Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuhifadhi Joto Katika Theluji

Kuhifadhi Joto Katika Theluji

Kuhifadhi Joto Katika Theluji

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND

BILA nguo za kutosha na viatu vinavyofaa, wanadamu wangeumia sana au hata kuangamia katika majira ya baridi kali katika maeneo ya Kaskazini ya Mbali. Lakini wanyama wengi wanaendelea na maisha yao ya kawaida katika majira yote. Zaidi ya kuwa na manyoya mengi, wanyama pia hutumia uwezo mzuri wa theluji wa kuzuia baridi isipenye ndani.

Theluji hufanyizwa kwa chembe ndogo za barafu ambazo hutokana na mvuke wa maji. Theluji yenye kina cha sentimita 25 ni sawa na maji yenye kina cha sentimita 2.5 hivi. Kwa hiyo, theluji ina kiasi kikubwa cha hewa ambacho kinapatikana katikati ya chembe hizo za barafu. Muundo huu wa ajabu unafanya theluji isipenye baridi kali, na hivyo kulinda mbegu na mimea hadi majira ya kuchipua. Kisha, mkusanyo huo wa maji yaliyoganda unayeyuka na kulowesha mchanga na kuingia kwenye vijito.

Maisha Chini ya Theluji

Wakipitia mitaro mingi iliyo chini ya theluji, wanyama fulani wadogo wenye manyoya wanaendelea na shughuli zao, wakati mwingi wakitafuta chakula. Wanyama hao wanatia ndani lemming, panyabuku, na aina ya fuko ambao hula wadudu nyakati za usiku. Nao panya wengine wanaonekana wakikimbia juu ya theluji wakitafuta beri, njugu, mbegu, na maganda ya miti michanga.

Wanyama wadogo wanawezaje kudumisha joto la mwili linalofaa? Zaidi ya kuwa na manyoya mengi, wanyama wengi pia hutokeza joto jingi kwa kuyeyusha chakula haraka. Kwa hiyo, ili waweze kutokeza joto jingi wanahitaji kula chakula kingi. Kwa mfano, kila siku panya hula kiasi cha wadudu kinachokaribia uzito wao. Nao aina fulani ya panya wadogo wanakula chakula kingi hata zaidi! Kwa hiyo, wanatumia karibu wakati wao wote kutafuta chakula.

Panya hao wanawindwa sana na wanyama fulani kutia ndani bundi na jamii kadhaa za kicheche, na ermine. Vicheche ni wanyama wembamba na wepesi, kwa hiyo ni rahisi kwao kupitia chini ya theluji katika vijia vilivyofichika wanapotafuta chakula. Wao huwinda hata sungura, wanyama wanaowazidi kwa ukubwa.

Bundi pia huwinda. Bundi mkubwa wa rangi ya kijivu ana uwezo mkubwa wa kusikia hivi kwamba anaweza kumfuata panyabuku anayetembea chini ya theluji ikiwa theluji hiyo si yenye kina kirefu. Bundi anapomwona mnyama anayetaka, anaruka na kuingia ndani ya theluji na kumbeba akitumia kucha zake. Hata hivyo, kukiwa na theluji yenye kina kirefu wawindaji hukosa chakula au hata kufa na wanyama wanaowindwa huongezeka sana.

Ili wasife njaa katika majira ya baridi kali, wanyama wengi hutumia mafuta waliyokusanya katika miezi yenye joto. Lakini kwa kawaida wao hupata kiasi fulani cha chakula. Kwa mfano, kongoni hula matawi ya miti michanga hasa misonobari. Kindi hula mbegu walizokusanya na kuhifadhi, nao sungura-mwitu hula maganda ya miti michanga, matawi, na majani. Jamii fulani za ndege hufurahia beri zilizoganda na vitawi vya msonobari.

Kuingia Ndani ya Theluji!

Ndege kadhaa hutumia uwezo wa theluji wa kuzuia baridi isipenye kwa kupumzika wakati wa mchana au kulala wakati wa usiku chini ya theluji. Ndege hao wanatia ndani hazel hen, kwale weusi, na ptarmigan, pia ndege wadogo zaidi kama vile linnet, aina fulani ya shorewanda, na shore. Ikiwa theluji ina kina kirefu na ni nyororo, ndege fulani huingia ndani ya theluji, kama vile tu ndege wa baharini wanavyopiga mbizi majini. Mbinu hiyo inawasaidia wasiache alama zitakazoonekana au kunuswa na wanyama wanaowinda.

