Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuongoza Ndege Kunukulindaje?

Kuongoza Ndege Kunukulindaje?

Kuongoza Ndege Kunukulindaje?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FILIPINO

NDEGE inapokuwa angani, je, umewahi kujiuliza rubani hujuaje anakoenda? Huenda ukawa na wasiwasi unapofikiria makumi au hata mamia ya ndege zinazosafiri angani wakati uleule. Ni nini kinachozuia ndege hizo zisigongane?

Maswali kama hayo huwahangaisha wasafiri wengi. Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kwamba kusafiri kwa ndege ya abiria ni salama sana, * hata kuliko kusafiri kwa pikipiki au kwa gari. Mojawapo ya mambo muhimu yanayochangia usalama huo ni mifumo ya kuongoza ndege.

Kuelekeza Ndege kwa Usalama

Kapteni, au rubani mkuu, ana daraka la kuhakikisha ndege inaelekezwa kwa usalama. Hata hivyo, kuna pindi nyingi ambazo hawezi kuona au hata kutambua ikiwa kuna ndege nyingine zinazosafiri karibu naye. Kwa sababu hiyo, nchi nyingi zina mfumo wa kuongoza ndege. Wafanyakazi walio ardhini wanafuata hatua zote za safari ya ndege iliyo angani ikielekezwa na mifumo ya kuongoza ndege.

Samuel, ambaye amekuwa akiongoza ndege huko California kwa miaka 13 anasema hivi: “Mtaalamu wa kuongoza ndege ana wajibu muhimu wa kuhakikisha usalama wa safari za ndege. Jambo muhimu zaidi ni kuhakikisha kwamba ndege hazikaribiani.” Melba, msimamizi wa kituo cha kuongoza ndege anaongeza hivi: “Usalama ndilo jambo kuu na muhimu zaidi, lakini mbali na hilo tunasaidia ndege kutua na kupaa haraka na kwa utaratibu.” Hivyo, mbali na kuzuia ndege zisigongane, watu wanaoongoza ndege wanasaidia kuendesha ndege.

Yote hayo yanamaanisha kwamba rubani anapotimiza majukumu yake ndani ya chumba cha rubani, kuna macho na masikio mengi ardhini ambayo yanafuata ndege hiyo. Rubani hazungumzi kwa redio na waongozaji wa ndege walio katika viwanja vya ndege anakotoka na anakoenda tu bali pia anazungumza na waongozaji wengine njiani.

Kutambua vitu ambavyo rubani bado hajaviona ni jambo muhimu sana wakati huu ambapo ndege zina uwezo wa kusafiri kwa kasi sana. Wazia kwamba ndege mbili za abiria zinaelekea kugongana. Kufikia wakati ambapo marubani wa ndege hizo wanaonana ana kwa ana, huenda wakawa na sekunde chache tu za kuepuka kugongana! Ni jukumu la mwongozaji wa ndege kuzuia ndege hizo zisigongane. Muda mrefu kabla marubani hao hawajaonana, watakuwa wamepewa maagizo ili wasikaribiane.

Kuifuata Ndege Yako

Mitambo ya redio ya kurusha mawimbi kutoka ardhini hutoa ishara za kuongoza ndege. Rubani ana mitambo ambayo hupokea ishara hizo na kumwonyesha mahali hususa alipo. Kwa kuwa mitambo ya kurusha mawimbi inapatikana katika vituo hususa, ndege huruka kutoka kituo hadi kituo mpaka inapofika iendako. Kwa hakika, mitambo hiyo ya kuongoza ndege imetokeza njia hususa angani.

Waongozaji wa ndege wanafuata ndege kupitia njia hizo. Kabla ya kuanza safari, marubani wanapaswa kujaza daftari ya usafiri inayoonyesha njia wanayokusudia kufuata. Mwongozaji wa ndege ana nakala ya kikaratasi kilicho na habari zinazohitajiwa katika safari hususa ya ndege. Salvador Rafael, mwongozaji wa ndege, anaeleza jinsi habari hiyo inavyosaidia: “Kuna sehemu ambazo njia za angani zinapitana. Rubani anapofika hapo anapaswa kumjulisha mwongozaji wa ndege. Kisha mwongozaji huyo atatia alama katika kikaratasi chake.” Sasa mwongozaji huyo anaweza kuwazia njia ambayo ndege hiyo inafuata.

Ili apate ripoti hizo, mwongozaji ana kifaa kingine, yaani, redio. Anajua ilipo ndege, naye rubani anapokea maagizo ya kumsaidia kuepuka kukaribiana sana na ndege nyingine. Kwa kawaida waongozaji wa ndege na marubani wanatumia redio na mawimbi mbalimbali. Wanaposhindwa kuwasiliana wakitumia njia moja wanaweza kutumia nyingine.

