Hamia kwenye habari

OKTOBA 23, 2019
JAPANI

Kimbunga Hagibis, Dhoruba ya Karibuni Zaidi Kupiga Japani

Kimbunga Hagibis, Dhoruba ya Karibuni Zaidi Kupiga Japani

Kimbunga Hagibis kilipiga Japani Oktoba 12 hadi 13, 2019, kikaua watu 77 hivi na kusababisha mafuriko makubwa. Hakukuwa na umeme wala maji katika maelfu ya nyumba. Bado maofisa nchini Japani wanaendelea kuwatafuta wale waliopotea. Kimbunga hicho kimekuwa kimbunga chenye nguvu zaidi kuwahi kupiga Japani tangu 1958, ambacho kimeambatana na mvua kubwa sana katika maeneo mbalimbali.

Ndugu zetu wote wako salama na hakuna yeyote aliyekufa katika kimbunga hicho. Hata hivyo, ndugu kumi walipatwa na majeraha madogo. Isitoshe, zaidi ya nyumba 1,200 za ndugu zetu ziliharibiwa. Jumla ya Majumba ya Ufalme 23 yaliharibiwa, na matatu kati ya hayo hayawezi kutumika kwa sababu ya mafuriko au kutokuwa na umeme. Jumba la Kusanyiko huko Tochigi lilipatwa na uharibifu mdogo.

Halmashauri za kutoa msaada ziliundwa katika majimbo ya Fukushima na Nagano. Huenda halmashauri nyingine zikaundwa baada ya kiwango cha uharibifu kuchanganuliwa. Akina ndugu walioathiriwa wanapokea msaada wa chakula na maji. Waangalizi wa mzunguko katika maeneo hayo wameombwa kutoa msaada wa kiroho na kuwatia moyo akina ndugu.

Tuna hakika kwamba Yehova ataendelea kuwa kimbilio kwa ndugu zetu katika kipindi hiki kigumu.—Zaburi 142:5.