Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jeuri Dhidi ya Wanawake—Tatizo la Ulimwenguni Pote

Jeuri Dhidi ya Wanawake—Tatizo la Ulimwenguni Pote

Jeuri Dhidi ya Wanawake—Tatizo la Ulimwenguni Pote

NOVEMBA (Mwezi wa 11) 25 ni Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Jeuri Dhidi ya Wanawake. Siku hiyo iliwekwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka wa 1999 ili kuhamasisha umma kuhusu kuvunjwa kwa haki za wanawake. Kwa nini hatua hiyo ilihitajika?

Katika jamii nyingi, wanawake huonwa na kutendewa kama raia wa hali ya chini. Ubaguzi dhidi yao umekita mizizi. Aina mbalimbali za jeuri dhidi ya wanawake ni tatizo la kuendelea, hata katika nchi zilizoendelea. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alisema kwamba “jeuri dhidi ya wanawake imeenea ulimwenguni pote na ni jambo linalotukia katika jamii na utamaduni wote. Inawaathiri wanawake haidhuru rangi, kabila, malezi, au hali zao nyingine.”

Radhika Coomaraswamy, Katibu Maalumu wa zamani wa Umoja wa Mataifa wa Tume ya Haki za Kibinadamu kuhusu jeuri dhidi ya wanawake, anasema kwamba kwa wanawake wengi, jeuri dhidi ya wanawake ni “suala lisilozungumziwa, linalofichwa katika jamii, na jambo la aibu lisiloweza kuepukika.” Takwimu zilizotolewa na taasisi ya kuchunguza uonevu huko Uholanzi zinaonyesha kwamba asilimia 23 ya wanawake katika nchi moja ya Amerika Kusini, yaani, mwanamke 1 kati ya 4 hutendewa aina fulani ya jeuri nyumbani. Pia, Baraza la Ulaya linakadiria kwamba mwanamke 1 kati ya 4 huko Ulaya hutendewa jeuri nyumbani angalau mara moja maishani. Kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza, imekadiriwa kwamba katika mwaka mmoja hivi karibuni huko Uingereza na Wales, kwa wastani, wanawake wawili waliuawa kila juma na wapenzi wao wa zamani au wa sasa. Gazeti India Today International liliripoti kwamba “wanawake nchini India, huishi kwa woga, na kulalwa kinguvu ni jambo wanaloweza kukabili katika kila kona, kila barabara, mahali popote pa umma, wakati wowote ule.” Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International linasema kwamba leo, jeuri dhidi ya wanawake na wasichana ndilo “tatizo kubwa zaidi linalohusiana na kuvunjwa kwa haki za kibinadamu.”

Je, takwimu zilizotajwa zinaonyesha mtazamo wa Mungu kuhusu wanawake? Swali hilo litazungumziwa katika makala inayofuata.