Vipi safari za kimataifa ambazo wahusika wanatumia lugha tofauti-tofauti? Ili kuepuka hatari zinazoweza kutokana na matatizo ya mawasiliano, Shirika la Kimataifa la Safari za Ndege za Abiria lilichagua Kiingereza kiwe lugha ya mawasiliano katika safari zote za ndege. Pia, kwa kuwa maneno, herufi, na nambari fulani zinafanana zinapotamkwa kwenye redio, waongozaji wa ndege wanafundishwa kutumia taarifa na matamshi rasmi wanapowapa marubani maagizo. Ili kuboresha kiwango cha usalama, marubani wanaulizwa kurudia maagizo fulani ya waongozaji wa ndege.

Rada ni chombo kingine ambacho waongozaji wa ndege hutumia. Mawimbi ya redio yanagonga ndege halafu yananaswa na antena za rada. Kisha ndege zinaonekana kama vitu, au shabaha katika kiwambo cha rada cha mwongozaji. Ndege nyingi zina kifaa kinachoitwa transponder ambacho hutuma ishara ya utambulisho kwenye rada. Ishara hiyo inapounganishwa na habari katika kompyuta, ndege na pia habari zote kuhusu namba, mwendo, mwinuko, na aina ya ndege huonekana kwenye kiwambo cha rada.

Mwongozaji wa ndege akiona uhitaji wa kuzuia ndege zisigongane, anaweza kufanya mojawapo ya mambo yafuatayo. Anaweza kumwagiza rubani abadili (1) mwelekeo, au anaweza kumwagiza abadili (2) mwendo, kwa mfano ikiwa ndege moja inaipita nyingine. Njia anayotumia zaidi kuzuia ndege zisikaribiane sana ni kuwaagiza wabadili (3) mwinuko.

Ili kuongeza usalama, mifumo mingi inaweza kumtahadharisha mwongozaji hali hatari inapotokea. Kwa mfano, ishara zinazoonekana na pia ving’ora huanza kulia mfumo huo unapotambua kwamba ndege mbili zinaelekea kukaribiana sana. King’ora kingine hulia inapoonekana kwamba ndege fulani inakaribia sana ardhi.

Usalama Wako Ndio Shabaha Yao

Tayari mipango ya kuboresha mifumo ya kuongoza ndege inaendelea. Mara nyingi mifumo iliyo ardhini ya kuongoza ndege hutaka ndege zifuate njia hususa na ziwe umbali hususa kutoka ardhini. Hilo hupoteza nafasi kubwa angani na hulazimu ndege zifuate njia ndefu sana. Wakati ujao, ndege zitafuata zaidi mifumo inayoongozwa na satelaiti kama vile Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Satelaiti (GPS), ambayo haitalazimu ndege kufuata njia hususa na itarahisisha zaidi kuongoza ndege zinazosafiri kuvuka bahari.

Kama vile mazungumzo yetu mafupi kuhusu kuongoza ndege yameonyesha, rubani siye mtu pekee anayejua ilipo ndege fulani wakati wowote ule. Kwa kweli, watu kadhaa ardhini wanaifuata ndege inaposafiri angani. Mfumo wa kuongoza ndege umebuniwa ili kupunguza hatari na kuzidisha usalama. Haishangazi kwamba kuna aksidenti chache sana za ndege za abiria.

Hivyo huna sababu ya kuwa na wasiwasi ukisafiri kwa ndege. Wakati ujao ukisafiri mbali kwa ndege, kumbuka kwamba macho na masikio ya waongozaji wa ndege yamekazwa ili kuhakikisha usalama wako. Keti, tulia, na ufurahie safari yako ya ndege!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Katika mwaka mmoja hivi karibuni nchini Marekani, ndege zilisafiri kilomita 11,000,000,000 hivi, na kwa wastani kulikuwa na aksidenti moja katika kila kipindi cha saa 334,448 za safari hizo.

[Mchoro katika ukurasa wa 14, 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KUFUATA NDEGE

Mfumo wa kuongoza ndege

Mfumo wa rada

Mitambo ya redio ya kurusha mawimbi kutoka ardhini

Radio

Antena ya rada

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mnara wa kuongoza ndege

[Picha katika ukurasa wa 15]

Waongozaji wa ndege

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kituo cha kuongoza ndege

[Picha ya Hisani katika ukurasa wa 15]

Tower and controllers: NASA Ames Research Center; control center: U. S. Federal Aviation Administration