Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nyani Walifikaje Gibraltar?

Nyani Walifikaje Gibraltar?

Nyani Walifikaje Gibraltar?

NYANI wengi huishi maeneo yenye joto. Hata hivyo, kuna jamii moja au mbili ambazo huishi maeneo yenye baridi.

Kwenye Milima ya Atlasi ya Afrika Kaskazini ambako theluji humwagika wakati wa majira ya baridi kali, vikundi vidogo vya nyani wanaoitwa Barbary hupatikana katika misitu ya mierezi na mialoni. * Kikundi kimoja cha nyani hao kinapatikana kilomita 300 upande wa kaskazini, juu ya Mwamba wa Gibraltar, unaopakana na Ulaya.

Wataalamu wa viumbe wanasema nyani hao walifikaje Gibraltar? Wengine wanasema kwamba zamani za kale nyani hao waliishi sehemu nyingine za Ulaya na kwamba wale walio Gibraltar ndio tu wanaobaki. Wengine wanasema kwamba walipelekwa huko na wakoloni Waarabu au Waingereza. Hekaya zinasema kwamba nyani hao walivuka mlango-bahari mwembamba unaotenganisha Ulaya na Afrika kupitia njia ya chini ya ardhi ambayo sasa haitumiki. Vyovyote vile, sasa nyani hao ndio nyani pekee wanaoishi mwituni huko Ulaya.

Nyani wa Barbary huishi kwenye misitu ya msonobari iliyo upande wa juu wa Mwamba wa Gibraltar. Ingawa kuna nyani 100 hivi tu kwenye mwamba huo, wao ndio “wakaaji maarufu zaidi wa rasi hiyo,” kulingana na Shirika la Kimataifa la Kulinda Nyani. *

Kwa kuwa watalii milioni saba hutembelea Gibraltar kila mwaka, nyani hao watukutu hupata chakula kingi. Ingawa wao hutafuta mimea ya mwituni, wamekuwa stadi wa kuomba na nyakati nyingine hata kuiba chakula kutoka kwa watalii. Pia serikali ya huko huwapa nyani hao matunda na mboga.

Mbali na kula, nyani hao hutumia asilimia 20 ya siku yao wakisafishana. Nyani wa kiume na wa kike huwatunza watoto wao na kucheza nao. Wao huishi katika vikundi ambavyo hushirikiana kwa ukaribu, na nyakati nyingine hilo huwafanya wapigane. Ingawa nyani wakubwa huwatisha na kuwapigia kelele nyani wachanga ili kuwafukuza, wao pia wana tabia isiyo ya kawaida ya kugonganisha meno yao na inaonekana kwamba jambo hilo huwatuliza.

Huenda isijulikane jinsi nyani hao walivyofika Gibraltar; hata hivyo, nyani hao huwavutia watu kwenye Mwamba wa Gibraltar ulio kwenye mwingilio wa Bahari ya Mediterania. Kwa kweli wao ni sehemu muhimu ya Gibraltar.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Nyani wa Barbary ni tofauti kidogo na nyani wengine kwani hawana mikia.

^ fu. 5 Nyani wa Japani wanaoitwa macaque, ambao ni wa jamii moja na wa Barbary, huwavutia watalii kwenye chemchemi za maji moto huko Japani ambako wao hukusanyika wakati wa majira ya baridi kali.