Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Simbamarara wa Siberia—Je, Ataokoka?

Simbamarara wa Siberia—Je, Ataokoka?

Simbamarara wa Siberia—Je, Ataokoka?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI URUSI

Katika siku nyangavu ya majira ya baridi kali huko mashariki kabisa mwa Urusi, kwa ghafula paka mkubwa anapita mbio kwenye theluji inayong’aa huku akifukuzwa na helikopta. Mlenga-shabaha aliye na bunduki anaegemea nje ya helikopta, simbamarara anaruka juu ya mti na kunguruma. Mtu huyo anafyatua risasi. Helikopta inatua na watu wanashuka na kumkaribia kwa tahadhari mnyama huyo aliyepigwa.

JE, WAO ni wawindaji haramu? Hapana, ni watafiti wanaotumia vishale vyenye dawa ya kupoteza fahamu. Wamekuja kuchunguza mnyama anayekabili hatari kubwa zaidi ya kutoweka, yaani, simbamarara wa Siberia asiyepatikana kwa urahisi. *

Kiumbe wa Kifahari

Wakati mmoja, simbamarara wa Siberia aliishi Korea, kaskazini mwa China, Mongolia, na sehemu za magharibi kabisa kama Ziwa Baikal, huko Urusi. Hata hivyo, katika muda wa karne moja hivi, idadi yao imepungua. Sasa wamekimbilia usalama katika safu ya milima iliyo mbali kaskazini ya Vladivostok, Urusi, kando ya Bahari ya Japani.

Simbamarara huwatambua wenzao kwa harufu, na hilo huwawezesha wa kiume kuwapata wa kike wakati wa kujamiiana. Simbamarara huzaa watoto wawili au watatu wakati mmoja. Watoto hao huzaliwa wakiwa vipofu, wakigaagaa. Tofauti na watoto wa paka, watoto wa simbamarara hawakoromi. Wao hunguruma kwa sauti ndogo, hunyonya kwa miezi tano au sita, kisha wao huanza kula nyama. Mwanzoni, wao huwinda pamoja na mama yao lakini hawawezi kuwinda peke yao mpaka wanapofikia umri wa miezi 18. Simbamarara wachanga wanaweza kuishi na mama yao kwa miaka miwili hivi. Kisha wanahama na kutafuta eneo lao wenyewe.

Msituni, simbamarara wengine ni wakubwa sana. Simbamarara-dume anaweza kuwa na uzito wa kilogramu 270 hivi, na urefu wa zaidi ya mita 3, kutia ndani mkia. Simbamarara wanaweza kuhimili majira ya baridi kali na theluji. Wana manyoya mengi, na miguu yao mikubwa imefunikwa kwa manyoya ambayo huwasaidia kutembea juu ya theluji.

Simbamarara wa Siberia wana milia myeusi kwenye manyoya yao ya rangi ya machungwa. Kila simbamarara ana milia tofauti, na hilo huwatofautisha kama tu alama za vidole zinavyowatofautisha wanadamu. Kwa sababu ya milia na rangi yake, simbamarara aliyetulia msituni hawezi kuonekana kwa urahisi. Lakini akitokea mahali pasipo na miti katika majira ya baridi kali, anaonekana waziwazi kwenye theluji nyeupe. Hilo hufanya waonekane kwa urahisi na wawindaji pekee wa simbamarara, yaani, wanadamu.

Tisho la Kutoweka

Simbamarara hula wanyama wakubwa kama vile mbawala, kongoni, na nguruwe-mwitu. Lakini idadi ya mawindo yake imepungua katika misitu ya Siberia mashariki. Msitu wenye ukubwa wa kilomita 1,000 za mraba unaweza kuwa na wanyama wanaotosha kuwalisha simbamarara wanne au watano tu. Kwa hiyo, ili simbamarara waendelee kuwapo msituni, lazima wawe na eneo la kutosha.

Kwa miaka mingi, misitu mikubwa na isiyofikika kwa urahisi ya Siberia imewafaa simbamarara hao wakubwa. Wanadamu, ambao ndio tisho lao pekee hawakufika huko mara nyingi. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, kampuni za kukata miti kutoka nchi nyingine zimekata miti mingi ya misitu hiyo.

Kadiri miti inavyotoweka, ndivyo mbawala, kongoni, nguruwe-mwitu, na simbamarara wa Siberia wanavyotoweka. Ili kupunguza hilo, serikali ya Urusi ina maeneo makubwa ya kuhifadhi wanyama mwitu kama vile Mbuga ya Asili ya Sikhote Alin. Lakini simbamarara wanapotoka katika maeneo hayo, wanahatarishwa na wawindaji haramu wanaowauzia watu bidhaa za kumbukumbu. Meno, kucha, mifupa, na ngozi ya simbamarara na hata ya watoto wake huuzwa bei ghali sana.

Kumwokoa Simbamarara

Jitihada nyingi zinafanywa ili kumwokoa simbamarara wa Siberia, na wenyeji wako katika mstari wa mbele. Hivyo, idadi ya simbamarara wa Siberia imeongezeka kidogo. Hesabu iliyochukuliwa mwaka wa 2005 inaonyesha kwamba kuna simbamarara kati ya 430 na 540 huko Siberia.

Kwa upande mwingine, simbamarara wa Siberia walio katika hifadhi za wanyama huzaana haraka na wana afya nzuri. Kuna zaidi ya simbamarara 500 katika hifadhi za wanyama ulimwenguni pote. Basi, kwa nini wanyama hao hawaachiliwi huru ili kuongeza idadi ya wale walio msituni? Wanasayansi wanasita kufanya hivyo. “Hakuna haja ya kumwachilia mnyama aende msituni,” akasema mtafiti mmoja, “usipohakikishiwa kwamba atakuwa salama.”

Viumbe vyote hai, kutia ndani simbamarara wakubwa, wanaonyesha hekima na nguvu za Mungu, naye huwajali na kuwatunza. (Zaburi 104:10, 11, 21, 22) Watu wengi wanaothamini sana kazi za Muumba wana hakika kwamba kutakuwa na wakati ambapo simbamarara wa Siberia hawatakabili tena hatari ya kutoweka.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Nyakati nyingine simbamarara wa Siberia anaitwa simbamarara wa Amur, kwa kuwa wanyama hawa sasa wanapatikana hasa katika bonde la Mto Amur, mashariki ya mbali ya Urusi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

PAKA MKUBWA ZAIDI

Katika jamii ya paka, simbamarara wa Siberia amepitwa kwa ukubwa na liger, ambaye ni mzao wa simba-dume na simbamarara-jike. Wanyama hao wanaweza kukua na kufikia urefu wa zaidi ya mita 3 na uzito wa zaidi ya kilogramu 500. Liger huzalishwa kwenye hifadhi za wanyama, na ni nadra sana kuwapata msituni.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Top: © photodisc/age fotostock; bottom: Hobbs, courtesy Sierra Safari Zoo, Reno, NV