Hamia kwenye habari

Polisi walivamia mkutano wa kidini uliokuwa ukifanywa kwenye nyumba ya mtu binafsi katika jiji la Tomsk

JUNI 20, 2018
URUSI

Mashahidi Zaidi Wafungwa Baada ya Uvamizi Mbaya wa Nyumba Nchini Urusi

Mashahidi Zaidi Wafungwa Baada ya Uvamizi Mbaya wa Nyumba Nchini Urusi

Kwa miezi kadhaa sasa, wenye mamlaka nchini Urusi wameendeleza kampeni yao ya kuwatisha, kuwakamata na kuwafunga Mashahidi wa Yehova wengi zaidi kwa madai ya kupambana na msimamo mkali. Maofisa wa polisi walivamia nyumba katika maeneo ya Birobidzhan, Khabarovsk, Magadan, Orenburg, Naberezhnye Chelny, Perm, Pskov, Saratov, na Tomsk. Wamewakamata wanaume wengine 15 ambao ni Mashahidi, na kufanya idadi ya waliowekwa mahabusu ifikie Mashahidi 20. Wengine wawili wamehukumiwa kifungo cha nje. Mashahidi 15 hivi, kutia ndani wale wenye umri wa miaka kati ya 70 na 80 walikuwa wametakiwa kutia sahihi mkataba wa kutosafiri kutoka katika eneo wanaloishi. Juni 14, 2018, wenye mamlaka nchini Urusi waliwafungulia Mashahidi zaidi ya 40 mashtaka ya uhalifu. Wakipatikana na hatia, wanaweza kukabili kifungo cha hadi miaka kumi.

Maeneo ambako uvamizi ulitokea nchini Urusi

Serikali ya Urusi imekuwa ikikiuka waziwazi makubaliano iliyofanya katika mahakama ambapo ilidai kwamba kupigwa marufuku kwa mashirika ya kisheria ya Mashahidi wa Yehova hakutaweza kuathiri haki kila Shahidi kufanya ibada yake. Urusi haizingatii kabisa makubaliano haya na inatumia vibaya Kifungu cha 282 cha Sheria ya Uhalifu ili kuwashtaki Mashahidi kwa kushiriki, kupanga, au kutegemeza shirika “lenye msimamo mkali.” Kwa kweli, badala ya kupambana na msimamo mkali, Urusi inawatesa raia wake kwa sababu ya kufanya ibada kwa amani.

Uvamizi wa Karibuni, Kukamatwa, na Kuwekwa Mahabusu

Juni 12, 2018, Saratov. Polisi walivamia na kupekua nyumba kadhaa za Mashahidi na kuwapeleka Mashahidi kumi hivi katika kituo cha polisi kwa ajili ya kuwahoji. Wakati wakipekua nyumba moja, wenye mamlaka walipandikiza machapisho ya kidini ambayo awali yalipigwa marufuku na mahakama za Urusi. Mashahidi watano wanaume waliwekwa rumande. Wawili waliachiliwa baadaye, lakini polisi waliendelea kuwashikilia watatu na waliwashtaki Konstantin Bazhenov na Felix Makhammadiev kwa ‘kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali.’ Mashtaka ya uhalifu ya Shahidi wa tatu anayeitwa, Aleksey Budenchuk, bado hayajathibitishwa. Juni 14, 2018, Mahakama ya Wilaya ya Frunzenskiy, Saratov ilitoa uamuzi wa kuwaweka mahabusu Bw. Bazhenov na Bw. Makhammadiev hadi Agosti 12, 2018. Mahakama hiyohiyo pia ilitoa uamuzi kwamba Bw. Budenchuk awekwe mahabusu, lakini tarehe ya kutolewa haijajulikana. Katika kisa kingine, polisi walimwamuru Shahidi mwingine atie sahihi mkataba wa kutoondoka katika eneo analoishi.

Juni 3, 2018, Tomsk. Saa 04:00 asubuhi, polisi na washiriki wa Kikosi Maalum cha Jeshi la Urusi (Spetsnaz) walivamia nyumba mbili za Mashahidi wa Yehova katika eneo la Tomsk, Siberia. Waliwaweka mahabusu Mashahidi 30, kutia ndani na mwanamke mwenye umri wa miaka 83. Polisi walipora vitu vya kibinafsi kutoka katika nyumba na magari ya Mashahidi, wakawaingiza kwenye mabasi na kuwasindikiza hadi kwenye Kituo cha Kupambana na Msimamo Mkali.

Katika Kituo hicho, wapelelezi Ivan Vedrentsev, Aleksandr Ivanov, na Vyacheslav Lebedev walilazimisha kuwahoji baadhi ya Mashahidi hadi saa 8:00 ya usiku. Wachunguzi walimtisha mmojawapo wa wale waliowahoji kwamba watafanya afukuzwe kazi. Wakati walipokuwa wakiwahoji, gari la kubeba wagonjwa mahututi lililetwa mara kadhaa, na angalau Shahidi mmoja ndiye alipelekwa hospitali kutokana na mahojiano hayo.

