Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kusafiri kwa Mashua Huko Kerala

Kusafiri kwa Mashua Huko Kerala

Kusafiri kwa Mashua Huko Kerala

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI INDIA

WAZIA ukiabiri kupitia delta za mito 44 ukiwa ndani ya mashua-nyumba maridadi sana. Unaweza kufanya hivyo ukisafiri kwenye eneo lenye maji lenye urefu wa kilomita 900 katika jimbo la Kerala, kusini magharibi mwa India. Hiyo ni safari yenye kupendeza na ya pekee sana. Huku ukisafiri taratibu kwa mashua, lazima utavutiwa na nyangwa zenye minazi, mashamba ya mpunga yenye rutuba, maziwa ya asili, na mifereji iliyotengenezwa na watu. Naam, inaelekea kwamba kwa sababu ya umaridadi wa eneo hilo, kichapo National Geographic Traveler kiliorodhesha Kerala kuwa “mojawapo ya maeneo 50 bora ambayo ‘mtu anapaswa kutembelea maishani.’”

Pia, hatupaswi kuwasahau watu wanaoishi kwenye fuo za mifereji mingi ya eneo hilo. Wanakumbuka pindi ambapo hapakuwa na watalii au hoteli za kifahari katika ujirani wao. Hata hivyo, maisha yao hayajabadilika sana. Ingawa baadhi yao sasa wameajiriwa katika hoteli hizo mpya au wanafanya kazi nyingine zinazohusiana na utalii, kwa kadiri kubwa utamaduni na maisha yao ya kila siku hayajabadilika. Wanashughulikia mashamba yao ya mpunga na minazi, na vilevile wanapata chakula na mapato kutokana na uvuvi na uuzaji wa samaki.

Kuvua Katika Eneo Hilo

Uvuvi ni sehemu ya maisha katika eneo hilo. Jambo moja ambalo huenda huwezi kamwe kujionea mahali pengine popote ni wanawake wakivua samaki wanaoitwa karimeen kwa mikono. Samaki hao wanaopatikana tu huko Kerala, wanapendwa sana na Wahindi na wageni. Wanapotafuta samaki hao, wanawake hutembea kwa miguu ndani ya maji huku sufuria zao zikielea nyuma yao. Samaki wanapowaona wanawake hao wakikaribia, wanapiga mbizi na kuficha vichwa vyao kwenye matope. Ili samaki wasiwashinde akili, wanawake hao hupapasa-papasa kwenye matope hayo kwa miguu yao ambayo imezoea kazi hiyo na kuwapata. Kisha, wanatumbukiza mikono yao upesi ndani ya maji na kuwashika samaki hao wasiotazamia kisha wanawaingiza ndani ya sufuria. Wakiisha kushika samaki wa kutosha, wanarudi ufuoni ambako wanunuzi wanawasubiri kwa hamu. Samaki wakubwa zaidi na wanaouzwa kwa bei ya juu zaidi wananunuliwa na hoteli za kifahari ambako matajiri wanafurahia kuwala, huku samaki wadogo wakiwa mlo mtamu kwa ajili ya watu wenye mapato ya chini.

Nyavu za Wachina

Kwa kawaida nyavu maridadi za Wachina huonekana zikitanda fuo za eneo hilo. Nyavu hizo pia huwavutia sana watalii.

Inaaminika kwamba mwanzoni wafanyabiashara Wachina waliotoka Kublai Khan walileta nyavu hizo huko Cochin (sasa panaitwa Kochi) kabla ya mwaka wa 1400. Nyavu hizo zilizovutwa kwa mikono zilitumiwa kwanza na Wachina na baadaye na walowezi Wareno. Leo wavuvi wengi Wahindi wanazitumia kujiruzuku, na pia zinawaandalia chakula watu wasiohesabika, kama tu zilivyofanya miaka zaidi ya 600 iliyopita. Inashangaza kwamba samaki wanaoshikwa na wavu mmoja wanaweza kulisha kijiji kizima. Katika vitabu vya picha vya safari za utalii za watalii wengi kuna picha za nyavu hizo wakati wa kushuka kwa jua.

Si nyavu za Wachina tu zinazowavutia watalii watembelee eneo hilo. Shughuli za majini kama vile mashindano ya mashua-nyoka huwavutia maelfu kila mwaka.

