Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Maziwa ya Mama

Maziwa ya Mama

 Kitabu kimoja cha marejezo cha ukunga kinasema, “maziwa ya unga yanayotengenezwa kwa ajili ya watoto hayawezi kufanana kamwe na maziwa ya mama.” Sababu moja inayofanya maziwa ya mama kuwa bora kwa mtoto, ni kwamba mwili wake huyabadilisha kulingana na mahitaji ya mtoto.

 Fikiria hili: Kila mara mama anapomnyonyesha mtoto, maziwa yake hubadilika kadiri mtoto anavyozidi kunyonya. Maziwa yanayotoka kwanza yanakuwa na protini, vitamini, madini, na maji mengi zaidi, lakini maziwa yanayotoka baadaye yanakuwa na mafuta mengi na yanamfanya mtoto ashibe. Isitoshe, maziwa yake hubadilika kulingana na umri wa mtoto na majira.

 Baadhi ya homoni katika maziwa ya mama, kama vile melatonin, huongezeka usiku, na homoni nyingine huongezeka mchana. Mabadiliko hayo ya homoni humfanya mtoto ahisi usingizi au awe makini, na hilo humsaidia mtoto asitawishe utaratibu hususa wa kulala na kuamka.

 Siku chache za kwanza baada ya kujifungua, mama hutoa maziwa yenye rangi ya njano yanayoitwa kiamo. Ni rahisi kwa mtoto kumeng’enya maziwa hayo ya mwanzo na ni yenye lishe hivi kwamba, hata anaponyonya kidogo tu ananufaika sana. Maziwa ya kiamo yana kingamwili muhimu ambazo humlinda mtoto asiambukizwe magonjwa. Kwa kuongezea, yanamsaidia mtoto kutoa uchafu tumboni, na hivyo kusafisha tumbo lake.

 Mama hahitaji kuwa na wasiwasi kuhusu kuwa na maziwa ya kutosha, kwa sababu hata anapopata mapacha, maziwa yake yataongezeka kulingana na uhitaji uliopo.

 Una maoni gani? Je, maziwa ya mama ambayo ni ya pekee sana, yalijitokeza yenyewe? Au yalibuniwa?