Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maisha Nyakati za Biblia—Wanamuziki na Vyombo Vyao vya Muziki

Maisha Nyakati za Biblia—Wanamuziki na Vyombo Vyao vya Muziki

Maisha Nyakati za Biblia​—Wanamuziki na Vyombo Vyao vya Muziki

“Msifuni [Mungu] kwa kupiga baragumu. Msifuni kwa kinanda na kinubi. Msifuni kwa matari na kwa dansi ya mzunguko. Msifuni kwa vinanda na zumari. Msifuni kwa matoazi yenye sauti tamu. Msifuni kwa matoazi ya kugonganishwa.”​—ZABURI 150:3-5.

KWA muda mrefu, muziki na wanamuziki wametimiza fungu muhimu sana katika ibada ya Yehova Mungu. Kwa mfano, wakati Yehova alipowakomboa Waisraeli kimuujiza kupitia Bahari Nyekundu, Miriamu, dada ya Musa aliongoza wanawake kuimba wimbo wa ushindi na kucheza dansi. Wacheza dansi hao walikuwa wakipiga matari. Tukio hilo linaonyesha jinsi muziki ulivyokuwa muhimu kwa Waisraeli. Walikuwa tu wamelikimbia jeshi la Wamisri, hata hivyo, idadi kubwa ya wanawake walikuwa wamebeba vyombo vyao vya muziki, tayari kuvitumia. (Kutoka 15:20) Baadaye, Mfalme Daudi alifanya mpango ili maelfu ya wanamuziki wacheze vyombo vyao vya muziki kama sehemu ya ibada kwenye hema la kukutania. Baadaye, mpango huo uliendelea katika hekalu ambalo lilijengwa na mwana wake Sulemani.​—1 Mambo ya Nyakati 23:5.

Vyombo hivyo vilikuwa vimetengenezwa na nini? Vilikuwa na muundo gani? Vilitokeza sauti za aina gani? Na vilitumiwa wakati gani?

Aina za Vyombo vya Muziki

Vyombo vya muziki vinavyotajwa katika Biblia vilitengenezwa kwa chuma, mifupa, mbao zenye thamani, na ngozi ya mnyama iliyovutwa. Vyombo vingine vilifunikwa kwa pembe za ndovu. Nyuzi zilitengenezwa kwa matumbo ya wanyama au nyuzi-nyuzi za mimea. Ingawa leo ni vigumu kupata vyombo hivyo vya kale, picha zake zinapatikana.

Vyombo vilivyotumiwa nyakati za Biblia vinaweza kugawanywa katika vikundi vitatu: vinanda, kama vile kinubi, zeze (1), na udi (2); vyombo vya kupulizwa, kama vile baragumu (3), tarumbeta (4), filimbi, au zumari, iliyopendwa sana (5); vyombo vilivyogongwa au kutikiswa ili kutoa sauti, kama vile tari (6), tasa (7), matoazi (8), na kengele (9). Wanamuziki walitumia vyombo hivyo walipokariri mashairi, kuimba nyimbo, au kucheza dansi. (1 Samweli 18:6, 7) Jambo la muhimu zaidi ni kwamba walivitumia katika ibada ya Mungu aliyewabariki kwa kuwapa zawadi ya muziki. (1 Mambo ya Nyakati 15:16) Chunguza kwa makini zaidi aina hizo za vyombo vya muziki.

Vinanda Kinubi na zeze vilikuwa vyombo vyepesi vinavyoweza kubebwa. Vilikuwa na nyuzi zilizokuwa zimekazwa juu ya kiunzi cha mbao. Daudi alicheza kinanda ili kutuliza nafsi ya Mfalme Sauli mwenye kuteseka. (1 Samweli 16:23) Vyombo hivyo vilitumiwa na wanamuziki wakati wa kuwekwa wakfu kwa hekalu la Sulemani na kwenye pindi nyingine zenye furaha, kama vile sherehe.​—2 Mambo ya Nyakati 5:12; 9:11.

Chombo kilichoitwa udi kilifanana na kinubi, lakini kwa kawaida kilikuwa na umbo tofauti. Kilikuwa na nyuzi chache zilizokazwa juu ya kiunzi kilichounganishwa na ubao wa kuvumisha sauti. Huenda nyuzi hizo zilitokeza muziki mtamu kama ule wa gitaa. Nyuzi zake zilitengenezwa kwa kutumia matumbo ya wanyama au nyuzi-nyuzi za mimea.