Mashindano ya Mashua

Mashua-nyoka ni mitumbwi mirefu myembamba. Matezi yake yana umbo la kichwa cha swila na ndiyo sababu zinaitwa mashua-nyoka. Zamani, wafalme waliopambana katika eneo hilo walitumia mashua hizo katika vita walivyopigana baada ya mavuno. Hatimaye vita vilipokoma, uhitaji wa mashua hizo ulipungua. Mashua hizo kubwa ziliabiri tu wakati wa sherehe za hekalu. Kwa mbwembwe, mabaharia wanaingia, nayo mashua inapambwa na kutumiwa kuonyeshea utamaduni wa eneo hilo. Siku za sherehe, mashindano ya mashua yalifanywa kwa heshima ya wageni waheshimiwa waliohudhuria. Utamaduni huo, ulioanza maelfu ya miaka iliyopita unaendelea kusitawi.

Ni jambo la kawaida kwa mashua 20 hivi za aina hiyo kushiriki mashindano hayo, kila moja ikiendeshwa na wanaume kati ya 100 na 150. Zaidi ya wanaume 100 walio na makasia madogo wanaketi katika safu mbili ndani ya kila mashua. Wanaume wanne wanaoshikilia usukani wana makasia marefu zaidi nao wanasimama kwenye tezi ili kuielekeza mashua. Wanaume wengine wawili wanasimama katikati ya mashua, wakigongagonga ubao fulani ili kuwaelekeza wapiga makasia. Mbali na sauti ya ubao huo kuna wanaume wengine sita hivi wanaowachochea. Wanaume hao wanapiga makofi, mbinja, makelele, na kuimba nyimbo za pekee za mabaharia ili kuwahimiza wadumishe mwendo. Kisha, baada ya kupiga makasia kwa muda fulani wakifuatana na mipigo ya ule ubao, wanaume hao wanayapiga kwa nguvu zaidi na kuongeza mwendo kuelekea mwisho wa mashindano.

Katika 1952, waziri mkuu wa kwanza wa India, Jawaharlal Nehru, alitembelea Alleppey, mji muhimu katika eneo hilo, naye alipendezwa sana na mashindano ya mashua aliyohudhuria huko. Kwa kweli alipendezwa sana hivi kwamba akapuuza walinzi wake na kuruka ndani ya mashua iliyoshinda, huku akiimba na kupiga makofi pamoja na wapiga makasia. Aliporudi Delhi, alituma zawadi, umbo la fedha la mashua-nyoka, ambayo ilikuwa na sahihi yake na maneno haya: “Kwa washindi wa mashindano ya mashua ambayo ni sehemu ya pekee katika maisha ya jamii.” Mashua hiyo ya fedha inatumiwa kama tuzo wakati wa Mashindano ya Tuzo ya Nehru yanayofanywa kila mwaka. Watu elfu mia moja hivi huja kushuhudia mashindano kama hayo kila mwaka. Pindi hizo, kunakuwa na shughuli nyingi katika maji ya eneo hilo ambayo kwa kawaida yametulia.

Hoteli za Starehe Zinazoelea na Kuabiri

Mashua-nyoka sivyo vyombo pekee vya majini katika eneo hilo ambavyo vinavutia watalii. Vyombo vingine vinavyozidi kupendwa na wengi ni mashua za mchele—vyombo vya muundo wa kale ambavyo vimefanyiwa marekebisho na kuwa mashua-nyumba.

Ijapokuwa mashua nyingi zinazotumiwa na watalii ni mpya, bado kuna mashua za mchele zilizoundwa miaka zaidi ya mia moja iliyopita ambazo zimerekebishwa kwa ajali ya utalii. Mwanzoni ziliitwa kettuvallam, yaani, “mashua zenye mafundo.” Mashua nzima iliundwa kwa mbao zilizounganishwa kwa kamba zenye mafundo, bila kutumia hata msumari mmoja. Mashua hizo zilitumiwa kusafirisha mchele na bidhaa nyingine kijiji kwa kijiji na kupeleka vikolezo katika maeneo ya mbali. Vyombo vipya vya usafiri vilipotokea, mashua hizo ziliacha kutumika sana. Lakini mfanyabiashara mmoja akapata wazo la kuzirekebisha ziwe mashua-nyumba kwa ajili ya biashara ya utalii. Zikiwa na roshani, vyumba vya kulala vya kifahari vilivyo na bafu, na sebule yenye fanicha maridadi, mashua hizo zinaweza kuitwa hoteli zinazoelea. Kuna wafanyakazi walio tayari kuipeleka mashua kokote unakotaka na kukupikia chochote unachotaka.