Mmoja wa wale waliohojiwa anayeitwa, Sergey Klimov, aliwekwa rumande. Juni 5, 2018, Mahakama ya Wilaya ya Oktyabrskiy ya Tomsk ilimshtaki kwa ‘kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali’ na iliamuru aendelee kuwa mahabusu hadi Agosti 4, 2018. Hakimu alikataa hoja aliyotoa kwamba ahukumiwe kifungo cha nje au atolewe kwa dhamana.

Juni 3, 2018, Pskov. Polisi walivamia nyumba kadhaa za Mashahidi wa Yehova jijini Pskov. Katika nyumba moja, waliwazuia watu wote waliokuwepo na kuwahoji, kutia ndani wageni wawili ambao hawakuwa Mashahidi. Mashahidi wa Yehova kadhaa, kutia ndani Gennadiy Shpakovsky, walipelekwa kwenye Kituo Kikuu cha Mkoa wa Pskov cha Idara ya Usalama wa Taifa kwa ajili ya kuhojiwa. Baadhi ya wale waliopelekwa kwenye kituo cha polisi walilazimishwa watoe ushahidi dhidi ya Bw. Shpakovsky. Wenye mamlaka walimfungulia kesi kwa mashtaka ya ‘kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali.’ Ingawa aliachiliwa, maofisa wanaweza kumwongezea mashtaka wakati wowote.

Mei 30, 2018, Khabarovsk. Polisi walimkamata Ivan Puyda baada ya kuvamia nyumba yake na kuipekua. Walimpeleka Magadan, ambapo walimweka rumande. Juni 1, 2018, Mahakama ya Wilaya ya Zheleznodorozhniy ilimshtaki Bw. Puyda kwa ‘kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali’ na iliamuru awekwe mahabusu hadi Julai 30, 2018.

Mei 30, 2018, Magadan. Polisi waliokuwa na silaha ambao walifunika nyuso zao walivamia makazi ya kibinafsi katika eneo la Magadan na kuwakamata na kuwaweka kizuizini Konstantin Petrov, Yevgeniy Zyablov, na Sergey Yerkin. Juni 1, 2018, Mahakama ya Jiji la Magadan iliwashtaki Bw. Petrov na Bw. Zyablov kwa ‘kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali.’ Siku hiyohiyo, Mahakama ya Wilaya ya Magadanskiy pia ilimshtaki Bw. Yerkin madai hayohayo. Wanaume hao watatu Mashahidi waliamuriwa kubaki mahabusu hadi Julai 29, 2018.

Dmitriy Mikhailov

Mei 29, 2018, Shuya, Mkoa wa Ivanovo. Wenye mamlaka walimchukua Dmitriy Mikhailov na kumweka rumande kwa mara ya pili. Baada ya kuvamia nyumba yake Aprili 20, polisi walimshtaki kwa ‘kushiriki katika shughuli za shirika lenye msimamo mkali’ na kumtaka atie sahihi mkataba wa kutoondoka katika eneo analoishi. Mei 29, wenye mamlaka pia walimshtaki kwa ‘kutegemeza kifedha shughuli za watu wenye msimamo mkali.’ Juni 3, 2018, Mahakama ya Jiji la Shuya iliamuru awekwe mahabusu hadi Julai 19, 2018.

Mei 27, 2018, Naberezhnye Chelny, Jamhuri ya Tatarstan. Kwa usiku mzima, maofisa wa Usalama wa Taifa walipekua nyumba kumi na kupora vifaa vya kielektroni, simu za mkononi, na kuchukua pasipoti zao. Ilkham Karimov, Konstantin Matrashov, na Vladimir Myakushin walikamatwa na kuwekwa rumande. Mei 29, 2018, Mahakama ya Wilaya ya Naberezhnochelninskiy iliwashtaki wanaume watatu kwa kupanga na kutafuta wanachama wa shirika lenye msimamo mkali na kushiriki katika utendaji wake. Mahakama iliamuru wawekwe mahabusu hadi Julai 25, 2018. Baada ya muda, Aydar Yulmetyev alikamatwa pia, na Mei 31, 2018, mahakama iliamua awekwe mahabusu pia.

Mei 22, 2018, Perm. Aleksandr na Anna Solovyev walipofika tu kutoka Moldova, polisi waliwakamata katika kituo cha gari moshi, wakamfunga pingu Bw. Solovyev, wakapora vitu vyake na kuwapeleka wenzi hao wa ndoa katika kituo cha polisi kwa magari tofauti. Bw. Solovyev alipokuwa kizuizini, polisi walipekua nyumba yake na kumhoji mke wake. Mei 24, 2018, Mahakama ya Wilaya ya Sverdlovskiy ilimshtaki Bw. Solovyev kwa ‘kushiriki utendaji wa shirika lenye msimamo mkali’ na kumhukumu kifungo cha nje.

