Hamia kwenye habari

NOVEMBA 5, 2013
ARMENIA

Armenia Yaruhusu Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Wafanye Utumishi wa Badala wa Kiraia

Armenia Yaruhusu Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Wafanye Utumishi wa Badala wa Kiraia

Hatimaye serikali ya Armenia imetambua haki za wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao. Mnamo Oktoba 23, 2013, Tume ya Jamhuri ya Armenia ilikubali maombi ya kufanya utumishi wa badala wa kiraia kutoka kwa Mashahidi wa Yehova 51 kati ya Mashahidi zaidi ya 90 walioomba wasajiliwe kwenye mpango huo (Tume hiyo itafikiria pia maombi yaliyosalia). Kisha, Tume hiyo ilienda kwenye Gereza la Erebuni na ikakubali kuwaingiza kwenye mpango huo Mashahidi 6 kati ya 20 waliofungwa kwenye gereza hilo. Mashahidi hao sita waliachiliwa huru mnamo Oktoba 24, 2013. Tume hiyo itafikiria maombi ya Mashahidi waliobaki ya kusajiliwa kwenye mpango huo na inatarajiwa kwamba itakubali waachiliwe huru.

Mpango Mpya

Mabadiliko hayo yalianza Juni 8, 2013, wakati serikali ya Armenia iliporekebisha Sheria inayohusu Utumishi wa Badala ili ipatane na viwango vya Ulaya, na ikaanza kuitumia Julai 25, 2013. Mnamo Oktoba 2, 2013, rais wa Armenia alisema hivi kwenye Mkutano wa Baraza la Bunge la Ulaya alipokuwa akizungumzia kuhusu sheria hiyo iliyorekebishwa: “Kulingana na sera yetu, watu wasiotaka kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao, hawatahesabiwa kuwa wahalifu.” Mnamo Oktoba 3, 2013, serikali ya Armenia ilianzisha sheria inayowasamehe wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kwa kuwapunguzia kipindi cha kufungwa gerezani kwa miezi sita. Kutokana na msamaha huo, Mashahidi 8 waliokuwa wamebakiza miezi sita ya vifungo vyao waliachiliwa huru mnamo Oktoba 8 na 9, 2013.

Mpango mpya wa utumishi wa badala wa kiraia unawawezesha wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao kutumikia nchi yao kwa njia inayopatana na dhamiri zao zilizozoezwa na Biblia. Kwa sasa Jeshi la Armenia halishughulikii jambo hilo na badala yake mashirika ya kiraia ndiyo yanayosimamia mpango huo. Kulingana na mpango huo, mtu atafanya utumishi wa kiraia kwa miaka 3, akitumikia kwa saa 48 kila juma. Pia atakuwa na siku 10 za likizo kwa mwaka. Wale watakaojiandikisha kwenye mpango huo watapewa kazi karibu na mahali wanapoishi na kazi zao hazitahusisha mambo ya kijeshi.

Mambo Yaliyochangia Marekebisho Hayo Yafanywe

Armenia ilipojiunga na Baraza la Ulaya mwaka wa 2001, ilikubali kwamba itafuata sharti la kila Nchi mpya inayojiunga na baraza hilo kuanzisha sheria ya utumishi wa badala na kuwaachilia huru wote waliofungwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao. Ijapokuwa ilikubali jambo hilo, Armenia iliendelea kuwafungulia mashtaka na kuwafunga gerezani wanaume vijana Mashahidi.

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, zaidi ya Mashahidi wa Yehova 450 wametumikia vifungo virefu gerezani, mara nyingi wakivumilia hali ngumu na kutendewa vibaya.

Wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao walianza kuwa na matumaini baada ya serikali ya Armenia kuanzisha Sheria ya Utumishi wa Badala wa Kiraia mnamo Julai 1, 2004. Hata hivyo, sheria hiyo ilipoanza kutumiwa, mpango wa utumishi wa badala ulidhibitiwa na kusimamiwa na jeshi na ulitumiwa kama adhabu. Baraza la Ulaya lilisema mara nyingi kwamba mpango huo haukupatana na viwango vya Ulaya. Kwa mfano, kwenye Azimio la 1532 (mwaka wa 2007), Mkutano wa Baraza la Bunge la Ulaya ulieleza hangaiko lake kwa njia hii: “Kwa sababu mpango huo hauendeshwi kama ulivyotarajiwa, wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao, wengi wao wakiwa ni Mashahidi wa Yehova, wanaendelea kufungwa kwa kuwa wanachagua kufungwa gerezani kuliko kufanya utumishi wa badala wa kiraia ambao unahusisha mambo ya kijeshi.”

Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa pia ilieleza hangaiko lake kuhusu Armenia kuendelea kuwafunga Mashahidi wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao. Kamati hiyo ilisema hivi kwenye mkutano wake wa 105 (mwaka wa 2012):

“Nchi hii ambayo ni mwanachama wa Baraza la Ulaya inapaswa kuwa na utumishi wa badala kwa wale wasiotaka kujiunga na jeshi, utumishi ambao hauhusishi kabisa mambo ya kijeshi, ambao unaweza kuwafaa wote wasiotaka kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao na usiohusisha adhabu kali, ubaguzi, gharama kubwa au wakati mwingi. Pia inapaswa kuwaachilia huru wote waliofungwa gerezani kwa kutojiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao au kwa kukataa kufanya utumishi wa badala wa kiraia uliopo sasa.”