Baada ya kuingia ndani ya theluji, ndege hao wanachimba shimo lenye upana wa sentimita 60 hivi linaloitwa kieppi katika Kifini. Upepo unaovuma usiku unafanya isiwe rahisi kutambua kwamba kuna viumbe chini ya theluji. Watu wanaotembea wanapofika karibu sana, ndege hao wanawasikia kwa sababu ya kelele ya kutembea kwao. Wanaporuka ghafula na kutifua theluji huku wakipiga mabawa yao wanaweza kumshtua sana mtu ambaye hakuwatarajia.

Manyoya Katika Majira ya Baridi Kali

Majira yanapobadilika, wanyama fulani wa maeneo ya aktiki wananyonyoka manyoya ya majira ya kiangazi na kumea manyoya ya majira ya baridi kali yanayofanana na theluji. Huko Finland, mbweha wa aktiki, sungura-mwitu, na jamii kadhaa za vicheche, wanakuwa na manyoya mengi meupe au ya rangi inayokaribia hiyo katika majira ya kupukutika kwa majani.

Vivyo hivyo, ptarmigan hubadilisha manyoya yake yenye madoadoa ya majira ya kiangazi na kupata manyoya meupe kabisa. Pia, kucha zao ambazo huwa hazina manyoya mengi wakati wa kiangazi, zinakuwa na manyoya mengi na hivyo anakuwa ni kama amevaa viatu vya theluji. Hata wanaponyonyoka manyoya yao, jamii fulani hulindwa kwa sababu mchanganyiko wa manyoya yanayonyonyoka na yanayomea unaonekana kama mchanga uliofunikwa kidogo na theluji.

Je, umewahi kujiuliza ni kwa nini ndege, wengi wao wanaotembea kwenye theluji au barafu bila viatu hawapati madhara? Kwa sababu wana mfumo wa kuongeza joto miguuni. Mfumo huo wa ajabu unafanya damu yenye joto kutoka kwa moyo iende miguuni na kupasha joto damu baridi inayotoka miguuni.

Ndiyo, kutoka ncha ya Kaskazini na Kusini ya dunia hadi maeneo ya Tropiki, viumbe hawastahimili tu hali mbaya ya hewa. Badala yake, wanasitawi katika hali hizo. Kwa kawaida, wanaume na wanawake wanaogundua na kupiga picha viumbe katika hali hizo hupewa sifa wanazostahili kwa jitihada zao. Lakini, tunapaswa kumsifu Muumba wa viumbe wa ajabu wa dunia hata zaidi! Andiko la Ufunuo 4:11 linasema hivi: “Unastahili, Ee Yehova, naam, Mungu wetu, kupokea utukufu na heshima na nguvu, kwa sababu uliumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako navyo vikaumbwa.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

Wahubiri Wasiojali Hali ya Hewa!

Katika miezi ya majira ya baridi kali, Mashahidi wa Yehova huko Finland huvaa nguo za kujikinga baridi na kuendelea na utendaji wao wa kiroho. Kwa furaha, Mashahidi fulani husafiri mwendo mrefu ili kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Kwa kweli, hudhurio huko vijijini halipungui wakati wa miezi mirefu ya baridi kali. Pia Mashahidi wa Yehova wana bidii katika utumishi wa hadharani. Wao huliona kuwa pendeleo kubwa kutoa ushahidi kumhusu Muumba, Yehova Mungu, hivi kwamba wanaacha nyumba zao zenye joto ili washiriki katika kazi ya kutangaza Ufalme wake.—Mathayo 24:14.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Koikoi ndani ya pango

[Hisani]

By courtesy of John R. Peiniger

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

“Ermine”

[Hisani]

Mikko Pöllänen/Kuvaliiteri

[Picha katika ukurasa wa 17]

Bata-maji

[Picha katika ukurasa wa 17]

Sungura-mwitu

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mbweha wa Aktiki