Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Daraja Lililojengwa Upya Mara Nyingi

Daraja Lililojengwa Upya Mara Nyingi

Daraja Lililojengwa Upya Mara Nyingi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BULGARIA

KWENYE Mto Osŭm ulio kaskazini ya kati ya Bulgaria kuna daraja lililoezekwa la Lovech. Daraja hilo la kupendeza lina historia yenye kusisimua kama tu ya watu wa eneo hilo.

Mwanajiolojia Mwaustria Ami Boué, aliyetembelea eneo la Lovech katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 alikuwa kati ya watu wa kwanza kuzungumza kuhusu daraja hilo. Aliandika kuhusu “daraja la mawe, lililokuwa na paa na lililopambwa kwa maduka madogo.” Naam, daraja hilo la pekee lilikuwa sehemu ya mfumo wa usafiri wa Lovech, likiunganisha sehemu mbili za mji huo, na pia lilitumiwa kama soko! Kwa sababu hiyo, lilikuwa sehemu muhimu ya jamii hiyo.

Mwanzoni, daraja la Lovech lililokuwa na paa lilijengwa kwa mbao, si kwa mawe. Hata hivyo, kadiri miaka ilivyopita daraja hilo liliharibiwa mara nyingi na mafuriko na hivyo lilihitaji kujengwa upya. Mwishowe, mnamo 1872, daraja hilo lilifagiliwa mbali na mafuriko na kuwafanya watu wa mji huo kukosa njia hiyo muhimu ya kuwaunganisha na miji mingine.

Kujenga upya daraja hilo halikuwa jambo rahisi. Hivyo, Kolyo Ficheto, mjenzi maarufu Mbulgaria, alipewa kazi ya kubuni na kujenga daraja jipya lililo imara.

Ubunifu Mpya wa Pekee

Ficheto aliamua kufuata muundo wa daraja la kwanza lililokuwa na paa likiwa na maduka madogo. Ili kutegemeza daraja hilo lenye urefu wa mita 84 na upana wa mita 10, aliongeza gati zenye umbo la yai. Gati hizo zenye kimo cha mita 5, ambazo miisho yake ilielekea upande wa juu wa mto, zilikuwa na muundo mpya. Katikati ya gati hizo kulikuwa na mianya iliyokaribia kufika juu ya gati hizo ili kuruhusu maji ya mafuriko yapite. Juu ya gati, Ficheto aliweka nguzo za mialoni. Sehemu nyingine za daraja hilo, kutia ndani maduka 64 yaliyokuwa upande huu na huu wa daraja hilo, zilijengwa kwa mbao za mifune. Pia paa lilijengwa kwa mbao za mifune na kuezekwa kwa mabati.

Jambo lingine lenye kupendeza kuhusu ujenzi wa Ficheto ni kwamba alitumia vizibo na viunganishi vya mbao badala ya vyuma na misumari ili kuunganisha daraja hilo. Alitandaza mbao na kisha kufunika mbao hizo kwa mawe na akaweka changarawe juu ya mawe hayo. Mchana, madirisha madogo na mianya kwenye paa iliruhusu mwanga wa jua upenye. Jioni, taa za mafuta ziliwashwa. Kwa ujumla, uchoraji na ujenzi wa daraja hilo ulichukua miaka mitatu hivi [1].

Shughuli Kwenye Daraja

Maisha yalikuwaje juu ya daraja hilo? Mtazamaji mmoja alisema hivi: “Wauzaji, wapita-njia, na watazamaji, ambao hawakusumbuliwa na magari yaliyokuwa yakipita, magari ya kukokotwa kwa farasi, au punda waliobeba mizigo, waliongea kwa sauti huku kelele za wafua-mabati . . . na za wachuuzi, waliokuwa wakitangaza bidhaa zao kwa sauti kubwa zikiongezea kelele hizo. Daraja hilo lilikuwa na shughuli zake za pekee. Maduka mengi yenye rangi maridadi yaliyojaa vitu vilivyofumwa, shanga, na bidhaa mbalimbali, yalikuwa na utaratibu wake wa pekee.”

Zaidi ya kununua bidhaa kwenye daraja hilo lililoezekwa, watu walikusanyika huko kwa ajili ya burudani kwa kuwa wengi wa wenye maduka walikuwa pia wanamuziki. Mtazamaji aliyenukuliwa awali alisema hivi: “Katika vibanda vya vinyozi, kulikuwa na vinyozi watano au sita ambao, mbali na kuwa vinyozi, walikuwa wanamuziki wazuri waliopiga hasa vyombo vya nyuzi. Mara nyingi walipata wakati wa kupiga muziki, na wateja wao walifurahia kuwangoja mpaka wamalize.” Baada ya vita vya ulimwengu vya kwanza, baadhi ya vinyozi hao walikuwa waanzilishi wa ile iliyoitwa Okestra ya Vinyozi.

Msiba Watokea

Kwa karibu miaka 50, daraja la Ficheto lilistahimili mafuriko, vita, na majanga mengine. Lakini usiku wa Agosti 2/3, 1925, moto mkubwa ulizuka huko Lovech na daraja hilo likateketea kabisa. Hilo lilitukiaje? Kufikia leo hakuna mtu anayejua ikiwa moto huo ulisababishwa na ukosefu wa uangalifu au lilichomwa kwa makusudi. Vyovyote vile, kwa mara nyingine tena, Lovech ilikuwa bila daraja la kuunganisha fuo zake.

Mnamo 1931, daraja jipya lenye maduka madogo na vibanda lilikamilika [2]. Hata hivyo, badala ya kujenga daraja hilo kwa mbao na mawe, mjenzi mpya alitumia vyuma na zege. Muundo huo ulikuwa tofauti kabisa na ule wa Ficheto. Paa lilikuwa la kioo na sehemu fulani ya katikati ya daraja hilo haikuwa na kuta za nje. Mnamo 1981/1982, daraja hilo lilijengwa upya kulingana na ujenzi wa awali wa Kolyo Ficheto [3].

Daraja lenye paa la Lovech ni ishara maarufu ya mji huo na ubunifu wa mjenzi stadi. Leo daraja hilo lililo na maduka, linaendelea kuwavutia wenyeji na wageni wanapotembea kwenye daraja hilo.

[Ramani katika ukurasa wa 22]

 

BULGARIA

SOFIA

Lovech

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Photo 2: From the book Lovech and the Area of Lovech