JULAI 23, 2020
JAPANI
Mvua Kubwa na Mafuriko Yasababisha Uharibifu Japani Kusini
Mvua kubwa iliyonyesha mwanzoni mwa Julai 2020 imesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika kisiwa cha Kyushu, nchini Japani. Janga hilo limewaathiri zaidi ndugu na dada zetu wanaoishi katika majiji ya Minamata na Hitoyoshi yaliyo katika Jimbo la Kumamoto na jiji la Omuta katika Jimbo la Fukuoka. Hakuna Shahidi wa Yehova aliyekufa, ingawa ndugu mmoja na dada mmoja wana majeraha madogo. Kwa kuongezea, mafuriko hayo yameathiri nyumba 48 za ndugu zetu na Majumba mawili ya Ufalme. Majumba mengine mawili yameharibiwa na maporomoko ya ardhi.
Ofisi ya tawi ya Japani iliunda Halmashauri ya Kutoa Msaada kwa ajili ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) katika eneo la Kyushu na Okinawa. Halmashauri hiyo ndiyo sasa inatumiwa kushughulikia kazi ya kutoa msaada kwa walioathiriwa na mafuriko hayo. Wawakilishi wa Idara ya Usanifu-Majengo na Ujenzi pamoja na waangalizi wa mzunguko wanasaidia katika kazi ya dharura ya kutoa msaada.
Tunasali kwamba Yehova, “Mungu anayetoa uvumilivu na faraja,” aendelee kuwategemeza ndugu na dada zetu walioathiriwa na janga hili.—Waroma 15:5.