Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Fahali Katika Duka la Kuuza Kauri

Je, umewahi kufikiria kile kinachoweza kutukia fahali akiingia katika duka la kuuza kauri? Shirika la Habari la BBC liliripoti kisa kama hicho. Fahali alitoroka kutoka kwenye mnada wa mifugo huko Lancashire, Uingereza, kisha akaingia katika duka la kuuza vitu vya kale. Gazeti moja lililoripoti kisa hicho lilisema kwamba “duka hilo huuza vyombo vya zamani vya kauri, na kama ilivyotarajiwa, fahali huyo alikanyaga-kanyaga vyombo kadhaa vya thamani.” Baada ya kuzungumza na mwenye fahali na kufikiria hatari mbalimbali za kumkamata mnyama huyo, iliamuliwa kwamba inafaa fahali huyo auawe. Kwa hiyo polisi walizingira eneo hilo na kumpiga risasi fahali huyo aliyekuwa dukani.

Nchi Inayopata Radi Nyingi

Kulingana na gazeti O Globo, watafiti wanaochunguza habari za setilaiti wamegundua kwamba “Brazili ndiyo nchi inayopata radi nyingi sana ulimwenguni. Cheche mbili au tatu za umeme hutokea [nchini Brazili] kila sekunde, zikifanyiza jumla ya cheche milioni 70 kila mwaka.” Ni nini kinachosababisha hali hiyo? Ni misitu mingi ya mvua na joto kali. Mambo hayo huchangia sana kutokea kwa radi. Mbali na kusababisha vifo vya Wabrazili 100 hivi kila mwaka, radi husababisha hasara ya dola milioni 200 hivi wakati inapoharibu nyaya za umeme na za simu na vilevile vifaa vya viwandani na vinginevyo. Tofauti na maoni ya wengi, “radi inaweza kutukia mara tatu, tano, au hata kumi mahali palepale,” asema mwanasayansi Osmar Pinto, Jr., wa Taasisi ya Kitaifa ya Kuchunguza Mambo ya Angani.

Kutumia Simu za Mkononi Kupeleleza

Gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung linaripoti kwamba simu za mkononi zenye kamera ni hatari kwa habari za siri za kibiashara. Ijapokuwa hapo awali kamera hizo zilidhaniwa kuwa zingeleta faida, simu hizo za kisasa za mkononi zinapiga picha safi sana na hivyo kuwapa wasiwasi maafisa wa usalama katika kampuni nyingi. Zaidi ya kwamba hazionekani kwa urahisi, kamera hizo ni tofauti na kamera za kawaida kwani zinamwezesha mtu kupata picha mara moja na hivyo zinaweza kutumiwa na wapelelezi wa viwanda. Hata mtu anayepiga picha hiyo akikamatwa, tayari mambo huwa yameharibika. Hivyo, kampuni kadhaa zimepiga marufuku simu za mkononi zenye kamera mahali penye ulinzi mkali, kama vile katika idara za uchoraji na mahali ambapo bidhaa mpya zinajaribiwa.

Misiba Mingi ya Barabarani

Gazeti El País la Hispania linasema kwamba “watu wengi zaidi hufa katika misiba ya barabarani kuliko kutokana na uhalifu.” Kila mwaka, watu 55,000 hufa na milioni 3.5 hujeruhiwa katika misiba ya barabarani huko Ulaya. Nchini Hispania, asilimia 35 ya watu wanaokufa katika misiba ya barabarani wako kati ya umri wa miaka 15 na 29, hivyo misiba hiyo ndicho kisababishi kikuu cha vifo vya watu wa umri huo. Jeanne Picard Mahaut, msemaji wa La Ligue, shirika lisilo la kiserikali ambalo limejitoa kuhakikisha usalama barabarani, anasema: “Hilo ndilo tatizo kubwa la afya ya umma.” Anaongeza hivi: “Ikiwa hamniamini, basi waulizeni madaktari ambao huwashughulikia wagonjwa wa dharura kila mwisho wa juma.” Kati ya hatua nyingine, shirika hilo na mashirika mengine mawili ya Ulaya yanataka vifaa vya kudhibiti mwendo viwekwe ndani ya magari na vilevile kifaa cha kuonyesha chanzo cha msiba wa barabarani.

