Hamia kwenye habari

NOVEMBA 26, 2014
JAPANI

Mashahidi wa Yehova Wasaidia Waathiriwa wa Maporomoko ya Ardhi Huko Hiroshima

Mashahidi wa Yehova Wasaidia Waathiriwa wa Maporomoko ya Ardhi Huko Hiroshima

EBINA, Japani—Mvua kubwa huko Hiroshima ilisababisha maporomoko hatari ya ardhi ambayo yaliua watu 74 hivi na kuharibu nyumba za zaidi ya watu 1,600 asubuhi ya Agosti 20, 2014. Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Japani inaripoti kwamba hakuna Shahidi yeyote aliyekufa au kujeruhiwa, ingawa nyumba nane za Mashahidi ziliharibiwa.

Nyumba iliyoharibiwa huko Hiroshima.

Mvua kubwa ya kiasi cha milimita 218 ilinyesha kwa muda wa saa tatu tu, na kusababisha uharibifu mkubwa ambao ulifanya serikali ianzishe mpango wa kuokoa watu. Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Japani ilipanga mara moja kuwe na halmashauri ya kutoa msaada na ikapanga kwamba Mashahidi waliojitolea wasaidie kuondoa uchafu. Vikundi hivyo vya kuondoa uchafu vilifanya kazi kwa kusimama katika mstari na kupokezana ndoo zenye uchafu na matope kutoka ndani ya nyumba hizo. Wajitoleaji walisafisha pia maeneo yaliyoondolewa uchafu baada ya kuhifadhi vyombo ambavyo havikuharibiwa na maporomoko hayo.

Mashahidi wakitoa matope na uchafu ndani ya nyumba za watu.

Gazeti la taifa Yomiuri Shimbun liliripoti kuhusu jitihada za Shahidi wa Yehova ambaye aliokoka msiba huo. Liliripoti kwamba Kayoko Nakamizo, mwanamke anayeishi katika wilaya ya Yagi kwenye Kata ya Asaminami, alikimbia kutoka katika nyumba yake na kisha “kubisha milango ya jirani zake, ili kuhakikisha kama walikuwa salama.” Kayoko alifaulu kuokoa jirani mmoja na kuwasaidia wengine kuondoka katika eneo hilo la msiba.

Ichiki Matsunaga, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Japani, anasema: “Tunasikitika pamoja na walioathiriwa na maporomoko hayo. Licha ya hali hiyo ngumu, tunadumisha mtazamo unaofaa tunapoendelea kutoa msaada unaohitajiwa na faraja kwa jirani zetu.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Japani: Ichiki Matsunaga, simu +81 46 233 0005