Mei 17, 2018, Birobidzhan. Katika msako mkali ulioitwa Siku ya Hukumu, maofisa wa polisi 150 na maofisa wa Usalama wa Taifa walivamia nyumba 22 za Mashahidi wa Yehova. Polisi walipora kompyuta ndogo, simu za mkononi, na pesa zao. Polisi walimkamata na kumfunga Alam Aliev, mmojawapo wa Mashahidi 34 ambao walipekuliwa wakati wa uvamizi. Mei 18, Mahakama ya Wilaya ya Birobidzhanskiy ilimshtaki kwa ‘kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali’ na kuamuru awekwe mahabusu hadi Julai 13, 2018. Mei 25, 2018, Hakimu A. V. Sizova wa Mahakama ya Rufaa ya Mkoa wa Utawala ya Kiyahudi alikubali rufaa ya Bw. Aliev na kuondoa amri ya kuwekwa mahabusu.

Mei 16, 2018, Orenburg. Maofisa wa polisi walivamia na kupekua nyumba za watu binafsi. Waliwakamata Mashahidi watatu wafuatao: Aleksandr Suvorov, Vladimir Kochnev, na Vladislav Kolbanov. Mei 18, Mahakama ya Wilaya ya Promyshlenniy ilimshtaki Bw. Kolbanov kwa ‘kutegemeza kifedha shughuli za shirika lenye msimamo mkali.’ Mahakama ilimwachilia lakini ilitoa uamuzi kwamba awe katika kifungo cha nje. Siku iliyofuata, mahakama hiyohiyo iliwashtaki Bw. Kochnev na Bw. Suvorov kwa ‘kupanga utendaji wa shirika lenye msimamo mkali’ na kuamuru awekwe mahabusu hadi Julai 14, 2018. Wapelelezi pia waliamuru Mashahidi wengine saba watie sahihi mkataba wa kutosafiri nje ya jiji kwa muda wote wa uchunguzi.

Kushoto: Aleksandr Suvorov; Kulia: Vladimir Kochnev

Je, Shutuma za Kimataifa Zitakuwa na Matokeo?

Umoja wa Ulaya na nchi ya Marekani zote kwa pamoja zimetoa maelezo rasmi ya kushutumu matendo ya Urusi ya kukiuka uhuru wa msingi. Umoja wa Ulaya uliieleza Urusi “iheshimu mikataba yake ya kimataifa kuhusu uhuru wa ibada au imani, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa kukusanyika.” Kwa kuongeza, Marekani iliisihi Urusi “iwaachilie mara moja wale wote iliyowafunga kwa sababu tu ya kutekeleza uhuru wao wa kidini au kuamini.”

Philip Brumley, Wakili wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanahangaishwa sana na mateso makali wanayokabili waabudu wenzao nchini Urusi. Mashahidi wa Yehova wanakabili hali ileile ambayo ndugu zao walikabili katika kipindi cha Ukomunisti. Kupitia matendo yake na ukandamizaji unaoendelea sasa, Urusi inakiuka kimakusudi makubaliano iliyofanya yenyewe ya kutetea haki za msingi za kibinadamu.”

Mashahidi ambao awali waliwekwa mahabusu a

  • Dennis Christensen

    Mwenye umri wa miaka 45, Oryol, aliwekwa mahabusu tangu Mei 25, 2017, na aliamriwa abaki mahabusu hadi Agosti 1, 2018.

  • Valentin Osadchuk

    Mwenye umri wa miaka 42, Vladivostok, aliwekwa mahabusu tangu Aprili 19, 2018, na aliamriwa abaki mahabusu hadi Juni 20, 2018.

  • Viktor Trofimov

    Mwenye umri wa miaka 61, Polyarny, aliwekwa mahabusu tangu Aprili 18, 2018, na aliamriwa abaki mahabusu hadi Oktoba 11, 2018.

  • Roman Markin

    Mwenye umri wa miaka 44, Polyarny, aliwekwa mahabusu tangu Aprili 18, 2018, na aliamriwa abaki mahabusu hadi Oktoba 11, 2018.

  • Anatoliy Vilitkevich

    Mwenye umri wa miaka 31, Ufa, aliwekwa mahabusu tangu Aprili 10, 2018, na aliamriwa abaki mahabusu hadi Julai 2, 2018.

a Kwa habari zaidi, ona makala kwenye sehemu ya Habari katika jw.org yenye kichwa “Kampeni ya Kuwatisha Mashahidi wa Yehova Yaanza Nchini Urusi.”