Jioni inapofika, mashua zinatia nanga karibu na ufuo, lakini wale wanaopenda amani na faragha wanatia nanga ziwani. Mtu akiwa ziwani anaweza kufurahia utulivu wa eneo hilo, ingawa mara kwa mara utulivu huo utakatizwa na samaki waliokosa usingizi!

Hata hivyo, bado kuna shughuli nyingine zinazoendelea huko Kerala. “Wavuvi wa watu” wako macho na wanafanya kazi kwa bidii katika eneo hilo.

‘Kuvua Watu’ Huko Kerala

Maneno “wavuvi wa watu” yanatokana na maneno ambayo Yesu aliwaambia wavuvi fulani waliokuja kuwa wanafunzi wake. Aliwaambia hivi: “Nifuateni, nami nitawafanya ninyi kuwa wavuvi wa watu.” Yesu alikuwa akizungumzia kazi ya kuwasaidia watu kuwa wanafunzi wake. (Mathayo 4:18, 19; 28:19, 20) Kazi hiyo inatimizwa na Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote kutia ndani maeneo yanayozunguka Kerala.

Kuna makutaniko 132 ya Mashahidi wa Yehova huko Kerala, kutia ndani makutaniko 13 kuzunguka eneo lenye maji. Washiriki wengi wa kutaniko ni wavuvi pia. Mmoja wao alipokuwa ameenda kuvua, alizungumza na mvuvi mwenzake kuhusu Ufalme wa Mungu. Muda si muda, mtu huyo aliona tofauti kati ya mafundisho ya dini yake na yale ya Biblia. Mke wake na watoto wao wanne walipendezwa pia. Walianza kujifunza Biblia. Walifanya maendeleo haraka, na wanne kati ya watu hao sita tayari wamebatizwa. Watoto wawili waliobaki wanafanya maendeleo ili wabatizwe.

Washiriki wa kutaniko moja la Mashahidi wa Yehova walisafiri kwa mashua ili kuhubiri katika kisiwa fulani kidogo. Kwa sababu mashua hazisafiri kwa ukawaida kwenda na kutoka kwenye kisiwa hicho, wenyeji walikiita kisiwa hicho kadamakudi, yaani, “utanaswa ukiingia.” Wakiwa huko Mashahidi hao walikutana na Johny na mke wake, Rani. Ingawa walikuwa Wakatoliki tangu kuzaliwa, walishirikiana na kituo fulani cha kutafakari na wakakipa pesa zote walizoweza. Johny alipendezwa sana na ujumbe wa Biblia, na akaanza kujifunza Biblia. Alianza kuwaambia wengine kuhusu imani yake mpya. Kweli ya Biblia ilimwezesha kuacha kuvuta sigara na kulewa!

Kazi ambayo Johny alikuwa akifanya haikupatana na Maandiko, hivyo akaiacha. Mwanzoni hilo lililetea familia yake matatizo ya kiuchumi. Hata hivyo, muda si muda, Johny alianza kuvua kaa na kuwauza na hivyo kuiruzuku familia yake. Alibatizwa Septemba 2006, na mke na watoto wake wawili wakabatizwa mwaka mmoja baadaye. Tarajio la kuishi milele katika dunia paradiso limebadili kabisa mtazamo wao kuhusu maisha.—Zaburi 97:1; 1 Yohana 2:17.

Kwa kweli, inafurahisha sana kutembelea eneo la Kerala. Haifurahishi kwa sababu ya nyavu za Wachina, mashua-nyoka, na mashua-nyumba tu, bali pia kwa sababu ya “wavuvi wa watu,” Mashahidi waaminifu wa Yehova wanaoishi huko.

[Picha katika ukurasa wa 22, 23]

 

INDIA

KERALA

[Picha katika ukurasa wa 23]

Uvuvi ni sehemu ya maisha huko Kerala

[Hisani]

Top photo: Salim Pushpanath

[Picha katika ukurasa wa 23]

Wanawake wakivua samaki kwa mikono

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mashindano ya mashua-nyoka

[Picha katika ukurasa wa 24]

“Kettuvallam”

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Mashua-nyumba

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Johny na mke wake, Rani

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Salim Pushpanath