Hamia kwenye habari

Habtemichael Tesfamariam akiwa na mke wake, Leterberhan Bezabih, kabla ya kufungwa

APRILI 25, 2018
ERITREA

Mashahidi Wawili Wazee Wamekufa Wakiwa Gerezani Nchini Eritrea

Mashahidi Wawili Wazee Wamekufa Wakiwa Gerezani Nchini Eritrea

Mashahidi wawili wa Yehova, Habtemichael Tesfamariam na Habtemichael Mekonen, wamekufa wakiwa katika gereza la Mai Serwa karibu na Asmara mwanzoni mwa mwaka 2018. Wote wawili walikamatwa na kufungwa katika majira ya kiangazi ya mwaka 2008 kwa sababu ya imani yao ya dini na wamekabili hali ngumu sana ya kuwa katika mazingira mabaya ya gerezani kwa karibu miaka kumi.

Bw. Tesfamariam alikufa ghafla Januari 3, 2018 katika gereza la Mai Serwa akiwa na umri wa miaka 76. Wafungwa wenzake wanaamini kwamba alikufa kwa sababu ya mshtuko wa moyo. Bw. Tesfamariam alizaliwa mwaka wa 1942 huko Adi Yakulu, Mendefera, Eritrea. Alikuwa Shahidi wa Yehova mwaka 1970 na alikataa kukana imani yake licha ya kufungwa isivyo haki na kutendewa vibaya. Ameacha mke, Leterberhan Bezabih; wavulana wanne na binti watatu.

Bw. Mekonen alikufa Machi 6, 2018 katika gereza la Mai Serwa akiwa na umri wa miaka 77. Wafungwa wenzake wanaamini kwamba alikufa kwa sababu ya ugonjwa wa figo. Bw. Mekonen alizaliwa mwaka 1940 katika kijiji cha Kudo Felasi kusini mwa Eritrea. Alikuwa Shahidi zaidi ya miaka 55 iliyopita na kama Bw. Tesfamariam, alikataa kukana imani yake, ingawa alifungwa bila sababu na kutendewa isivyo haki. Ameacha mke, Mihret Ellias, pamoja na mwana na binti.

Kukamatwa Isivyo Haki na Kutendewa Isivyofaa

Bw. Mekonen alikamatwa Julai 2008 na wenye mamlaka akiwa nyumbani kwake bila mashtaka yoyote, na Bw. Tesfamariam pia alikamatwa Agosti 2008 na wenye mamlaka akiwa nyumbani kwake bila mashtaka yoyote. Wote wawili walipelekwa kwenye kambi inayojulikana kwa mateso ya Meitir, katika jangwa lililoko kaskazini ya Asmara, ambako walikabili hali mbaya sana na isiyo ya kawaida. Ili kuwapa wafungwa Mashahidi adhabu maalumu, wenye mamlaka waliwafunga katika jengo ambalo nusu yake iko chini ya ardhi linalojulikana kama “chini ya ardhi” tangu Oktoba 2011 hadi Agosti 2012. Katika gereza hilo wafungwa wanateseka sana kutokana na joto kali huku wakipata chakula kidogo au maji kidogo. Kwa sababu ya hali hizo baadhi ya wafungwa wamekabili hali mbaya sana ya kiafya.

Mwaka wa 2017, wenye mamlaka waliwahamisha Mashahidi waliofungwa kwenye kambi ya Meitir na kuwapeleka kwenye gereza la Mai Serwa, ambako wanaruhusiwa kupata chakula kutoka kwa ndugu zao wa ukoo na kupata matibabu ikiwa wanakabili hali mbaya ya afya. Wafungwa wengi walifurahi kuhamishiwa katika mazingira yasiyo mabaya sana, lakini hali ya Bw. Tesfamariam na Bw. Mekonen haikuwa nzuri kutokana na jinsi walivyotendewa isivyofaa awali.

Habtemichael Mekonen akiwa na mke wake, Mihret Ellias, kabla ya kufungwa

Bw. Tesfamariam na Bw. Mekonen si Mashahidi wa kwanza kufa wakiwa katika magereza ya Eritrea au muda mfupi baada ya kuachiliwa kutoka gerezani. Kutokana na kutendewa isivyofaa na kuteswa, Mashahidi wengine wawili walikufa wakiwa gerezani, na Mashahidi wengine watatu walikufa muda mfupi baada ya kuachiliwa. Mashahidi saba walioachiliwa kutoka gerezani miaka kadhaa iliyopita bado wanaendelea kukabili matatizo makubwa ya afya kwa sababu ya hali ngumu walizopitia wakiwa gerezani. Mashahidi 53, kutia ndani kaka ya Bw. Tesfamariam anayeitwa Tareke, wamefungwa gerezani nchini Eritrea kwa sababu ya imani yao.

Mateso Ni “Uhalifu Dhidi ya Binadamu”

Juni 8, 2016, Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu lilichapisha ripoti iliyotegemea uchunguzi wa Tume ya Haki za Kibinadamu Nchini Eritrea (COIE). Baraza hilo limeanzishwa ili kuchunguza matendo ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu nchini Eritrea. COIE iliisihi Eritrea “iheshimu uhuru wa ibada au imani” na “ikomeshe matukio ya kuwakamata isivyo haki na kuwaweka watu mahabusu kwa kutegemea imani yao ya kidini, kwa kukazia uangalifu hasa vikundi fulani vya kidini, kama vile Mashahidi wa Yehova, . . . na iwaachilie mara moja na bila masharti yoyote wale wote waliofungwa isivyo haki.” COIE ilikata kauli kwamba mateso yanayofanywa na serikali ya Eritrea dhidi ya watu kwa kutegemea imani yao ya kidini ni “uhalifu dhidi ya binadamu.”

Mashahidi wa Yehova wanatumaini kwamba vifo vya Bw. Tesfamariam na Bw. Mekonen vilivyotokea hivi karibuni vitafanya mashirika ya kimataifa yatambue hali wanazokabili Mashahidi na vitawachochea maofisa wa Eritrea wenye usawaziko kuchukua hatua kuwasaidia waliofungwa isivyo haki kwa sababu ya imani yao.