Vyombo vya Kupulizwa Vyombo hivi vinatajwa mara nyingi katika Biblia. Kati ya vyombo hivyo, baragumu ya Wayahudi inayoitwa shofar ndiyo ya kale zaidi. Baragumu hiyo ilitengenezwa kwa kutoa sehemu ya ndani ya pembe ya kondoo-dume na ilitoa mlio mkali sana. Waisraeli walitumia baragumu kukusanya vikosi kwa ajili ya vita na pia kuagiza taifa lichukue hatua fulani.​—Waamuzi 3:27; 7:22.

Aina nyingine ya chombo cha muziki cha kupulizwa ni tarumbeta iliyotengenezwa kwa chuma. Hati moja iliyopatikana miongoni mwa vile Vitabu vya Kukunjwa vya Bahari ya Chumvi inaonyesha kwamba wanamuziki walitokeza sauti nyingi ajabu wakitumia tarumbeta hizo. Yehova alimwagiza Musa atengeneze tarumbeta mbili za fedha ili zitumiwe kwenye maskani, au hema la kukutania. (Hesabu 10:2-7) Baadaye, wakati hekalu la Sulemani lilipokuwa likizinduliwa, tarumbeta 120 zilitoa sauti kubwa kwenye sherehe hiyo. (2 Mambo ya Nyakati 5:12, 13) Wasanii walitengeneza tarumbeta zenye urefu tofauti-tofauti. Baadhi ya tarumbeta hizo zilikuwa na urefu wa sentimita 91, kuanzia sehemu ya kupulizia hadi sehemu ya mbele yenye umbo la kengele.

Chombo cha kupulizwa kilichopendwa sana na Waisraeli ni filimbi. Sauti yake tamu ilichochea furaha miongoni mwa watu waliohudhuria sherehe, arusi, na karamu za kifamilia. (1 Wafalme 1:40; Isaya 30:29) Sauti ya filimbi pia ilisikika kwenye mazishi, ambapo wanamuziki waliimba nyimbo walipokuwa wakiomboleza (ona ukurasa wa 14).​—Mathayo 9:23.

Vyombo vya Muziki Vilivyogongwa au Kutikiswa ili Kutoa Sauti Kwenye sherehe, Waisraeli walitumia aina mbalimbali za vyombo hivyo. Mdundo wake ulichochea sana hisia. Chombo kinachoitwa tari, kilitengenezwa kwa ngozi ya mnyama iliyovutwa juu ya kiunzi cha mbao chenye umbo la mviringo. Chombo hicho kilitoa sauti kama ya ngoma mwanamuziki au mcheza dansi alipokipiga kwa mkono wake. Mwanamuziki alipokitikisa, kengele ambazo zilikuwa zimeunganishwa na tari hilo zilitoa sauti yenye kupendeza.

Tasa ni chombo kingine kilichotoa sauti kilipogongwa. Chombo hicho chenye umbo la yai kilitengenezwa kwa chuma, kikiwa na sehemu ya kushikilia. Pia kilikuwa na vipande vya chuma ambavyo vilishikilia visahani vya chuma vilivyocheza-cheza. Kilipotikiswa haraka-haraka mbele na nyuma, chombo hicho kilitoa sauti yenye kupendeza.

Matoazi ya shaba yalikuwa na sauti kali hata zaidi. Matoazi yalikuwa visahani vyenye ukubwa tofauti. Matoazi makubwa yaligonganishwa pamoja kwa nguvu. Lakini matoazi madogo yenye sauti tamu yalichezwa kwa kutumia vidole viwili. Matoazi hayo—makubwa na madogo—yalitoa sauti tofauti.—Zaburi 150:5.

Kufuata Kielelezo

Leo, Mashahidi wa Yehova wanaanza na kumalizia mikutano yao ya ibada kwa muziki na nyimbo. Kwenye makusanyiko yao, wao husikiliza muziki uliorekodiwa na kikundi cha wanamuziki ambao hutumia vinanda, vyombo vinavyogongwa au kutikiswa, na vyombo vya kupulizwa vya kisasa.

Kwa kucheza muziki na kuimba katika ibada yao, Mashahidi hufuata kielelezo kilichowekwa na Waisraeli wa kale na Wakristo wa karne ya kwanza. (Waefeso 5:19) Kama watumishi wa Mungu walioishi nyakati za Biblia, Mashahidi wa Yehova leo wanafurahia kuimba nyimbo zilizotungwa kishairi wakifuatana na muziki mtamu ili kumsifu Yehova.

[Picha katika ukurasa wa 23]

(Picha hizi hazionyeshi ukubwa halisi)

(Ona nakala iliyochapishwa)