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) Yaingilia Kati

Baada ya kushindwa kupata msaada kwenye mahakama za Armenia, Vahan Bayatyan na vijana wengine wawili Mashahidi ambao walikuwa wamehukumiwa walipeleka kesi yao dhidi ya Armenia kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR). Kesi ya Bwana Bayatyan ilileta mabadiliko makubwa wakati Baraza Kuu la mahakama ya ECHR lilipotoa uamuzi mkubwa uliomuunga mkono mnamo Julai 7, 2011. Kwa mara ya kwanza katika historia yake, mahakama ya ECHR iliamua kwamba Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu unapaswa kuwalinda wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao. Uamuzi huo wa Baraza Kuu ulifuatiwa na maamuzi mengine manne ya mahakama ya ECHR ambayo pia yalitetea haki za wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao. a

Waliopeleka kesi zao kwenye mahakama ya ECHR ambapo maamuzi yalitolewa yanayotetea haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri: Vahan Bayatyan, Hayk Bukharatyan, Ashot Tsaturyan.

Kwa kupuuza uamuzi wa Baraza Kuu katika kesi ya Bayatyan dhidi ya serikali ya Armenia, serikali ya Armenia iliwakamata na kuwashtaki Mashahidi vijana 29 waliokuwa wamekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao ambapo 23 kati yao walifungwa gerezani. Kuanzia Julai 2011 hadi Oktoba 2013, wanaume 86 wametumia zaidi ya miaka 168 kwenye magereza ya Armenia. Baadhi ya wanaume hao vijana walipinga uamuzi huo usio wa haki kwa kupeleka kesi zao kwenye mahakama ya ECHR.

Mambo Ambayo Hayajashughulikiwa

Wale waliomaliza vifungo vyao wanatumaini kwamba rekodi zao za uhalifu zitafutwa kufuatia marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria ya uhalifu ya Armenia. Jambo lingine linalohangaisha ni ikiwa wale walioshtakiwa na kufungwa watalipwa fidia baada ya uamuzi huo wa kesi ya Bayatyan.

Tunaendelea kusubiri kuona jinsi sheria hiyo iliyofanyiwa marekebisho ya utumishi wa badala wa kiraia itakavyofanya kazi nchini Armenia. Hata hivyo, inaonekana kwamba sasa serikali ya Armenia imefanya jitihada kubwa kutambua haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Safari Ndefu ya Kupata Mpango wa Utumishi wa Kiraia Unaofaa

Wakati

Maendeleo

2001

Armenia yawa mshiriki wa Bunge la Ulaya na yatakiwa kuanzisha sheria ya utumishi wa badala unaofaa

2004

Sheria ya Utumishi wa Badala yaanzishwa, lakini mpango wenyewe waendelea kusimamiwa na jeshi na hivyo kutowafaa Mashahidi wa Yehova

2006

Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Badala yaruhusu adhabu zihusishwe kwenye mpango huo huku mambo ya kijeshi yakiwemo na hivyo kutowafaa Mashahidi wa Yehova

2011

Katika uamuzi wa 16-1 wa kesi ya Bayatyan dhidi ya serikali ya Armenia, Baraza Kuu la mahakama ya ECHR lafikia mkataa kwamba uhuru wa dhamiri wa wale wanaokataa kujiunga na jeshi umevunjwa na laamua kulinda haki zao

2012

Maamuzi mawili ya Mahakama ya Ulaya dhidi ya nchi ya Armenia kuhusu suala la kutojiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri: Bukharatyan dhidi ya serikali ya Armenia na Tsaturyan dhidi ya serikali ya Armenia

2013

Juni 8, mabadiliko mengine yafanywa, na maagizo ya sheria hiyo yaanza kutumiwa mnamo Julai 25, hivyo kuwa na uwezekano wa kupata utumishi wa kiraia usiohusisha mambo ya kijeshi

Oktoba 8 na 9, Armenia yawaachilia huru kutoka gerezani wafungwa 8 waliokuwa wamekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao

Oktoba 23, Tume ya Jamhuri ya Armenia yakubali ombi la kuwasajili Mashahidi wa Yehova 57 kwenye mpango wa utumishi wa kiraia wa badala kutia ndani Mashahidi 6 kati ya wale 20 ambao bado wako gerezani nchini Armenia

Oktoba 24, Armenia yawaachilia huru Mashahidi sita waliofungwa kwenye Gereza la Erebuni

a Ona kesi ya Erçep dhidi ya Uturuki, na. 43965/04, 22 Novemba 2011; Bukharatyan dhidi ya Armenia, na. 37819/03, 10 Januari 2012; Tsaturyan dhidi ya Armenia, na. 37821/03, 10 Januari 2012; Feti Demirtaş dhidi ya Uturuki, na. 5260/07, 17 Januari 2012.