Mwaka Ambao Barafu Iliyeyuka Zaidi

Gazeti la Italia Corriere della Sera lilisema kwamba majira ya joto kali ya mwaka wa 2003 yalikuwa “majira mabaya zaidi” kwa mito ya barafu ya milimani. Kutokana na ongezeko la joto kali wakati wa kiangazi, theluji na barafu iliyotanda juu ya milima ya kaskazini mwa Italia imeyeyuka “haraka kuliko wakati mwingine wowote.” Kitu kimoja cha kushangaza kilichopatikana katika barafu iliyoyeyuka ni mzinga uliotengenezwa Austria wenye uzito wa kilogramu 3,300, ambao ulipatikana meta 3,178 juu ya usawa wa bahari. Mzinga huo ulitumiwa kushambulia majeshi ya Waitaliano wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Makala hiyo inasema: “Kumekuwa na uvumbuzi mwingi kama huo katika miaka 20 iliyopita. Joto kali la kiangazi limefanya mito ya barafu iyeyuke sana kama friji iliyofunguliwa.”

Tatizo la Kujiua Huko Korea Kusini

Gazeti The Korea Times linaripoti kwamba “visa vya kujiua vimeongezeka kila mwaka nchini Korea Kusini tangu mwaka wa 1999. Katika miezi ya karibuni, visa vya kujiua vimeripotiwa karibu kila siku, hasa vikisababishwa na matatizo ya kiuchumi kama vile madeni ya kadi za mikopo na mfadhaiko. Kulingana na habari zilizotolewa na Idara ya Polisi ya Kitaifa, watu 13,055 walijiua [katika mwaka wa 2002], hilo likiwa ongezeko la asilimia 6.3 ikilinganishwa na watu 12,277 mwaka uliotangulia. Hiyo inamaanisha kwamba watu 36 hujiua kila siku, na watu 1.5 kila saa moja.” Lakini kuna jambo la kuogopesha hata zaidi. Gazeti Times linasema: “Wazazi waliofadhaika huwaua watoto wao kwanza kisha wanajiua.” Kwa mfano, mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 37 alijiua alipogundua kwamba mume wake alipoteza dola 140,000 za Marekani katika biashara ya hisa. Watoto wake wawili—mwana wake wa miaka 14 na binti yake wa miaka 12—walipatikana pia wakiwa wamekufa. Makala hiyo inamalizia kwa kusema: “Wanasaikolojia wanasema kwamba watu wengi zaidi wanaamua kujiua kwa kuwa jamii haiwasaidii kutatua matatizo yao.”

Wasafiri Wanaoambukizwa Magonjwa

Gazeti The Medical Post la Kanada linasema: “Ulimwenguni pote, zaidi ya msafiri mmoja kati ya tisa hupata magonjwa ya kupumua.” Habari hizo zilitokana na uchunguzi uliofanywa na GeoSentinel, kikundi kinachohusiana na Chama cha Kimataifa cha Matibabu ya Wasafiri na Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa. Kikundi hicho hukusanya habari na kina kliniki 25 ulimwenguni pote zinazowatibu wasafiri. Kati ya Januari 1997 na Desemba 2002, wasafiri 18,817 walienda kwenye kliniki hizo na 2,173 walipatikana na magonjwa kama vile kuumwa na koo, maambukizo kwenye sikio, kwenye uwazi wa mfupa unaowasiliana na pua (sinus), mkamba, na maambukizo ya bakteria sugu. Wasafiri wanaotembelea nchi zenye maambukizo mengi wanashauriwa kuhakikisha kwamba wamepata chanjo karibuni na vilevile wapate chanjo za mafua hata iwe ni wakati gani wa mwaka. Kulingana na Dakt. Isabelle Nuttall, mtaalamu wa maambukizo kwenye Shirika la Afya Ulimwenguni, usafi ndio kinga ya msingi dhidi ya maambukizo ya bakteria au virusi. Alisema: “Tunataka kukazia sana jambo hili, ‘Nawa mikono.’”