizi vyovyote ambavyo vingeathiri ibada yetu. Serikali hiyo pia ilikubali kulipa zaidi ya euro 35,000 (dola 40,000 za Marekani) ambazo ni gharama za kesi.

Novemba 16, 2022, serikali ya Monaco ilitoa hati iliyothibitisha kusajiliwa kwa Association Monégasque pour le Culte des Témoins de Jéhovah (Monaco Association for the Worship of Jehovah’s Witnesses). Novemba 18, 2022, hati hiyo ilichapishwa katika gazeti rasmi la serikali ya Monaco.

Tunashangilia kwa sababu ndugu na dada zetu walio Monaco wanaweza kufanya ibada bila vizuizi vya serikali. Tunamshukuru Yehova kwa usajili huu ambao tumesubiri kwa muda mrefu. —Wafilipi 1:7.