Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Watu Wengi Wanaogopa Nini Hasa?

Watu Wengi Wanaogopa Nini Hasa?

Watu Wengi Wanaogopa Nini Hasa?

“Si wanadini tu wanaoamini kwamba karibuni wanadamu watakabili msiba mkubwa.”—STEPHEN O’LEARY, PROFESA MSAIDIZI WA CHUO KIKUU CHA SOUTHERN CALIFORNIA. *

JE, UNAKUBALIANA na maoni hayo? Sehemu zifuatazo zinaonyesha baadhi ya sababu zinazofanya watu waogope mambo yatakayotukia wakati ujao. Pia, zinaonyesha kwa nini unaweza kuwa na hakika kwamba uhai hautakoma duniani. Ijapokuwa habari zinazofuata ni zenye kushtua, kuna sababu nzuri za kutarajia mema.

Bado kuna uwezekano mkubwa wa vita vya nyuklia kuzuka. Mwaka wa 2007, wanasayansi walionya katika gazeti lao la Bulletin of the Atomic Scientists kwamba mwaka huo ulimwengu ulikuwa ukikabili maamuzi hatari kama yale uliokabili wakati ambapo mabomu ya kwanza ya atomiki yaliangushwa jijini Hiroshima na Nagasaki. Kwa nini kuna wasiwasi huo? Gazeti la Bulletin lilisema kwamba katika mwaka wa 2007, bado kulikuwa na silaha 27,000 hivi za nyuklia, na 2,000 kati ya hizo “zilikuwa zimewekwa tayari, na zingeweza kutumiwa wakati wowote.” Hata kama silaha chache tu kati ya hizo zingelipuliwa, bado zingesababisha uharibifu mkubwa sana!

Je, uwezekano wa kuzuka kwa vita vya nyuklia umepungua tangu wakati huo? Kitabu cha Mwaka cha SIPRI cha 2009 (cha Kiingereza) * * kinasema kwamba nchi tano zenye silaha nyingi sana za nyuklia, yaani, China, Marekani, Ufaransa, Uingereza, na Urusi, “zinaendelea kuweka silaha za nyuklia ziwe tayari kutumiwa, au zinakusudia kufanya hivyo.” Lakini kitabu hicho cha mwaka kinasema kwamba si nchi hizo tu ambazo zina silaha za nyuklia. Watafiti wanakadiria kwamba kila moja kati ya nchi ya India, Pakistan, na Israeli, ina mabomu 60 hadi 80 ya nyuklia. Wanasema pia kwamba duniani kote kuna silaha 8,392 za nyuklia ambazo ziko tayari kutumiwa!

Huenda mabadiliko ya hali ya hewa yakaleta msiba. Gazeti la wanasayansi linalotajwa hapo juu linasema kwamba “madhara ambayo huenda yakasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, yanaweza kuwa mabaya kama tu madhara ambayo silaha za nyuklia zinaweza kusababisha.” Wanasayansi wanaoheshimiwa, kama vile Stephen Hawking ambaye ni profesa aliyestaafu wa hisabati kwenye Chuo Kikuu cha Cambridge, na Bwana Martin Rees, Mkuu wa Chuo cha Trinity kwenye Chuo Kikuu cha Cambridge, wanatoa maonyo kama hayo yenye kutia hofu. Wanaamini kwamba huenda maisha duniani yakabadilika kabisa au hata ustaarabu ukakoma kwa sababu wanadamu wametumia tekinolojia bila kufikiria matokeo ya baadaye, na utendaji wao umesababisha mabadiliko ya mazingira.

Utabiri kuhusu siku ya maangamizi unawatia watu wengi hofu. Chapa maneno “mwisho wa ulimwengu” kwa Kiingereza, na mwaka wa “2012” kwenye kituo fulani cha Intaneti, na utapata habari nyingi sana kuhusu makisio ya watu wanaoamini kwamba mwisho utakuja mwaka huo. Kwa nini? Mwaka wa 2012 umekadiriwa kuwa mwaka wa mwisho katika kalenda fulani ya kale ya Wamaya. Watu wengi wanahofu kwamba mwaka huo ustaarabu uliopo utakwisha kwa njia moja au nyingine.

Wanadini wengi wanaamini kwamba Biblia inafundisha kuwa dunia halisi itaharibiwa. Wengine wanaamini kwamba watu wote waaminifu wataenda mbinguni, na wanadamu wengine wataachwa wakiteseka kwenye dunia yenye msukosuko au kutupwa motoni.

Je, Biblia inasema kwamba hali duniani zitaharibika kabisa au dunia yenyewe itaharibiwa? Mtume Yohana alionya: “Msiamini kila neno lililoongozwa na roho, lakini yajaribuni maneno yaliyoongozwa na roho ili kuona kama yanatokana na Mungu.” (1 Yohana 4:1) Badala ya kuamini tu maneno ya watu wengine, fungua Biblia yako na ujisomee mambo ambayo inasema kuhusu mwisho wa ulimwengu. Huenda ukashangaa unapoona mambo inayofundisha.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Maneno haya yamenukuliwa kutoka katika makala “Misiba ya Hivi Karibuni Inawachochea Watu Watabiri Siku ya Maangamizi.” Makala hii ilipatikana kwenye kituo cha Intaneti cha MSNBC, Oktoba 19, 2005 (19/10/2005).

^ fu. 5 SIPRI ni kifupisho cha Taasisi ya Utafiti Kuhusu Amani ya Kimataifa ya Stockholm.

^ fu. 5 Ripoti hiyo katika Kitabu cha Mwaka cha SIPRI cha 2009 iliandikwa na Shannon N. Kile, mtafiti mkuu na msimamizi wa mradi wa silaha za nyuklia wa Kitengo cha SIPRI cha Kudhibiti na Kuzuia Kuenea kwa Silaha; Vitaly Fedchenko, mtafiti wa Kitengo cha Kudhibiti na Kuzuia Kuenea kwa Silaha; na Hans M. Kristensen, mkurugenzi wa mradi wa kutoa habari za mambo ya nyuklia wa Shirika la Wanasayansi wa Marekani.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]

Mushroom cloud: U.S. National Archives photo; hurricane photos: WHO/League of Red Cross and U.S. National Archives photo